MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Tuesday, November 1, 2011

EXIM BANK YAKUBALI KUSAIDIA MITAJI YA UWEKEZAJI NJE YA NCHI

Mwenyekiti wa bodi wa Benki ya Exim Tanzania Yogesh Manek akizungumza Dar es Salaam jana na washiriki wa mkutano wa uwekezaji kwa wawekezaji wazalendo (hawapo pichani) uliodhaminiwa na kuratibiwa na benki hiyo kwa malengo ya kuwapanua mawazo wawekezaji wa nchini katika kupata uthubutu wa kuwekeza mitaji yao nje ya Tanzania. Mada za mkutano huo zilitolewa na wataalamu wa Kampuni ya ushauri wa mambo ya kifedha ya India Infoline Group (IIFL Group) ya India.
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Exim Tanzania imesema ipo tayari kusaidia mitaji ya uwekezaji kwa wawekezaji wazelendo kuwekeza nje ya Tanzania katika kuongeza tija na kupanua wigo wa shughuli za kibiashara wanazofanya.
Pamoja na faida binafsi kwa wawekezaji husika pia uwekezaji nje ya Tanzania utasaidia kuinuka kwa taasisi za kifedha nchini kwa pamoja na uchumi wa nchi kutokana na muingiliano wa biashara baina ya pande husika.
Hayo yalibainishwa katika mkutano wa uwekezaji kwa wawekezaji wazalendo uliodhaminiwa na kuratibiwa Benki ya Exim Tanzania chini ya Kampuni ya Ushauri wa mambo ya kifedha ya India Infoline Group (IIFL Group) ya India na kushirikisha wawekezaji wa kitanzania katika sekta mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano huo Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa bodi wa benki hiyo Yogesh Manek alisema ni jukumu la benki hiyo kuhakikisha watanzania wanapata fursa ya kupanua wigo wa uwekezaji wa biashara zao.
Alisema kupitia mkutano huo anaamini washiriki husika watakuwa na uthubutu wa kuwekeza nje ya Tanzania kwa wigo mpana zaidi na kwamba benki hiyo ipo tayari kuwasaidia kufikia malengo husika.     
"Exim imeendelea kujijenga tangu kuanzishwa kwake na inachukua nafasi hii kuwapa nafasi watanzania kupanua elimu waliyonayo kuhusu uwekezaji ndani na nje ya Tanzania na tunaamini kupitia mkutano huu wengi mtapata pa kuanzia au pa kuendelea kupiga hatua," alisema Manek.
Mada zilizowasilisha katika mkutano huo na wataalamu kutoka kampuniya IIFL Group ni pamoja na dhana ya uwekezaji duniani,nafasi za uwekezaji nje ya Tanzania,mbinu za uwekezaji,kodi na mambo ya kisheria katika sekta ya kifedha na nafasi za uwekezaji nchini India.
Akiwasilisha mada ya uwekezaji duniani, mtaalamu Trivan Mathur alisema wigo mpana wa uwekezaji ni nguzo muhimu ya mafanikio iliyowainua wawekezaji katika maeneo mengi ya dunia.
Alisema kutokana na mabadiliko ya kiuchumi duniani wawekezaji wa kitanzania hawana budi kuangalia nafasi ya kufanya hivyo katika maeneo mengine na kwamba taasisi za fedha nyingi zipo tayari kuwainua watu wa aina hiyo.
Kwa upande wake mtaalamu Nicolas Duchene aliyewasilisha mada ya nafasi za uwekezaji nchini India alisema ni nafasi nyingine kwa watanzania kupanua biashara zao kwa kuwekeza nchini India.
Alisema India ni miongoni mwa nchi za Bara la Asia zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo hivyo kuwa na wigo mpana wa kuwekeza unaochagizwa na mazingira ya kuridhisha ya uwekezaji.
Benki ya Exim Tanzania imekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake ambapo pamoja na huduma za kibenki imekuwa na huduma nyingi za uwezeshaji ikiwemo ya mikopo na uwezeshaji wa wajasiriamali kupitia mpango wao wa WEF.

No comments:

Post a Comment