Wazazi nchini wametakiwa kutoa elimu ya uzazi na ujinsia kwa watoto wao ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kipindi cha kubalehe.
Wito huo umetolewa leo na mke wa Rais Mama Salma
Kikwete wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa Chama
cha uzazi na malezi bora Tanzania (UMATI) unaofanyika katika hoteli ya
Blue Pearl jijini Dar es Salaam .
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema kuwa miaka ya nyuma jamii ilikuwa inampa mtoto mafunzo
maalum mara baada ya kubalehe mafunzo hayo yaliweza kumsaidia mtoto
kuepukana na mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na yale yanayopelekea upatikanaji wa ujauzito.
“Mtoto
anaweza kupata ujauzito kutokana kwa kutofahamu elimu ya uzazi na
kutambua mabadiliko ya mwili wake, ikitokea kwa bahati mbaya amepata
ujauzito wazazi washirikiane kwa pamoja kuhakikisha kuwa mtoto anarudi
shule na kupata elimu, jukumu hili wasiachiwe kina mama peke yao”,
alisema Mama Kikwete.
Kuhusiana
na vifo vinavyotokana na uzazi hapa nchini Mama Kikwete alisema kuwa ni
vifo 454 katika vizazi hai laki moja lakini idadi ya vifo hivyo inaweza
kupungua iwapo huduma na elimu kuhusu afya ya uzazi na uzazi wa mpango
itawafikia wanawake wengi zaidi.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema, “Ninawashukuru UMATI kwa kazi nzuri mnayoifanya ya
kutoa elimu na huduma bora za afya ya uzazi na ujinsia aidha nawasihi
muongeze bidii na kasi ya kuzifikisha huduma hizi karibu zaidi na
wananchi wanaozihitaji hususan maeneo ya vijijini ambako watanzania
wengi wanaishi”.
Akiongea
kuhusu jitihada zinazofanywa na UMATI za kumuwezesha mtoto wa kike
Josephine Mwankusye ambaye ni Mkurugenzi mtendaji alisema kuwa wameweza kuwapatia elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kupitia vituo vya vijana na kliniki zao na katika kipindi cha mwaka 2012 waliwafikia watoto wa kike zaidi ya laki mbili na nusu.
Aliendelea kusema kuwa wanatengeneza mazingira mazuri kwa mtoto wa kike ili aweze kujimudu katika maisha na kutokuwa tegemezi, elimu ya ujasiliamali hutolewa kwa vijana na baadaye hupewa mitaji
midogo midogo na kutoa mfano wa kituo chaTemeke ambako watoto wa kike
walioacha shule baada ya kupata ujauzito wameweza kusaidiwa kutekeleza
shughuli za kuwapatia kipato kama vile uokaji wa mikate, utengenezaji wa
batiki, ushonaji na kozi ya usimamizi wa hoteli.
Mwankusye alisema, “Kupitia mradi wa vijana wa kike walio katika sekta zisizo rasmi kwa kipindi cha mwaka 2008 - 2012 vikundi 14 vilipatiwa elimu ya ujasiliamali na kupewa mtaji wa shilingi laki saba kwa kila kikundi katika mkoa wa Kilimanjaro”.
Alimalizia
kwa kusema kuwa wanatetea haki za mtoto wakike katika mlengo wa elimu,
afya na kutokomeza vitendo vya ukatiki. Pi wamekuwa mstari wa mbele
katika kutetea ubadilishwaji wa sera ya elimu ili mtoto wa kike
anayepata ujauzito akiwa shuleni aruhusiwe kuendelea na masomo mara tu
anapojifungua..
UMATI ilianzishwa mwaka 1959 na kujikita katika kutoa elimu na huduma mbalimbali za afya ya uzazi. Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Elimu na Afya ya Uzazi ni Haki ya mtoto wa kike, Timiza wajibu wako”.
No comments:
Post a Comment