Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Napenda kuwatangazia wana-Bumbuli kwamba ile ahadi niliyotoa
wakati wa kampeni – ahadi ya kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli –
imetimia. Shirika limepata usajili,
limefungua ofisi, lina watumishi wa mwanzo na tayari ipo miradi minne ambayo
utekelezaji wake utaanza mara moja. Tutazindua Shirika hili tarehe 4 Agosti
2012, katika mkutano wangu na wana-Bumbuli waishio Dar es Salaam na mikoa ya
jirani, na baadaye katika mikutano na wananchi jimboni Bumbuli.
Chimbuko
Nilipoamua
kugombea Ubunge wa Bumbuli mwaka 2010, niliamua kwamba katika utumishi wangu
kama Mbunge nitashirikiana na Wana-Bumbuli pamoja na marafiki na washirika wa
maendeleo wa ndani na nje ya nchi katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii Bumbuli.
Jimbo letu ni kati ya majimbo yaliyo nyuma kimaendeleo kwa kiasi kikubwa na
hivyo kuhitaji jitihada za ziada – zaidi ya zile za Serikali. Katika kufikia
lengo hilo, niliahidi kuanzisha Shirika litakaloratibu shughuli za maendeleo
katika Jimbo.
Nilifikia
uamuzi wa kuanzisha Shirika nikitambua kwa dhati uwepo wa jitihada nzuri za serikali katika kuboresha
maisha ya watu wa Bumbuli nikitegemea pia serikali kuendeleza jitihada zaidi.
Hata hivyo natambua kwamba kazi ya maendeleo si kazi ya serikali pekee,
inahitaji ushiriki wa kila mmoja na hasa sekta binafsi ili kuisadia juhudi za
serikali kufikia malengo ya maendeleo. Nilitaka kuchambua uwezo wa watu
binafsi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali katika kupanua wigo wa ajira na
shughuli za kipato kwa watu wa Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii.
Mpango wa Mageuzi Bumbuli
Mpango huu ulitokana na mawazo niliyokuwa
nayo nilipoamua kugombea ubunge juu ya haja kuunganisha jitihada za wenyeji wa
Bumbuli, wafanyabiashara na taasisi za hapa nchini, na wawekezaji kutoka nje
katika kufanikisha mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Niliamini jitihada za sekta
binafsi zikioana na mipango ya maendeleo
ya serikali kutachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa wana-Bumbuli na hivyo
kupanua wigo wa ajira na shughuli za kibiashara za uzalishaji mali katika
Jimbo.
Malengo
ya mpango wa kuikwamua Bumbuli kupitia uwekezaji katika jamii ni kama
ifuatavyo:
1.
Kuongeza
pato la wakulima wa Bumbuli kutokana na mazao wanayovuna kwa kuboresha mbinu za
kilimo, mbinu za kuhifadhi mazao, na hatua mahsusi za kuongeza thamani ya mazao
hayo (value-addition).
2.
Kuwavutia
wawekezaji kujenga taasisi au shule itakayokuwa na wanafunzi, walimu na
wafanyakazi wengine watakaotumia bidhaa zinazozalishwa Bumbuli, hivyo
kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi.
3.
Kuleta
huduma za kifedha kwa kuanzisha taasisi ya fedha Bumbuli ambayo hatimaye
itakuwa benki ya wananchi wa Bumbuli ambayo itatoa mikopo kwa masharti nafuu.
4.
Kuchukua
hatua mahsusi za kuhifadhi mazingira ya Milima ya Usambara kwani maisha na
maendeleo ya kiuchumi ya watu wa Bumbuli yanategemea sana mazingira na mandhari
ya milima ya Usambara.
5.
Kuanzisha
Shirika la Maendeleo Bumbuli litakalokuwa na jukumu la kubuni, kuratibu na
kusimamia uendeshaji wa shughuli zilizoainishwa hapo juu. Shirika hili ndilo
litakalokuwa kiini cha mtandao wa kijamii wa uchumi kwa Bumbuli.
Malengo
haya yamekusudiwa kuwanufaisha wananchi kwa kuanzisha mtandao wa kimataifa wa
kibiashara ambapo wadau mbalimbali watashiriki; na hatamu za uchumi
zikishikiliwa na watu wa Bumbuli wenyewe.
Shirika la Maendeleo Bumbuli
Shirika
la Maendeleo ya Bumbuli ni shirika la maendeleo lisilotengeneza faida lenye
lengo la kukuza uchumi na kuchochea
maendeleo ya Jimbo. Shirika hili
limesajiliwa kama kampuni yenye ukomo wa dhamana, na litafanya biashara ili
kulipia gharama za uendeshaji na faida inayopatikana itatumika kugharamia
miradi ya maendeleo ili kufikia malengo ya kijamii ya Mkakati wa Mageuzi ya
Uchumi wa Bumbuli. Shirika litakuwa na kazi zifuatazo;
1.
Kuihamasisha
sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya Bumbuli kwa kuwekeza katika maeneo
mblimbali. Uwekezaji huu utahusisha
wafanyabiashara wa ndani na wale wa kigeni na Shirika litajihusisha zaidi
katika kutoa msaada wa kitaalamu, na kuratibu mtandao wa kibiashara utakaoenea
kuanzia ngazi ya wilaya, taifa na kimataifa.
2.
Kubuni
na kuitangaza ‘Chapa Lushoto’ (Lushoto Brand) pamoja na kutayarisha mafunzo kwa
wakulima juu ya kutayarisha mazao yao ili yapate kuwa na thamani bora zaidi.
Shirika hili litajenga mfumo utakaosaidia kununuliwa kwa mazao ya wakulima na
masoko ya bidhaa, muundo utakaotumiwa na wafanyabiashara binafsi.
3.
Kuvutia
uwekezaji kwa njia ya kuitangaza Bumbuli pamoja na kuishauri halimashauri na
serikali za mitaa kuhusu maeneo ya kuwekeza na miundombinu ya kuboresha ili
kuvutia uwekezaji zaidi.
4.
Kutafuta
fedha kwa ajili ya uwekezaji wa kijamii na kibiashara na kutoa msaada wa
kihuduma kwa makampuni ya biashara ya nyumbani na uwekezaji wa kutoka nje.
5.
Kuratibu
mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya wadau mbalimbali wa maendeleo
Bumbuli.
6.
Kuhamasisha
ushiriki wa wananchi katika mpango wa Maendeleo na Mpango wa uwekezaji.
Shirika
litaongozwa na bodi itakayokuwa na watu kati ya nane na kumi na moja na
kuendeshwa na timu ya watu watano ambao watakuwa ni, Mkurugegenzi Mtendaji,
Mweka Hazina, Wachambuzi wawili na Mhasibu.
Miradi ya Mwanzo ya Shirika la Maendeleo
Bumbuli
1.
Mradi wa
Kituo cha Kukusanya, Kusafisha, Kugredi, Kupaki na Kutafuta Masoko ya Mboga na
Matunda ya Bumbuli (Bumbuli Packing House)
Wilaya
ya Lushoto, jimbo la Bumbuli likiwemo, inasifika kwa kilimo cha mboga na
matunda. Hata hivyo, asilimia hamsini (50%) ya mboga na matunda yanayolimwa
Bumbuli yanaharibika – kwa kutokufika sokoni au kutopata soko la uhakika. Hata
yale mazao yanayonunuliwa, wakulima wanapata mapato kidogo sana ambayo
hayaendani na thamani ya jasho lao.
Mradi
wa Bumbuli Packing House, ambao utajiendesha kibiashara, una dhamira ya
kumaliza tatizo hili. Pamoja na hili mradi huu utawawezesha wakulima kwa
pembejeo – mbegu, mbolea, pampu, nk – na mafunzo ili wazalishe mboga na matunda
bora zaidi ya kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.
Mradi
huu, katika awamu ya kwanza, utagharimu shilingi milioni 780. Utafiti wa
Kibiashara (Market Analysis Survey) umefanyika, Andiko la Kibiashara
limekamilika. Na majadiliano na wadhamini kupata fedha hizi yamefikia mwisho
ambapo ndani ya mwezi mmoja fedha hizo zitapatikana, na baada ya maandalizi
kukamilika (ikiwemo kupata professional management), mradi utaanza.
2.
Mradi wa
Kiwanda cha Kusindika Mboga na Matunda
Shirika
liko katika hatua za mwisho za mazungumzo ya kukifufua upya kiwanda cha
kusindika Mboga na Matunda (Natural Choice) kilichopo Soni, jimbo la Bumbuli,
ambacho mwanzoni kwa miaka ya 2000 kilikuwa na sifa kubwa ya kutoa bidhaa
nyingi, bora na za thamani kubwa.
Mradi huu utaenda hatua ya
mbele zaidi ya Bumbuli Packing House kwa kutengeneza juisi, jams, concentrates
na bidhaa nyingine za mboga na matunda kwa ajili ya soko la ndani na nje ya
nchi. Mradi huu, sio tu utatoa ajira kwa watu wa Bumbuli, bali pia utahakikisha
soko la uhakika kwa mboga na matunda ya Lushoto linapatikana na kuongeza
thamani ya mazao ya wakulima na hivyo kuwaongezea kipato.
3.
Mradi wa
Kutoa Mikopo kwa Masharti Nafuu (Bumbuli Microfinance Institutition)
Jimbo
la Bumbuli halina tawi la benki yoyote na huduma ya fedha ni tatizo kubwa. Shirika
la Maendeleo Bumbuli limeomba leseni kutoka Benki Kuu kuanzisha taasisi ya
fedha kwa ajili ya ukopeshaji kwa masharti nafuu na pamoja na huduma nyingine
za fedha. Andiko la Mradi huu limefanywa kitaalam sana, baada ya utafiti wa
karibu miezi nane kuhusu njia muafaka ya kutoa huduma ya fedha kwa masharti
nafuu kwa watu wa Bumbuli. Mradi huu utagharimu shilingi milioni 450 kwa
kuanzia na baada ya miaka mitatu mtaji utaongezwa na kufikia shilingi bilioni
1.6. Wakati tunasubiri usajili na leseni kutoka Benki Kuu tayari wapo wafadhili
ambao, baada ya kusoma andiko letu, wameonyesha nia ya kusaidia mradi huu.
Msingi
wa mradi huu ni kuwezesha vikundi vya kuweka na kukopeshana fedha ambavyo
tayari vipo lakini vina mtaji mdogo, kutoa mafunzo ya fedha kwa vikundi hivi,
na kuhamasisha kuanzishwa kwa vikundi vingine. Kipaumbele na nafuu ya mikopo
itatolewa zaidi kwa vikundi vitakavyotumia fedha hizi kwa uzalishaji mali na
shughuli ambazo zitaajiri watu wengine.
4.
Mpango wa Malipo kwa Kufanya Vizuri
kwa Shule za Sekondari (Cash-On-Delivery for Secondary Education in Bumbuli)
Shirika la Maendeleo
Bumbuli (BDC) litakavyotekeleza program ya msaada ya Malipo kwa kufanya vizuri** au
cash on delivery (COD), ambayo itaongeza umakini na tija kwenye kujifunza
na matokeo ya mitihani katika shule za sekondari jimboni Bumbuli. Kulingana na
utafiti wetu, jimbo la Bumbuli liko kwenye hali ya kukata tamaa ya kupata
msaada kwenye Sekta yake ya Elimu ya Sekondari. Shirika la Maendeleo Bumbuli
(BDC) litatekeleza program ya majaribio
ya malipo kwa kufanya vizuri (COD), ya miaka mitatu ambayo itafanya malipo
kulingana na idadi ya wanafunzi ambao wamefaulu Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne. Shirika la Maendeleo Bumbuli
(BDC) linalenga kuboresha matokeo ya kujifunza/elimu katika jimbo la Bumbuli
kupitia program hii ya kutoa motisha. Program hii itahusu Shule za Sekondari za
Serikali za Kata.
Malipo kwa kufanya vizuri (COD) ni
utaratibu mpya kutoa msaada ambapo wafadhili
hutoa pesa kwenye maendeleo yanayopimika
kwa kuangalia matokeo maalum. Unahusianisha moja kwa moja malipo na
matokeo maalum, ikiwapatia watendaji/wapokeaji motisha ya kuongeza nguvu
zao za kufanyakazi ili kufikia maendeleo.
Msingi na uhalali wa wazo la CDO, ulioanzishwa awali
na Kituo cha Maendeleo ya
Kimataifa(Center for Global Development) mjini Washington, umejikita kwenye
mtazamo kwamba kazi za maendeleo ni lazima zitathminiwe kwenye athari (impact)
zinazoletwa. Mbinu inawakilisha mabadiliko kutoka kufuatilia nguvu na
rasilimali ambavyo mashirika huwekeza
katika kutoa misaada - 'nyenzo/rasilimali', na pia shughuli na
vifaa/vitendeakazi vinavyotokana na uwekezaji huo - 'matokeo'. Badala yake,
mbinu hii inalenga kujikita kuangalia namna gani maisha ya watu masikini
yameweza kubadilishwa kutokana na uwekezaji kwenye sekta au eneo fulani la
maendeleo (afya, elimu, n.k).
Mnamo mwezi
Septemba 2011, Shirika la Maendeleo Bumbuli lilifanya utafiti wa kina juu ya
mazingira ya kujifunzia Bumbuli na kugundua kwamba shule nyingi, walimu, na
wanafunzi wa Bumbuli hawana motisha wala rasilimali zinazohitajika kuwawezesha
wafanye vizuri kama inavyotarajiwa.
Kwa wastani, kila
shule iliyotoa data za matumizi ya pesa ilionyesha ni Sh. 5,268 kwa kila
mwanafunzi kwa mwaka 2010 (kiasi kilichotarajiwa kwa shule za Sekondari ni
shilingi 25,000 kwa kila mwanafunzi). Pamoja na hayo, utafiti ulionyesha kuwa
ni 71% tu ya walimu walikuwepo shuleni, ambapo ni 19% tu walikutwa madarasani.
Utafiti huo ulionesha kuwa walimu hupata mishahara yao kwa wakati. Wastani wa
mshahara halisi wa mwalimu wa Bumbuli ni Sh.395,000 kutoa malipo ya deni ya
Sh.74,000 kila mwezi. Wengi walionesha kuwa na shughuli ya ziada ya kiuchumi
(67%), hasa kilimo (90%). Wengi wao (98%) walidai kutokuhusishwa katika hatua
za kupanga bajeti za shule. Wastani wa Pato la Mtanzania anayeishi kijijini
(ikiwemo Bumbuli) ni Sh.152,000 (HBS, 2010). Wakati 89% ya wanafunzi wanaonesha
kushiriki katika shughuli za kiuchumi wa familia, bado 70% wanafanikiwa kupata muda
kidogo wa kukamilisha kazi zao za masomo wakiwa nyumbani, huku 34% inaonesha
hawakufika shule kwa mwezi uliopita kutokana na kusaidia shughuli za nyumbani. Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne ya mwaka
2011 kwa Shule za Bumbuli yalikuwa mabaya sana. Kati ya wanafunzi 1,327
waliofanya mtihani, hakuna aliyepata Division 1, waliopata Division 2 ni wanne,
waliopata Division 3 ni 39, na waliobakia, yaani wanafunzi 1,274, walipata Division 4 na 0.
Pamoja na hatua
mahsusi ambazo Serikali inachukua kuboresha elimu nchini na kuongeza ufaulu, Shirika
la Maendeleo Bumbuli, kupitia Program hii ya COD, linataka kuonesha kwamba
fedha zinaweza kugawika vizuri na kwa usahihi ili kuboresha elimu kwa kupima
kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Hatua na mikakati
inayopendekezwa
Program ya
COD kwa Shule za Sekondari Bumbuli
itahusisha makubaliano kati ya Shirika la Maendeleo Bumbuli, Shule za
Sekondari Bumbuli na Halmashauri ya Wilaya kulipa jumla ya kiasi cha Dola za
kimarekeni 100 kwa kila mwanafunzi anayefaulu mitihani ya kidato cha IV kwa
daraja la I-III. Malipo ya COD yatafanyika baada
ya uthibitisho wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne. Fedha zitapelekwa
Halmashauri ya Wilaya, Shule za Sekondari na kwa walimu na wanafunzi. Fedha
zitakazogawiwa kwa shule zitatumika kwa ajili ya mahitaji ya kielimu ya shule
kama zilivyowekewa vipaumbele na Bodi za Shule.
Watakaonufaika na mradi:
Kwa kila mwanafunzi atakayefaulu mtihani (Div
I-III) anapomaliza kidato cha nne, Shirika la Maendeleo Bumbuli kupitia program
ya COD litatoa malipo yafuatayo:
1. Walimu: Tsh 60,040/= kwa kila mwanafunzi anayefaulu
mtihani
2. Wanafunzi: Tsh 50,500/= Kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
3. Shule: Tsh 31,600/= Kwa kila mwanafunzi
anayefaulu mtihani
4. Halmashauri ya Wilaya: Tsh
15,800/= kwa kila mwanafunzi anayefaulu mtihani
Vipimo na Ukaguzi:
Data za mitihani
kuanzia mwaka 2011 zitatoa msingi wa awali, na msingi huo utakuwa ukibadilishwa
kila mwaka na ufanisi wa utendaji wa shule, hivyo kila mwaka unakuwa msingi kwa
ajili ya malipo ya mwaka ujao wa. Kiashiria cha matokeo kitakuwa idadi ya
wanafunzi ambao wamefaulu kidato cha nne kwa kupata daraja la I-III. Ili
kuyadumisha matokeo hayo, hatua mbalimbali zitakuwa vikiripotiwa kila mwaka na
shule na halmashauri. Mkataba, matokeo, na taarifa nyingine zitawekwa wazi kwa
wananchi ili kuongeza uwajibikaji wa wafadhili na wapokeaji
Shirika la
Maendeleo Bumbuli halina nia ya kusema kwamba COD ndio suluhisho pekee la
tatizo la maendeleo ya elimu au ufumbuzi wa matatizo yote katika mfumo
wa elimu nchini lakini tunaamini inaonesha matarajio ya kutosha kuona thamani
ya kujaribu, kujifunza na kutathmini.
Uendelevu wa program
Ili program iwe endelevu, Shirika la Maendeleo
Bumbuli(BDC) litaweka mfumo thabiti wa kufanya tathimini na kutoa mrejesho,
ambao utatumika kama zana ya kupimia uwajibikaji, na kuendeleza uwazi. Pia ni
muhimu kuzingatia ushirikishwaji wa wenyeji wa Bumbuli na umiliki wa program ya
COD. Hili linaweza kufanikiwa kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha elimu bora
kama uwekezaji wa wenyeji, na Mtandao wa Wahitimu wa Shule za Sekondari Bumbuli
kwa ajili ya fedha za COD. Zaidi sana, Shirika la Maendeleo Bumbuli litahusisha
na kutumia Bodi za Shule, ambazo zinahusisha wazazi na walimu. Hii ndiyo njia itakayowafanya
watu wa Bumbuli wathamini juhudi zao wenyewe katika kuboresha jamii zao.
5. Kambi ya
Wanafunzi Wanaojiandaa na Mtihani wa Kidato cha Nne 2012
Kuanzia tarehe 4 Agosti hadi 5 Septemba,
wakati wa likizo za masomo, Shirika limeandaa kambi maalum kwa matayarisho ya
vijana wanaojiandaa na mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu. Kambi hii itakuwepo
kwenye Kituo cha Elimu Soni, ambacho kina mandhari, mazingira na eneo la
kutosha kufundishia na kuishi wanafunzi katika kipindi hiki.
Kila siku, wanafunzi hao watapigwa msasa kwa
masomo ambayo hawakupata fursa ya kuyasoma vizuri katika mwaka wa shule,
watafundishwa mbinu za kufanya mitihani (ikiwemo time-management), na kufanya
revision ya mitihani ya Kidato cha Nne ya kuanzia mwaka 1984 hadi sasa. Shirika
litatafuta walimu wenye sifa za kufundisha masomo ya Hesabu, Kiingereza,
Historia, Kemia, Fizikia na Biolojia, hata nje ya Jimboni na kuwalipa posho
kuja kufundisha kwenye kambi. Pia tutaomba watu mbalimbali, ikiwemo walimu
wastaafu, wenye moyo wa kujitolea waje kufundisha kambi hii.
Mwisho
Hadi sasa Shirika la Maendeleo Bumbuli halijapata mfadhili au ufadhili
kutoka kokote au kwa mtu yoyote. Miradi hii niliyoitaja ndio iko katika hatua
za kupata ufadhili. Fedha ambazo zimetumika hadi sasa kuanzisha Shirika, kuweka
ofisi, kuajiri watumishi wa muda na kufanya utafiti na kutengeneza maandiko ya
miradi zimetokana na mkopo niliouchukua kama Mbunge, ikiwemo mkopo wa gari
ambao sikuutumia kununua gari bali kuanzisha Shirika.
Napenda kutoa mwito kwa wana-Bumbuli wenzangu na Watanzania kwa ujumla
kusaidia kuchangia maendeleo ya Jimbo la Bumbuli, hasa kwa miradi ambayo hatukuitafutia ufadhili kama huu wa COD na
kambi. Kwa kuchangia unaweza kutumia
namba ya M-PESA 0762088050. Kwa maelezo zaidi kuhusu Shirika la Maendeleo
Bumbuli, tuma barua pepe: getinvolved@bumbuli.org au piga simu: +255 22 2129821/6 au tuma fax: +255 22 2129796
Katika miezi ijayo, BDC pia itatekeleza miradi ya
kitaifa yenye manufaa kwa maendeleo na utawala bora kwa nchi yetu. Naamini nchi
yetu itapiga hatua za maendeleo kwa kasi zaidi kama kila mmoja wetu, kwa nafasi
na uwezo wake, atathubutu, lakini pia kama sote tutasaidiana katika kuchangiana
na kupeana mawazo kuhusu shughuli za maendeleo.
January Makamba
Mbunge Bumbuli
8 Julai 2012
No comments:
Post a Comment