na Aron Msigwa-MAELEZO
Taasisi
ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono kauli
iliyotolewa hivi karibuni na Sheikh mkuu wa Tanzania, Mufti
Issa Shaaban Simba ya kuwataka waislamu na watanzania kote nchini kushiriki kikamilifu katika Sensa ya watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26 mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya mwenyekiti
wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania Sheikh Hamis
Mattaka amesema hatua hiyo inafuatia kuwepo kwa baadhi ya makundi
yanayowahamasisha waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kutoshirika
zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Amesema wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo la zoezi hilo kutokana na umuhimu wake kwa taifa na kuongeza kuwa Sensa ya watu na makazi ipo kwa mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jopo hilo limeiomba
serikali kuweka sheria itakayozuia utoaji wa takwimu zinazohusu dini za
watanzania zinazotolewa na vyanzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa
kuwa kipengele hicho si sehemu ya sensa nchini.
“Tunajua
kuwa serikali ilikua na nia njema kukiondoa kipengele cha dini katika
Sensa hapana budi nia njema hiyo ya serikali ilindwe kwa kuweka sheria
itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za watanzania” amesema Sheikh
Mattaka.
Amefafanua
kuwa Sensa ya awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilihusishwa na
baadaye kuondolewa katika Sensa zilizofuata kwenye madodoso ya
kukusanyia takwimu za kaya.
“Sisi kama jopo kila siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa nchi hii ni wajibu wetu kuheshimu
na kufuata sheria kwa maana ya kutii sheria bila shuruti, kwa hiyo
tunasema Sensa ya watu na makazi ni jambo la kisheria si jambo la
mitaani, hatuwezi kulumbana na kujadili jambo ambalo liko wazi kisheria
na limepitishwa na wabunge tuliowachagua sisi wenyewe”
Amefafanua
kuwa zoezi la Sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga
mipango ya maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na makazi, hali
ya kipato cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha serikali kwapatia
huduma bora wananchi wake.
Katika
hatua nyingine jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania
imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukusanyaji
wa maoni ya katiba.
Aidha
jopo hilo limewataka watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hiyo
muhimu kutoa maoni ambayo yataiwezesha nchi kupata katiba itakayokidhi
matakwa ya wananchi.
“
Sisi kama jopo la wanazuoni wa kiislamu tunawataka waislamu na
watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hii muhimu kwa kutoa maoni
yao ili hatimaye nchi yetu ipate katiba itakayokidhi matakwa ya
wananchi kwa miaka mingi ijayo” amesema Sheikh Mattaka.
No comments:
Post a Comment