Nahodha
wa Taifa Stars, Juma Kaseja na msaidizi wake Aggrey Morris wameng’ara
katika hafla ya kampuni ya Vodacom kukabidhi zawadi kwa wachezaji,
klabu, waamuzi na makocha waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom
msimu wa 2011/2012.
Katika
hafla hiyo iliyofanyika jana usiku (Juni 30 mwaka huu) hoteli ya Double
Tree Hilton, Dar es Salaam, Morris anayechezea Azam aliibuka mchezaji
bora wa ligi hiyo wakati Kaseja anayedakia Simba alikuwa kipa bora.
Kila
mmoja alizawadiwa sh. 3,312,500 katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi
alikuwa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye. Kaseja aliwashinda makipa
Mwadili Ally (Azam) na Deogratias Munishi (Mtibwa Sugar) wakati Morris
aliwashinda Haruna Niyonzima (Yanga) na Haruna Moshi (Simba).
John
Bocco wa Azam aliyefunga mabao 19 ndiye mfungaji bora, refa bora ni
Martin Saanya kutoka Morogoro ambaye aliwashinda Oden Mbaga (Dar es
Salaam) na Amon Paul (Mara) wakati kocha bora ni Stewart Hall wa Azam
aliyewashinda Charles Kilinda (JKT Ruvu) na Charles Mkwasa (Ruvu
Shooting). Kila mshindi mepata sh. 3,875,000.
Timu
yenye nidhamu bora ni Azam iliyopata sh. 7,750,000, mshindi wa tatu
Yanga sh. 15,500,000, makamu bingwa Azam sh. 22,000,000 na bingwa Simba
sh. 50,000,000.
Pia
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewazawadia sh. 1,000,000
kila mmoja kwa wachezaji watatu vijana wenye umri chini ya miaka 20
waliofanya vizuri kwenye ligi hiyo.
Wachezaji
hao ambao walikuwa kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao ni Frank
Domayo (JKT Ruvu), Rashid Mandawa (Coastal Union) na Hassan Dilunga
(Ruvu Shooting).
Wakati huohuo michuano ya Copa Coca Cola inaendelea
MARA YAKIONA CHA MOTO COPA COCA-COLA
Timu
ya Mara imeuanza vibaya mwezi Julai baada ya leo asubuhi kupata kipigo
cha mabao 5-0 mbele ya Dodoma katika mechi ya michuano ya Copa
Coca-Cola iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Dodoma
ambayo hiyo ni mechi yake ya nne mfululizo kushinda katika kundi hilo
la C ilipata mabao yake kupitia kwa Vicent Tarimo aliyefunga dakika ya
kwanza, Japhet Lunyungu (dakika ya sita), Ayoub Khalfan (dakika ya 65
na 89) na Abdul Madwanga (dakika ya 67).
Kundi
A limeshuhudia Ruvuma ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Kusini
Pemba katika mchezo uliofanyika leo asubuhi (Julai Mosi mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na
Sunday Leonard (dakika ya nne) na Shanely Michael (dakika ya 44).
Abdulatif Salim aliifungia Kusini Pemba dakika ya 90.
Nazo
Iringa na Tanga zimetoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kundi B
iliyochezwa Uwanja wa Tamco ulioko mkoani Pwani. Kagera imeitambia
Tabora baada ya kuifunga mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa
Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam. Athuman Kassim na
Shabani Ramadhan ndiyo walioifungia Kagera dakika ya sita na 88.
No comments:
Post a Comment