MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Wednesday, April 10, 2013

HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2013/2014





UTANGULIZI

1.            Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na Taarifa zilizowasilishwa leo na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya ndani ya Bunge lako Tukufu ambazo zimechambua Bajeti ya Mafungu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2012/2013 na Mwelekeo kwa mwaka 2013/2014. Vilevile, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2013/2014.

2.            Mheshimiwa Spika,  awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kwa maslahi ya Nchi yetu. Mheshimiwa Rais ameiletea Tanzania sifa, heshima na kuiwezesha kutambulika zaidi Kimataifa katika Nyanja mbalimbali. Ziara ya kihistoria ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya Nchini tarehe 24 hadi 25 Machi 2013 ni ushahidi tosha wa kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais ya kukuza ushirikiano wenye maslahi ya kiuchumi kati ya Nchi yetu na Nchi nyingine. Katika ziara hiyo, Mikataba 16 ya ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ilitiwa saini. Utekelezaji wa Miradi hiyo utachochea uwekezaji na hivyo kuongeza kasi ya ukuaji uchumi na kupunguza umaskini.

3.            Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuwa Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge. Vilevile, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika Taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Ni matumaini yangu kwamba wote walioteuliwa na kuchaguliwa watatumia nafasi hizo kwa manufaa ya Bunge na kwa maendeleo ya Watanzania kwa ujumla. Hongereni Sana!

4.            Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala inayoongozwa na Mheshimiwa Pindi Hazara Chana, Mbunge wa Viti Maalum na Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa Nzega. Nawashukuru pia Wajumbe wa Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara inayoongozwa na Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini na Kamati ya Masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya inayoongozwa na Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o Mbunge wa Viti Maalum. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Mafungu ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mfuko wa Bunge. Aidha, nawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali Zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Maoni na Ushauri wao utazingatiwa wakati wa kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali na utekelezaji wake.
5.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012/2013, kumekuwa na majanga na matukio mbalimbali yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Miongoni mwa matukio hayo ni ajali mbaya ya Jahazi la Sunrise iliyotokea Wangwi katika Bahari ya Hindi mwezi Januari 2013 na ajali mbalimbali za vyombo vingine vya usafiri ambapo watu walipoteza maisha na wengine kupata majeraha. Hivi karibuni pia tumeshuhudia ajali  mbaya ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa  16  Jijini Dar es Salaam  ambalo limesababisha vifo vya  watu  34  na  tukio linguine ni vifo  13  vilivyotokana  na  kufukiwa  na  kifusi cha   moram’   katika  machimbo  ya   Mushono   Jijini  Arusha. Aidha, tumempoteza ghafla Mbunge mwenzetu, Mheshimiwa Salim Hemed Khamis, Mbunge wa Chambani na baadhi yetu tumepoteza Ndugu, wakiwemo wazazi na watoto kutokana na sababu mbalimbali. Wote nawapa Pole Sana!

Mzunguko Mpya wa Bajeti

6.            Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014, tumekubaliana kuanza Mzunguko Mpya wa Bajeti ambao utatuwezesha kukamilisha mjadala wa Bajeti ya Serikali  mapema.  Lengo  ni  kwamba ifikapo tarehe 30 Juni ya  kila mwaka, taratibu zote za kuandaa, kuchambua na kupitisha Bajeti  ya Serikali ziwe zimekamilika na utekelezaji  wa  Bajeti  kuanza  ifikapo  tarehe  1 Julai. Tofauti na miaka ya nyuma ambapo Bajeti ya Serikali ilikuwa ikijadiliwa na kupitishwa kwanza na kufuatiwa na Bajeti za Kisekta, sasa makadirio na matumizi ya Wizara yatajadilwa kwanza na hatimaye kuhitimishwa na majadiliano ya kina ya Bajeti ya Serikali. Moja ya faida kubwa ya utaratibu huu mpya ni kwamba, mwaka mpya wa fedha unapoanza utekelezaji  wa kazi za Serikali unaanza mara moja. Utaratibu huo utawawezesha Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge pamoja na Watendaji wa Serikali kurejea katika kazi zao na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Bajeti na Mpango wa Maendeleo. Kwa kuwa tunaanza kwa mara ya kwanza kutumia utaratibu huo hazitakosekana dosari chache ambazo  zitafanyiwa   kazi  kadri   tunavyoendelea  kuutumia.   
Nawaomba  Waheshimiwa Wabunge kutumia fursa hii kutoa maoni na ushauri utakaosaidia kuboresha Bajeti ya Serikali ili iwe bora zaidi na yenye maslahi makubwa kwa wananchi wetu.

7.            Mheshimiwa Spika, maandalizi ya Bajeti yamezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali chache tulizonazo ili kutekeleza Miradi ya Maendeleo ya Kipaumbele ambayo itachochea ukuaji wa haraka wa uchumi.

8.            Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bwana Ludovick Utouh, pamoja na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia rasilimali za Serikali. Matunda ya kazi hii yameonekana hadi nje ya Nchi na ndiyo maana Ofisi hii sasa imepandishwa hadhi kutoka Daraja la Kwanza hadi la Tatu kwa vigezo vinavyotumiwa na Muungano wa Ofisi za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika Bara la Afrika kwa Nchi zinazotumia Lugha ya Kiingereza.

 

HALI YA SIASA

9.            Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imepiga hatua ya kuridhisha katika kuimarisha Demokrasia ya Vyama vingi. Kwa ujumla hali ya kisiasa Nchini ni tulivu na Vyama vya Siasa vinaendelea kutekeleza majukumu yake. Idadi ya Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu imefikia 20 baada ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kupata usajili wa kudumu. Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) kilipata usajili wa muda na zoezi la uhakiki wa wanachama linaendelea. Chama cha Movement for Democratic and Economic Change kilifutwa baada ya kukosa sifa za kupata usajili wa kudumu.

10.         Mheshimiwa Spika, ili Demokrasia Nchini izidi kuimarika na Wananchi washiriki kikamilifu kwenye siasa, Viongozi wote wa Vyama vya Siasa wana wajibu mkubwa wa kuendesha Siasa za kistaarabu zinazozingatia maadili ya Kitanzania na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu. Wito wangu kwa Vyama vyote ni kuendelea kuvumiliana na kutohamasisha siasa za chuki au vurugu ambazo zitatugawa na kuhatarisha Amani, Utulivu na Umoja wetu ambao umewekezwa kwa miaka mingi. Mwenye Macho haambiwi Tazama. Wote ni mashahidi wa matatizo makubwa ambayo yamezikumba Nchi zilizoingia katika siasa za chuki na vurugu.

11.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaandaa mapendekezo ya kufanya mapitio ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010. Aidha, itaendelea na usajili wa Vyama vya Siasa, kutoa elimu ya Demokrasia kwa Wananchi na kuboresha Baraza la Vyama vya Siasa. Hatua hizo zitazidi kuimarisha Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini.

 

ULINZI NA USALAMA


Hali ya Mipaka ya Nchi

12.         Mheshimiwa Spika, kwa ujumla hali ya mipaka ya Nchi yetu ni shwari na Wananchi wanafanya shughuli zao bila vikwazo. Katika kuimarisha usalama wa mipaka yetu, Viongozi wa Mikoa ya Kagera, Kigoma, Rukwa na Tanga wamefanya vikao vya  ujirani  mwema  na  wenzao  wa  Mikoa  ya mipakani mwa Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Zambia na Kenya. Pamoja na hali nzuri ya usalama wa mipaka yetu, bado tunakabiliwa na changamoto  ya  Wahamiaji  haramu  wanaotumia   Nchi  yetu  kama  mapito ya kuelekea  Nchi nyingine au kufanya makao Nchini.  Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali inaendesha misako ya kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria.  Serikali pia, imeendelea kutoa elimu kwa Wananchi wa Mikoa ya mipakani ili kutoa taarifa za Wahamiaji haramu. Natoa wito kwa Wananchi wote kushirikiana na Serikali kuwabaini na kuwafichua wahamiaji haramu na wale wanaowasafirisha ili wachukuliwe hatua stahiki za Kisheria.

 

Hali ya Uhalifu Nchini

13.         Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na jamii kupitia dhana ya Ulinzi Shirikishi inafanya kazi nzuri ya kudhibiti vitendo vya uhalifu Nchini. Jumla ya makosa makubwa ya jinai yaliyotolewa taarifa katika Vituo vya Polisi Nchini yalipungua kutoka 69,678 mwaka 2011 hadi 66,255 mwaka 2012. Katika kipindi cha Januari hadi Februari 2013 makosa ya jinai yalikuwa 10,548 ikilinganishwa na makosa 10,989 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Jeshi la Polisi pia limedhibiti kwa kiasi kikubwa uingizaji wa silaha haramu ambapo jumla ya silaha 405 zilikamatwa katika operesheni mbalimbali kati ya Januari na Desemba 2012. Natumia fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi nzuri ya kutekeleza kikamilifu dhana ya Ulinzi Shirikishi na kuwahamasisha Wananchi kuhusu Utii wa Sheria bila Shuruti. Aidha, napenda kuwakumbusha Wananchi wote kwamba, suala la Ulinzi na Usalama wa Nchi yetu ni jukumu letu sote. Ni wajibu wetu kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu kwa Jeshi letu ili hatua za kudhibiti vitendo hivyo zichukuliwe.

 

 

 

Mauaji ya Kishirikina

14.         Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi za Serikali za kuwahudumia wazee na watu wenye ulemavu, siku za karibuni kumeibuka tena dalili za vitendo vya ukatili dhidi ya wazee, wanawake  na  walemavu wa ngozi katika baadhi ya Mikoa kwa sababu za kishirikina. Ukatili huo siyo tu unyama uliopindukia kwa Binadamu wenzetu bali pia unaondoa sifa kubwa  ya  jamii  yetu  ya kupendana  pasipo  kujali  rangi, dini au kabila. Nitumie  fursa  hii  kuwahakikishia ndugu  zetu wenye ulemavu wa ngozi, akina mama na wazee kwamba, Serikali haitavumila kuona ukatili wowote unafanywa dhidi yao.

Naziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya zote Nchini kwa kushirikiana na Jamii kuwabaini na kuwafikisha kwenye Vyombo vya Sheria wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu.

 

Migogoro ya Dini

15.         Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa uhuru kwa Wananchi wake kuabudu, kila mtu kwa Dini anayoitaka. Hata hivyo, hivi karibuni kumejitokeza migongano na chokochoko za kidini ambazo zimeanza kueneza chuki miongoni mwetu. Chokochoko zinazojitokeza si dalili nzuri kwa mustakabali wa Nchi yetu inayopenda  kudumisha  Amani,  Utulivu  na  Umoja  wa  Kitaifa.
Uzoefu wa Mataifa mbalimbali umeonesha kwamba chokochoko za kidini zimesababisha machafuko makubwa na kutoweka kwa amani katika Nchi hizo. Tukumbuke kwamba yakitokea machafuko ya namna hiyo na kuvurugika kwa amani na utulivu, hakuna atakayesalimika. Hivyo, natoa wito kwa Viongozi wa Madhehebu ya Dini kuelimisha Waumini wao kuthamini na kuheshimu dini za wengine na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoamsha hisia za chuki miongoni mwa wafuasi wa Dini mbalimbali.

Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa

16.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali iliahidi kukarabati na kujenga Makambi kwa ajili ya kuchukua Vijana watakaojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria. Ninayo furaha kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imetekeleza ahadi ilizotoa mwaka jana kwa ufanisi mkubwa. Mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria yameanza mwaka huu kwa kuchukua Vijana 4,711 sambamba na Vijana 5,893 wa kujitolea wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Nitumie fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge vijana waliojiunga na mafunzo ya JKT mwaka huu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuchukua vijana kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.

 

SHUGHULI ZA UCHAGUZI, BUNGE, VITAMBULISHO VYA TAIFA, SENSA NA MUUNGANO


Tume ya Taifa ya Uchaguzi

17.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliendesha Chaguzi Ndogo za Madiwani katika Kata 29 Tanzania Bara ili kujaza nafasi wazi za Viti vya Udiwani. Katika chaguzi hizo, Chama Cha Mapinduzi kilishinda Viti 22, CHADEMA Viti 5 na CUF na TLP Kiti kimoja kimoja. Vilevile, Tume ilifanya teuzi 15 ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi za Udiwani wa Viti Maalum. Katika uteuzi huo, CCM ilipata viti 10, CHADEMA viti vinne na TLP kiti kimoja. Katika mwaka 2013/2014, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaboresha Daftari la Wapiga Kura ambapo Awamu ya Kwanza itakamilika mwezi Desemba, 2013. Uboreshaji huo utawezesha kuchapishwa kwa Daftari la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

18.         Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2014. Kazi za awali za uchaguzi huo zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kupitia upya Kanuni za Uchaguzi zitakazojumuisha maoni ya wadau mbalimbali. Ili kufanikisha uchaguzi huo, Halmashauri zote Nchini zinatakiwa kuanza maandalizi mapema kwa kupitia na kuhakiki orodha ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa.  Baada ya kuhakiki orodha hiyo, maombi mapya ya kugawa Vitongoji, Vijiji au Mitaa yawasilishwe katika ngazi husika kabla ya tarehe 31 Desemba 2013 kwa kuzingatia Sheria na Taratibu zilizopo.

Shughuli za Bunge

19.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Bunge limeendelea kutekeleza majukumu yake ya kuisimamia na kuishauri Serikali katika nyanja mbalimbali. Aidha, Bunge limefanya Mikutano  mitatu, kupitisha Miswada minne ya Sheria  na  kuridhia  Maazimio nane. Katika kuboresha utendaji wa Kamati za Kudumu za Bunge, Wajumbe wa Kamati hizo walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo ili kumudu majukumu yao vizuri katika nyanja za utafiti, uchambuzi wa Miswada, Sera na Bajeti, utunzaji wa kumbukumbu na taratibu za uendeshaji wa Bunge. Vilevile, kuanzia tarehe 4 hadi 7 Desemba 2012 Bunge liliandaa kwa mafanikio Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani uliofanyika Dar es Salaam ukiwa na kauli mbiu ya “Vita dhidi ya Ukatili wa Wanawake”.

20.         Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi, Kamati za Kudumu za Bunge zimefanyiwa mabadiliko makubwa kwa kuunda Kamati mpya ya Bajeti na kugawanya baadhi ya  Kamati. Iliyokuwa Kamati ya Nje, Ulinzi na Usalama imegawanywa mara mbili na kuwa Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati  ya  Ulinzi na  Usalama. Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala imegawanywa na kuwa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala na Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.  Vilevile, Kamati zilizokuwepo awali nazo zimeundwa upya na baadhi kuongezewa majukumu. Ni imani yangu kwamba Kamati hizo, zitatekeleza wajibu wake kikamilifu kwa maslahi ya Taifa.

 

Muungano

21.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kuratibu masuala yote ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa lengo la kudumisha Muungano na ushirikiano wa Serikali  zote mbili. Katika kudumisha  ushirikiano huo, Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ cha kushughulikia Masuala ya Muungano kilifanyika na kujadili Hoja zinazohusu utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; ushiriki wa Zanzibar katika Taasisi za Nje na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; Ongezeko la gharama za umeme wa TANESCO kwa ZECO; Usajili wa vyombo vya moto, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili na mgawanyo wa mapato.

 

Mabadiliko ya Katiba

22.         Mheshimiwa Spika, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea kuratibu, kukusanya na kuchambua maoni ya Wananchi ili kupata Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na ridhaa ya Wananchi wenyewe ifikapo mwaka 2014. Katika mwaka 2012/2013, Tume imekusanya maoni ya Wananchi kupitia njia mbalimbali na kuanza uchambuzi wa maoni yaliyotolewa ili kuandaa Rasimu ya Katiba. Tume pia, imeanza maandalizi ya kuunda Mabaraza ya Katiba katika Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Katiba yanayojumuisha Asasi, Taasisi na Makundi Maalum ya Watu. Mabaraza hayo yatakuwa na jukumu la kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume. Mabaraza ya Katiba yatawashirikisha na kuwakutanisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya wananchi katika jamii. 

23.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Tume itaratibu, Mikutano ya Mabaraza ya Katiba Mpya, kuchambua maoni  ya  Mabaraza  ya  Katiba  na  kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya itakayowasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba. Vilevile, itachapisha Katiba iliyotokana na maoni ya Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kupigiwa Kura ya Maoni. Naipongeza sana Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi sasa. Nawasihi Watanzania wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume ili iweze kukamilisha kazi hii muhimu kwa Taifa letu.

Sensa ya Watu na Makazi 2012

24.         Mheshimiwa Spika, mwaka 2012 ulikuwa ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi ambayo ni ya tano kufanyika tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Matokeo yanaonesha kuwa idadi ya watu Nchini imeongezeka kutoka watu milioni 34.5 mwaka 2002 hadi milioni 44.9 mwaka 2012. Hilo ni ongezeko la watu Milioni 10.4 kwa kipindi cha miaka kumi, sawa na ukuaji wa wastani wa Asilimia 2.7 kwa mwaka. Kwa ujumla matokeo ya Sensa yanaonesha kasi ya ongezeko la watu ni kubwa ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa. Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali pamoja na mambo mengine inaendelea kutekeleza Sera ya Idadi ya Watu ya mwaka 2006 kwa kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa Uzazi wa Mpango. Nitumie fursa hii kulikumbusha Bunge lako Tukufu na Watanzania kazi ya uchambuzi wa takwimu inaendelea ili kupata mchanganuo wa kina zaidi utakaoiwezesha Serikali kupanga vizuri Mipango yake ya Maendeleo. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itasambaza taarifa mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi zenye mchanganuo wa kitakwimu na kuhamasisha matumizi yake  katika tafiti na kuandaa Mipango ya Maendeleo katika ngazi zote.

Vitambulisho vya Taifa

25.         Mheshimiwa Spika, Tarehe 07 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu, Jijini Dar es Salaam. Vilevile, tarehe 13 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamedi Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alizindua Zoezi hilo kwa upande wa Zanzibar. Kuzinduliwa rasmi kwa mfumo huo ni mwanzo wa utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia kuwatambua na kuwahudumia Wananchi ipasavyo. Zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa linaendelea kwa watumishi wa umma waliokuwa wamesajiliwa na kuhakikiwa. Zoezi la kuingiza taarifa za Wananchi 220,000 kwa ajili ya kupatiwa Vitambulisho vya Taifa katika Wilaya ya Kilombero iliyoteuliwa kuwa Wilaya ya mfano limekamilika na uchambuzi wa taarifa za Wakazi wa Dar es Salaam 2,159,822 waliojiandikisha zinaendelea. Aidha, Wakaazi wa Zanzibar 160,645 na Wageni 180 wameandikishwa. Kazi ya Utambuzi na Usajili wa Watu katika Mikoa mbalimbali Nchini inaendelea sambamba na utoaji wa Vitambulisho kwa wale walioandikishwa na kuhakikiwa.

 

MASUALA YA UCHUMI


Hali ya Uchumi

26.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Pato halisi la Taifa lilikua kwa Asilimia 6.9 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.4 mwaka 2011. Sekta zilizochangia zaidi katika ukuaji  huo ni pamoja na Mawasiliano, Fedha, Viwanda, Ujenzi, Madini, Biashara na Utalii. Kutokana na ukuaji huo, Wastani  wa  Pato la  Mtanzania  umeongezeka  kutoka Shilingi 869,436 mwaka 2011 hadi Shilingi 995,298 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Asilimia 12.6. Mfumuko wa Bei umepungua kutoka  Asilimia 19.4 mwezi  Februari  2012 hadi  Asilimia 9.8 mwezi  Machi  2013. Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa na jitihada za Serikali za kuongeza usambazaji wa vyakula kwenye masoko, kupunguza ujazi wa fedha kwenye soko, kudhibiti upandaji wa bei ya mafuta ya petroli na kuimarika kwa upatikanaji wa umeme viwandani ikilinganishwa na mwaka 2011/2012.

Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano

27.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa  Miaka Mitano ambao ulipitishwa na Bunge lako Tukufu Mwaka 2011/2012. Katika kutekeleza Mpango huo, Tume ya Mipango imeweka utaratibu  wa  kuchambua kwa kina maandiko ya miradi yote ya kisekta ili  kuhakikisha kwamba imezingatia vipaumbele ambavyo sote tumekubaliana. Baada ya uchambuzi huo, ndipo fedha hutolewa kwa ajili ya utekelezaji. Pamoja na utaratibu huo, Serikali imeona ni muhimu kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa kuanzisha Mfumo imara zaidi wa kupanga Vipaumbele, kufuatilia na kutathmini Utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati ya Maendeleo. Mfumo huo ambao utasimamiwa na Chombo Maalum (President’s Delivery Bureau) chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu, unazingatia uzoefu wa Nchi ya Malaysia. Chini ya Mfumo huo, Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa itatengewa fedha za kutosha na usimamizi wa kina utafanyika kuhakikisha kwamba malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

28.         Mheshimiwa Spika, ili Mfumo huo ufanikiwe inabidi kwanza wadau wote wakubaliane kimsingi vipaumbele ambavyo vitatoa matokeo makubwa na ya haraka na kisha wataalamu kutoka Serikalini, Sekta Binafsi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kukaa pamoja na kuchambua kwa undani vipaumbele hivyo, namna ya kuvitekeleza, kubaini watekelezaji na kuibua viashiria vya kupima matokeo. Tayari zoezi hilo la awali limefanyika ambapo maeneo sita ya kwanza ya kipaumbele yamefanyiwa uchambuzi wa kina kwa utaratibu unaojulikana kama Maabara (Labs). Utaratibu huo wa maabara unatoa fursa kwa wataalam na watunga Sera kukaa pamoja, kufikiri na kuendesha majadiliano ya wazi hadi pale wanapokubaliana  kwamba  ufumbuzi  wa  tatizo umepatikana.Maeneo yaliyojadiliwa katika awamu ya kwanza ni Nishati na Gesi Asilia, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Kupanua wigo wa Mapato ya Serikali. Baada ya uchambuzi huo kukamilika, matokeo yake ikiwemo miradi iliyoandaliwa pamoja na Bajeti ya utekelezaji itawekwa hadharani ili kila Mtanzania ajue kitakachofanyika, kutoa maoni na kufuatilia kwa kina utekelezaji.

29.         Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo na uwajibikaji wa kutosha katika kutekeleza vipaumbele vya Kitaifa, Chombo kitakachoanzishwa (President’s Delivery Bureau) kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba kila Waziri wa Kisekta na Watendaji Wakuu wanawajibika kusimamia  utekelezaji wa miradi ya kipaumbele na pia kufanya tathmini za mara kwa mara kupima matokeo. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mawaziri wanaosimamia maeneo sita ambayo tumeanza nayo walitoa ahadi kwamba watakuwa mstari wa mbele kusimamia kwa weledi utekelezaji  wa miradi ya Sekta zao. Ahadi hizo walizitoa wakati  wa  uzinduzi  wa awamu ya kwanza ya mfumo wa maabara uliofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais  wa  Jamhuri  ya  Muungano wa Tanzania  tarehe  22 Februari  2013. Ni matumani yangu kuwa, utaratibu huo utasaidia sana kuimarisha uwajibikaji, ufuatiliaji na hatimaye kupata matokeo ya haraka ambayo yatasaidia  uchumi  kukua  kwa  kasi  zaidi na hivyo kupunguza umaskini miongoni mwa watu wetu.  Ni vyema ieleweke wazi kwamba, maeneo ya kipaumbele yaliyochaguliwa yatapata sehemu kubwa ya fedha za maendeleo. Hii ndiyo maana ya dhana ya kupanga ni kuchagua na haina maana kwamba kazi nyingine za uendeshaji wa Serikali zitasimama. Katika Mwaka 2013/2014, kutafanyika uchambuzi wa kina wa maeneo mengine ya kipaumbele ambayo yatasaidia Serikali kupanga Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka 2014/2015.

Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji

30.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini. Lengo ni kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika shughuli za uwekezaji na Biashara Nchini. Katika utekelezaji wa Mpango Kazi huo, Serikali imeazimia kupunguza muda unaotumika kupitisha mizigo Bandarini na Mipakani kwa kuanzisha utaratibu wa kubadilishana taarifa zinazohusu mizigo kwa njia za kielektroniki kabla mizigo haijafika kwenye Vituo vya Forodha. Vilevile, Kamati za Pamoja (Joint Border Post Committees) zimeundwa kwenye Vituo vya Mipakani vya Tunduma, Kabanga, Mutukula, Holili, Sirari na Namanga. Kupitia Kamati hizo wadau wote wanaoshughulika na utoaji huduma mipakani hufanya kazi kwa pamoja.

31.         Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Mkakati na Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Vilevile, Mwongozo wa Utendaji kwa ajili ya kutekeleza Sera, Sheria na Kanuni za Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi umekamilika. Aidha, Serikali imefanya tathmini ya Sera zinazohusu Uwekezaji kwa kutumia Mfumo wa Tathmini unaotumiwa na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD). Taarifa ya tathmini ya Sera hizo itachangia katika kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 pamoja na Sheria yake ya mwaka 1997. Nazihimiza Wizara na Taasisi za Serikali kuongeza juhudi katika kuainisha miradi inayokidhi vigezo vya kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP ili Nchi iweze kunufaika na fursa zinazotokana na utaratibu huo.

32.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu majadiliano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuibua fursa zilizopo na kupata ufumbuzi wa changamoto za kisera, kisheria na kitaasisi zinazokwamisha biashara na uwekezaji. Kutokana na umuhimu wa majadiliano hayo, Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa “Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote wa mwaka 2013” (Global 2013 Smart Partnership Dialogue) utakaofanyika mwezi Julai 2013, Jijini Dar es Salaam. Maandalizi ya Mkutano huo yanaendelea ambapo Mkutano maalum kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa ulifanyika mjini Dodoma mwezi Novemba 2012. Katika Mkutano huo, washiriki walipata uelewa wa pamoja wa dhana ya majadiliano ya ushirikiano kwa manufaa ya wote yatakayowasaidia kusimamia majadiliano katika maeneo yao.

33.         Mheshimwa Spika, Serikali imetoa mwongozo kwa Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya kuendesha majadiliano katika maeneo yao ili matokeo ya majadiliano hayo yatumike kikamilifu wakati wa majadiliano ya Kimataifa mwezi Julai 2013. Uzoefu wa Nchi ambazo zimeandaa majadiliano kama hayo umeonesha kwamba kuna manufaa makubwa yakiwemo kubaini wagunduzi na wabunifu, kuibua fursa mpya za teknolojia na uwekezaji na pia kupata uzoefu wa Mataifa mengine katika masuala mbalimbali. Natoa wito kwa Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya kuendesha majadiliano katika maeneo yao na kujiandaa kikamilifu kushiriki katika Mkutano huo.



34.         Mheshimiwa Spika,  katika  kipindi  cha Januari 2012 hadi Desemba 2012, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kilisajili Miradi 869 yenye thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 30,866. Kati ya miradi hiyo, Miradi 469 sawa na Asilimia 54 ni miradi ya wawekezaji wa ndani, Miradi 195 sawa na Asilimia 22 ni ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na Nje na Miradi 205, sawa na Asilimia 24 ni ya wawekezaji kutoka Nje. Usajili wa miradi hiyo umeongeza ajira Nchini ambapo zaidi ya Watanzania 174,412 walipata ajira kwenye miradi hiyo. Tathmini ya thamani ya uwekezaji  kisekta  inaonesha kwamba katika mwaka 2012 miradi ya Sekta ya Kilimo inaongoza ikiwa imechangia Shilingi Bilioni 14,226 ikifuatiwa na Sekta ya Uzalishaji Viwandani  iliyochangia  Shilingi   Bilioni 4,672. Sekta hizo zinafuatiwa na Sekta ya Mawasiliano iliyochangia Shilingi Bilioni 4,663 na Sekta ya Nishati iliyochangia Shilingi Bilioni 2,110. Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa ya kufanya kazi kama Timu moja katika kuvutia wawekezaji. Ili kuweza kuvutia wawekezaji katika hali endelevu, ni muhimu sana Sera na Sheria za Uwekezaji zikatoa  Mwongozo  ambao  unatabirika  kwa  muda  mrefu.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

35.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeratibu na kufanya tathmini ya Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi, Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, SIDO, SELF, Agriculture Input Trust Fund na Presidential Trust Fund.  Mifuko mingine ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya Nje na Mfuko wa Kudhamini Taasisi za Fedha Kutoa Mikopo kwa Miradi Midogo na ya Kati. Katika  Makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali na Taasisi za Fedha zilizoteuliwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali ni kwamba Taasisi hizo zikopeshe mara tatu zaidi ya dhamana iliyotolewa na Serikali. Katika kutekeleza makubaliano hayo, hadi Desemba 2012 Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira ulitoa mikopo kwa Wajasiriamali 76,546 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 50.06. Urejeshaji  wa  mikopo hiyo  umefikia  wastani  wa  Asilimia  82. Aidha, katika kipindi hicho, Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi umetoa mikopo ya Shillingi Bilioni 8.6 kwa Mikoa 11, Wilaya 27, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOs) 49 na Wajasiriamali 8,497. Ufuatiliaji wa maendeleo ya Mifuko mbalimbali ya Uwezeshaji unaonesha kuwa Wananchi waliopata mikopo wameweza kupiga hatua za kimaendeleo kwa kuongeza tija na uzalishaji katika shughuli zao na hatimaye kuongeza kipato na kuboresha hali zao za maisha.

36.         Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa awamu ya pili ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulikamilika mwaka 2012. Tathmini ya utekelezaji imeonesha kwamba TASAF imetoa mchango mkubwa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo Vijijini iliyoibuliwa na Wananchi. Katika utekelezaji wa awamu hiyo, jumla ya Miradi 1,010 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 20 iliibuliwa na kuwezeshwa katika Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, mafunzo ya ujasiriamali yalitolewa kwa Vikundi 1,778 vyenye wanachama 22,712 katika Halmashauri 44 kwa lengo la kuviimarisha ili kuongeza ufanisi zaidi katika shughuli zao.

37.         Mheshimiwa Spika, kutokana na mafanikio hayo, tarehe 15 Agosti 2012, awamu ya tatu ya TASAF ilizinduliwa Mjini Dodoma na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awamu hiyo itakayogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 440 inatekeleza Mpango wa  Kunusuru  Kaya  Maskini  Zilizo Katika Mazingira Hatarishi. Mpango huo unalenga kuziwezesha kaya maskini kupata chakula na kujiongezea fursa za  kipato kwa kuzipatia fedha ili  kumudu mahitaji ya msingi kama vile lishe bora, huduma za afya na elimu. Mpango huo utakaotekelezwa kwa awamu katika Halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar, umeanza kwa utambuzi wa Kaya maskini katika Vijiji 20 vya Halmashauri ya Bagamoyo ambapo jumla ya Kaya 3,056 zimetambuliwa. Zoezi hilo linaendelea kwenye Halmashauri nyingine 13 na ifikapo Juni 2014, Halmashauri zote Nchini zitafikiwa.

UZALISHAJI MALI


Kilimo cha Mazao ya Chakula na Biashara

38.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza Azma ya KILIMO KWANZA, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP), Mpango wa Utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo na Dawa za Kilimo, Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme – CAADP) na kuboresha huduma za ugani na utafiti katika Sekta ya Kilimo. Hatua nyingine ni pamoja na kuvutia Wawekezaji katika Sekta ya Kilimo, kuhimiza Kilimo cha Umwagiliaji, kuongeza fursa za upatikanaji wa zana bora za kilimo hasa matrekta, kuimarisha masoko na kurahisisha upatikanaji wa mitaji kutoka Vyombo vya Fedha, hususan kupitia Dirisha la Kilimo katika Benki ya Maendeleo Tanzania.

39.         Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa jitihada za kuendeleza Kilimo zimeanza kuleta matumaini hasa katika kuongeza upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo na kuongeza tija na uzalishaji. Kwa mfano, katika mwaka  2012/2013, Tani  226,092  za  mbolea  zilifikishwa  kwa  Wakulima 3,792,000 Nchini na upatikanaji wa mbegu bora ulifikia Tani 30,443 ikilinganishwa na Tani 28,612 zilizozalishwa mwaka 2011/2012.  Kutokana na ongezeko la matumizi ya mbolea na Wakulima kuzingatia Kanuni za Kilimo Bora, tija anayopata mkulima katika zao la mahindi chotara kwa sasa ni Wastani wa Tani 3.9 kwa hekta na tija ya uzalishaji wa zao la mpunga ni Tani 3.8 kwa hekta katika maeneo ya umwagiliaji. 

40.         Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa utoaji ruzuku ya mbolea na mbegu bora kwa kutumia utaratibu wa Vocha mwaka 2008/2009. Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kutokana na utaratibu huo, hasa kuongezeka kwa upatikanaji na matumizi ya  mbolea na mbegu bora pamoja  na  tija  katika  uzalishaji  wa mazao ya kilimo, mpango  huo  umekuwa  na changamoto kadhaa. Changamoto zilizojitokeza ni pamoja na mbolea na Vocha kuchelewa kufika kwa walengwa; uteuzi wa Mawakala usiozingatia vigezo na udanganyifu uliofanywa na baadhi ya Mawakala kwa kushirikiana na Watumishi wasio waaminifu pamoja na Wajumbe wa Kamati za Pembejeo katika ngazi mbalimbali za utekelezaji. Serikali imechukua hatua kwa kufanya ukaguzi maalum kwenye maeneo yaliyokuwa na upungufu huo na waliobainika kuhusika na udanganyifu wamefikishwa kwenye Vyombo vya Sheria.

41.         Mheshimiwa Spika, mwaka jana Serikali iliahidi kufanya mapitio ya Mfumo wa utoaji wa mbolea ya ruzuku na mbegu bora kwa kutumia utaratibu wa Vocha ili kuondoa upungufu uliojitokeza. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali imeboresha mfumo huo na kuanzia mwaka 2013/2014 ruzuku ya pembejeo za kilimo itatolewa kwa Mikopo kupitia Vikundi vya Wakulima.

 

Umwagiliaji

42.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imepanua eneo la Kilimo cha Umwagiliaji Nchini. Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu katika skimu 21 za umwagiliaji zenye eneo la hekta 19,567. Kazi nyingine zinazoendelea ni kukamilisha ujenzi wa Mabwawa matano ya Umwagiliaji ya Mahiga (Kwimba); Inala (Tabora); Lwanyo (Mbarali); Mesaga (Serengeti) na Dongobesh (Mbulu). Miradi mingine iliyotekelezwa ni Skimu 34 zenye eneo la Hekta 17,824 kwa kutumia Mfuko wa Wilaya wa Kuendeleza Umwagiliaji. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaanza ujenzi wa mabwawa matatu ya Idodi (Iringa); Manyoni (Singida) na Masengwa (Shinyanga Vijijini).

Kilimo cha Matunda na Mboga

43.         Mheshimiwa Spika, Kilimo cha matunda na mboga kina mchango mkubwa katika ukuaji uchumi, fursa za ajira, lishe na kupunguza umaskini. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Mazao ya Bustani wa mwaka 2010/2011 – 2020/2021. Utekelezaji wa Mkakati huo unaolenga kukuza uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mazao ya bustani; ujenzi wa miundombinu; uhifadhi bora wa Mazao ya Bustani;  ujenzi na utafutaji wa masoko; na ukuzaji rasilimali watu umeanza kuonesha matokeo mazuri. Uzalishaji wa mazao ya bustani umeongezeka kutoka Tani milioni 4.1 mwaka 2009/2010 hadi Tani milioni 5.1 mwaka 2012/2013 na mauzo ya mazao hayo nje ya Nchi yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 159.8 mwaka 2009 hadi Bilioni 602.1 mwaka 2012. Mafanikio haya ni ya kuridhisha ingawa bado kuna fursa kubwa ya kuongeza tija na ufanisi katika sekta hii. Tayari tunao Mwongozo wa Kilimo cha Embe ambao utatuwezesha kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo. Miongozo ya Uzalishaji bora wenye tija kwa mazao mengine ya bustani itaandaliwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itatoa mafunzo ya teknolojia za uzalishaji wa miche bora ya mazao ya bustani hususan kwa vikundi vya Vijana.

Mwenendo Wa Bei Za Mazao Makuu

44.         Mheshimiwa Spika, mwenendo wa bei za mazao makuu ya biashara Nchini ambayo ni Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Korosho, Katani na Pareto umekuwa ukibadilika mara kwa mara kwa kutegemea bei za Soko la Dunia. Mabadiliko hayo yanawaathiri sana wakulima wetu pale bei zinaposhuka. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilikutana na Wadau wa mazao makuu asilia ya biashara Nchini ili kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mfuko Maalum wa kufidia bei za Mazao kwa wakulima pale zinaposhuka (Price Stabilization Fund). Lengo ni kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri ya mazao na kuwaepusha na hasara inayotokana na kushuka kwa bei hizo katika masoko ya kimataifa na pia kuwahamasisha wakulima kuendelea kulima mazao husika. Serikali kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Bodi Sita za mazao inayafanyia kazi maoni ya wadau kuhusu kuanzisha Mfuko Maalum wa Kufidia Bei za mazao.  

45.         Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba na Novemba 2012, niliongoza Mikutano mikubwa iliyolenga kuwaleta pamoja Watunga Sera, Washirika wa Maendeleo na Wawekezaji ili kujadili fursa na changamoto mbalimbali za Sekta ya Kilimo. Katika Mikutano hiyo, wadau waliandaa na kukubaliana Mpango Kazi ulioainisha majukumu yatakayotekelezwa na kila mdau ili kuongeza uwekezaji katika Ukanda wa SAGCOT. Majukumu ya  Serikali  ni  pamoja  na  upimaji  ardhi kwa ajili ya kilimo, ujenzi  wa miundombinu  ya msingi na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha uwekezaji katika Sekta ya Kilimo. Serikali imechukua hatua kwa kuainisha na kuweka mipaka ya ardhi kwa kuanzia na Wilaya za Kilombero, Ulanga na Rufiji. Zoezi hilo la kuanisha ardhi limelenga kutoa kipaumbele cha kwanza katika upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wakulima wadogo. Hadi sasa ardhi ya Vijiji 100 katika Wilaya ya Kilombero imepimwa.

46.         Mheshimiwa Spika, wawekezaji wengi wa ndani na nje ya Nchi wameonesha mwamko mkubwa wa kuwekeza katika ukanda wa SAGCOT. Msisitizo wa Serikali ni kwamba kila mwekezaji mkubwa atakayewekeza atalazimika kuwa na Mpango wa kuendeleza na kushirikiana na wakulima wadogo. Hatua hiyo itamsaidia mkulima mdogo kupata teknolojia mpya, uhakika wa pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji pamoja na soko la uhakika. Tayari utaratibu wa namna hiyo umeanza kuonesha matokeo mazuri Wilayani Kilombero.

47.         Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Washirika wa Maendeleo  ambao ni Shirika la Maendeleo la Marekani, Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Uingereza wamekubali kusaidia ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 103 kwa kiwango cha lami ambayo itaunganisha Mikumi na Ifakara katika Bonde la Kilombero. Hatua za awali za ujenzi wa barabara hiyo zimeanza. Kukamilika kwa barabara hiyo muhimu kutafungua fursa zaidi za uwekezaji na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ya wakulima. Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati Washirika wetu hao wa Maendeleo kwa kukubali kusaidia utekelezaji wa mradi huo.

Miundombinu ya Masoko ya Mazao

48.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya masoko ya mazao kama moja ya mkakati madhubuti  wa kumrahisishia mkulima kufikisha mazao  yake  sokoni  na kuongeza bei ya mazao hayo. Chini ya Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini, Serikali, imekamilisha usanifu na kutangaza  zabuni  za  ujenzi  wa  barabara  zenye  jumla ya Kilometa 210.8 katika Halmashauri za Mbulu, Njombe, Iringa Vijijini, Kahama, Lushoto, Rufiji, Songea Vijijini na Singida Vijijini. Aidha, zabuni kwa ajili ya ujenzi wa maghala mawili katika Halmashauri za Wilaya ya Iringa Vijijini na Njombe zimetangazwa na taratibu za ujenzi wa ghala katika Halmashauri ya Mbulu zinakamilishwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara na miundombinu mingine ya masoko Tanzania Bara na Zanzibar.

Maendeleo ya Sekta ya Mifugo

49.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013 Serikali imeanza kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo (2011/2012 – 2015/2016). Programu hiyo inalenga kuwa na Sekta ya Mifugo ya kisasa itakayoongeza ukuaji wa Sekta kutoka Asilimia 2.3 hadi 4.5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2016. Ili kufikia malengo hayo, Serikali pamoja na mambo mengine, imezielekeza Halmashauri zote Nchini kufanya tathmini ya uwezo wa ardhi katika maeneo yao ili kufuga kulingana na uwezo wa eneo lililopo.

50.         Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeboresha huduma za uhamilishaji  pamoja  na  kutoa Ruzuku ya Dawa  za Kuogesha Mifugo Lita 92,323 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5 ambazo zimesambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Hatua hiyo imekwenda  sambamba na kujenga Majosho Mapya 14  na kukarabati  Majosho  20 katika  Mikoa ya Arusha, Iringa, Kagera, Lindi, Mara, Mbeya, Mwanza, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Simiyu, Singida, Geita na Tanga. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo ya unenepeshaji mifugo kwa Wafugaji wanaozunguka Ranchi za Taifa. Pia, Miradi 13 ya unenepeshaji mifugo imeibuliwa kupitia Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya katika Mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Mwanza, Shinyanga na Singida. Hatua hiyo imeongeza idadi ya Ng’ombe walionenepeshwa kutoka 132,246 mwaka 2011 hadi Ng’ombe 150,000 mwaka 2012.  Aidha, Vijiji 781 vya Halmashauri za Wilaya 80 katika Mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Pwani, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Singida vimepimwa ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

51.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo ili itoe mchango mkubwa zaidi katika uchumi. Aidha, itakamilisha ujenzi wa Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo ambao unatarajiwa kuanza kazi mwezi Agosti 2013. Vilevile, itaimarisha uhamilishaji Nchini kwa kuzalisha Dozi za mbegu bora za uhamilishaji.

Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi

52.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeanza kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na kuandaa Mkakati wa utekelezaji. Lengo ni kuihuisha Sera hiyo ili iendane na mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii yaliyojitokeza pamoja na kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia katika Sekta ya Uvuvi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itakamilisha kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na kuendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi. Aidha, Vikundi vya Ulinzi Shirikishi vya Kudhibiti Uvuvi Haramu na Vituo vya Doria vitaimarishwa. Serikali pia itaendelea kusimamia shughuli za ukuzaji wa viumbe kwenye maji ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kuzalisha vifaranga vya samaki.

Ufugaji Nyuki

53.         Mheshimiwa Spika, Uzalishaji wa Asali na Nta kwa miaka ya hivi karibuni unatupa moyo kwamba, Ufugaji wa Nyuki unaweza kuwa ni shughuli ya kiuchumi inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea umaskini. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita  2009 - 2012, uzalishaji wa Asali ulifikia Wastani wa Tani 8,747 na Nta Tani 583. Katika juhudi za kuongeza uzalishaji, Serikali imetoa elimu ya ufugaji nyuki katika Wilaya za Kahama (Vijiji 7), Chunya (Vijiji 4), Same (Vijiji 2), Manyoni (Vijiji 3), Singida (Vijiji 2) na Kibondo (Vijiji 13). Aidha, Mizinga 500 imesambazwa katika Wilaya za Ruangwa, Mtwara, Newala, Tunduru na Namtumbo ambapo kila Wilaya ilipata Mizinga 100. Pamoja na juhudi hizo, Hekta 56,290 zimepimwa kwa ajili ya kutenga hifadhi za nyuki katika Vijiji mbalimbali Nchini.

54.         Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ndogo ya Ufugaji Nyuki kwa maendeleo ya Wananchi, niliahidi kwamba yatafanyika Maonesho Maalum ya Ufugaji Nyuki. Maonesho hayo yamefanyika Kitaifa  Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 - 7 Oktoba 2012 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo yalitanguliwa na Kongamano lililofanyika tarehe 3 Oktoba 2012.  Kauli Mbiu ya Maonesho ilikuwa ni “ASALI KWA AFYA NA USTAWI”. Maonesho hayo yameleta chachu na matumaini makubwa ya kukua kwa biashara ya mazao ya Nyuki kwani tangu kumalizika, Wafugaji Nyuki wa Tanzania wamepata soko la kuuza zaidi ya Tani 100 za Asali Nchini Ujerumani. Aidha, Wajasiriamali wengi wamepata Alama ya Utambulisho wa Biashara (Barcode) kwa ajili ya kutambulisha Asali yao. Vilevile, kutokana na wananchi kuhamasika kufuga nyuki, Serikali imeanza kutengeneza mizinga bora ipatayo 70,000, kuiwekea chambo na kuisambaza kwa wananchi kwa gharama nafuu.

55.         Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Sekta ya Nyuki, kwa mara ya kwanza Tanzania iliadhimisha siku ya Kitaifa ya Kutundika Mizinga, tarehe 4 Machi 2013 katika Hifadhi ya Aghondi iliyopo Wilayani Manyoni Mkoa wa Singida. Katika uzinduzi huo, Wadau walipata nafasi ya kutambua fursa kubwa zilizopo katika Sekta hiyo na kujenga mahusiano ya karibu ya kibiashara. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itafanya mapitio ya Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 ili iendane na mabadiliko yanayotokea. Aidha, mafunzo na vifaa kwa ajili ya ufugaji nyuki yatatolewa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa Asali na Nta.

Maendeleo ya Viwanda

56.           Mheshimiwa Spika, mchango wa Sekta ya Viwanda kwenye Pato la Taifa uliongezeka na kufikia Asilimia 9.7 mwaka 2012 ikilinganishwa na Asilimia 9.0 mwaka 2011. Viwanda vinavyoendelea vizuri katika uzalishaji na kutoa mchango  mkubwa  ni  pamoja na viwanda vya saruji, bia, unga wa ngano,  vinywaji baridi, sukari, rangi, nyaya za umeme na usindikaji  wa  ngozi.  Kwa  upande  wa SIDO, jumla ya Wajasiriamali 4,766 wamepatiwa mafunzo mbalimbali ya  kukuza  ujuzi  wao  hususan  katika  usindikaji wa mafuta ya  kupikia,  ngozi,  ubanguaji  wa korosho pamoja na kuhifadhi  na  kusindika  vyakula  vya  aina  mbalimbali. Aidha,
SIDO ilitoa huduma za ugani kwa Wajasiriamali 6,779 ili kuboresha shughuli za uzalishaji. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kubuni mikakati mipya yenye lengo la kuendeleza na kuviwezesha viwanda vidogo na vya kati vya wajasiriamali wa ndani pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa viwanda Nchini.

57.           Mheshimiwa Spika, ili kuhamasisha Usindikaji wa Ngozi hapa Nchini na kuongeza thamani ya zao la ngozi, mwezi Julai 2012, Serikali iliongeza Ushuru wa Ngozi Ghafi zinazouzwa nje ya Nchi kutoka Asilimia 40 hadi 90 kwa kilo. Kutokana na hatua hiyo, ngozi zinazosindikwa Nchini zimeongezeka kutoka vipande vya ngozi za Ng’ombe 166,773 na vipande vya ngozi za Mbuzi na Kondoo 778,023 kipindi cha Januari - Juni, 2012 hadi vipande vya ngozi za Ng’ombe 343,860 na vipande vya ngozi za Mbuzi na Kondoo 1,173,875 kipindi cha Julai - Desemba, 2012. Ongezeko hilo linathibitisha kwamba hatua zilizochukuliwa na Serikali zimeongeza usindikaji wa ngozi na kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ya ngozi Nchini. Serikali itaendelea kusimamia mafanikio hayo na kuchukua hatua zaidi zitakazoongeza usindikaji wa ngozi hapa Nchini.

 

Sekta ya Utalii

58.           Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa kuifanya Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Tanga kuwa vituo vya utalii wa fukwe. Mikoa hiyo ina fukwe za kipekee zinazovutia watalii na pia zinafaa kwa uwekezaji wa kitalii. Vilevile, Serikali imevitangaza vivutio vya utalii katika soko la ndani na nje ya nchi kupitia Vyombo vya Habari na  maonesho ya ndani na Kimataifa. Kutokana na hatua hiyo, idadi ya Watalii walioingia nchini mwaka 2012 imeongezeka na kufikia watalii 930,753 ikilinganishwa na watalii 867,994 mwaka 2011. Aidha, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 2,119 mwaka 2011 hadi Shilingi Bilioni 2,183 mwaka 2012.

59.         Mheshimiwa Spika, matunda ya juhudi za kutangaza vivutio vya utalii na pia kuhamasisha utalii wa ndani yamedhihirika baada ya Taasisi ya The Seven Natural Wonders yenye Makao yake Nchini Marekani kuijumuisha Tanzania katika zoezi la kutafuta Maajabu Saba ya Asili katika Bara la Afrika. Zoezi hilo lilishirikisha wataalam wengi Duniani na kupigiwa kura na watu kutoka sehemu mbalimbali, wakiwemo Watanzania  kwa  kutumia  Tovuti. Matokeo ya zoezi  hilo  yalitangazwa tarehe 11 Februari 2013, Jijini Arusha, ambapo Tanzania  iliibuka  mshindi  kwa  vivutio  vitatu  vya  Maajabu Saba ya Asili ya Afrika yakijumuisha Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro Crater  na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Watanzania  wote  wa  ndani  na nje ya Nchi walioshiriki kupiga kura na hatimaye kutuwezesha kupata ushindi huo. Aidha,  namshukuru Dkt. Philip Imler ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi  ya  The Seven Natural Wonders aliyesimamia zoezi hilo. Pia, nayashukuru Makampuni yote yaliyofadhili mashindano hayo na kutangaza vivutio vya Tanzania Barani Afrika na Duniani kote. Natoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha kwamba tunavilinda, tunavitunza na kuviendeleza vivutio hivyo kwa manufaa ya Taifa letu. Tutumie pia ushindi huo kutangaza zaidi utalii wetu ili rasilimali hizi nzuri tulizo nazo ziendelee kuvutia watalii wengi na kuongeza mapato yetu.

 



Sekta ya Madini


60.         Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wa madini wana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi yetu. Ili kuwaendeleza wachimbaji hao, Serikali imekamilisha Mkakati, Mpango Kazi na Programu ya Mafunzo pamoja na kuwatengea maeneo  wachimbaji  wadogo  kwa  mujibu  wa Sheria. Maeneo hayo ni Mpambaa (Singida), Kilindi (Tanga), Dete na Melela (Morogoro), Winza (Dodoma), Songwe (Mbeya), Nyakunguru (Mara), Nyamilonge na Ilagala (Kigoma), Mihama (Katavi), Mwajanga (Manyara), Makanya (Kilimanjaro) na Mbesa (Ruvuma). Aidha, Serikali imekusanya takwimu na taarifa muhimu za wachimbaji wadogo kote Nchini kwa lengo la kuwatambua, kufahamu changamoto walizonazo na kujenga kanzidata (database). 

61.         Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa Mwanachama kamili wa Mpango wa Kimataifa Unaohimiza Uwazi katika Sekta ya Madini (Extractive Industries Transparency Initiatives- EITI) baada ya kutimiza vigezo vilivyowekwa kimataifa katika Sekta ya Madini. Hatua hiyo imeiwezesha Tanzania kuwa na mfumo thabiti wa utoaji taarifa za malipo na mapato kutoka katika kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji wa Madini, Gesi Asilia na Mafuta ambao unamwezesha mwananchi kufahamu na kujadili mchango wa Kampuni hizo katika Pato la Taifa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaimarisha ukaguzi kwenye uzalishaji na biashara ya madini pamoja na kuimarisha STAMICO ili itekeleze majukumu yake kikamilifu.

 

HALI YA AJIRA NCHINI

62.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza fursa za ajira kwa vijana wengi wanaoingia kwenye soko la ajira  kila  mwaka. Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti wa Ajira na Kipato Nchini wa mwaka 2010/2011, Ajira ziliongezeka kutoka 1,276,982 mwaka 2010 hadi Ajira 1,362,559  mwaka  2011, sawa na  ongezeko  la Asilimia 6.7. Ili kuongeza kasi ya ukuaji wa ajira, Serikali inakamilisha Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ajira kwa Vijana.  Programu hiyo ya miaka mitatu itaongeza fursa za Vijana 301,100 kuweza kujiajiri au kuajiriwa. Msukumo zaidi utawekwa katika Miradi ya Kilimo, Viwanda Vidogo, Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZ na SEZ), Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Sambamba na hatua hiyo, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi na vya Elimu ya Juu ili kuwawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.

 

HUDUMA ZA KIUCHUMI


Ardhi

63.         Mheshimiwa Spika, pamoja na Nchi yetu kuwa na ardhi ya kutosha na inayofaa kwa Kilimo na uwekezaji mwingine, bado hatujakamilisha zoezi la uwekaji mipaka, kupima na kutoa Hati kwa matumizi mbalimbali. Hali hiyo inachangia migogoro ya ardhi na kukwamisha uwekezaji kwa kiasi kikubwa. Serikali imechukua hatua muhimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa itakayoharakisha zoezi la upimaji ardhi. Katika kutekeleza kazi hiyo, Awamu ya Kwanza ya usimikaji wa Mtandao wa Alama za Msingi za Upimaji Ardhi Nchini (Geodetic Control Network) imekamilika. Mikoa iliyohusika ni Pwani, Morogoro, Mara, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Lindi, Tabora na Dodoma. Tayari majaribio ya matumizi ya Alama hizo yamefanyika katika Wilaya za Ngorongoro na Kilombero na kudhihirisha kuwa gharama na muda wa kupima ardhi zimepungua. Awamu ya Pili ya usimikaji wa Alama hizo utaendelea katika Mikoa iliyobaki na kuanza upimaji wa viwanja na mashamba kwa kutumia utaratibu mpya wa upimaji wa ardhi.

64.         Mheshimiwa Spika, ili kuwa na mfumo endelevu wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi. Mfumo huo utakaounganisha Ofisi za Ardhi Nchini unategemewa kukamilika mwaka 2014 na utaiwezesha Tanzania kuwa na kumbukumbu sahihi za ardhi. Vilevile, utaharakisha na kurahisisha utoaji wa maamuzi, upimaji na utoaji wa Hati Miliki na hivyo kupunguza migogoro ya ardhi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za ardhi na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Nishati

65.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusogeza huduma ya nishati ya umeme karibu na Wananchi ili kuharakisha   maendeleo yao.  Katika  kutekeleza  azma  hiyo, gharama  za  kuunganisha  umeme  wa  njia  moja  kwa  wateja  wadogo Vijijini na  Mijini  zimepunguzwa kwa wastani wa kati ya  Shilingi Milioni 1,311,000 na Shilingi 114,000. Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi kumudu gharama ya kuunganisha umeme na kuongeza kasi ya usambazaji umeme Nchini. Serikali pia, imefikisha umeme katika Makao Makuu ya Wilaya za Nkasi na Namtumbo, hivyo kufanya idadi ya Makao Makuu ya Wilaya zenye umeme kuwa 117, sawa na Asilimia 88 ya Wilaya zote Nchini. Vilevile, Serikali inatekeleza Programu Kabambe ya Kusambaza Umeme Vijijini ambapo wateja 8,046 wamelipiwa gharama za kuunganishiwa umeme kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini. Aidha, kazi ya kusambaza na kuboresha miundombinu ya umeme katika Mikoa ya Mtwara na Lindi inaendelea kufanyika.

66.         Mheshimiwa Spika, Sekta ndogo ya Gesi Asilia inakua kwa kasi ambapo hadi kufikia Januari 2013, kiasi cha futi za ujazo Trilioni 35 zimegundulika Nchini. Ili kusimamia rasilimali hiyo muhimu, Serikali imeandaa rasimu ya Sera ya Gesi Asilia na kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali. Aidha, tarehe 8 Novemba 2012, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme na kupunguza gharama za umeme Nchini.

67.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mradi wa bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ujenzi wa Mitambo ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi (MW 200). Vilevile, itaanza kutekeleza Awamu ya Pili ya Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini na kufikisha umeme wa gridi kwenye Makao Makuu ya Wilaya zisizokuwa na umeme.

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano

68.         Mheshimiwa Spika, Serikali  inatekeleza  Mradi  wa ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wenye Awamu Tano. Awamu  ya  Kwanza  na ya Pili ya Ujenzi wa Mkongo huo wenye urefu wa Kilomita 7,560 imekamilika na kuunganisha Makao  Makuu  ya  Mikoa  24  ya  Tanzania  Bara.  Kazi  ya   kuunganisha  Kisiwa  cha  Unguja  na  Mkongo huo kupitia Dar es Salaam itakamilika mwaka 2013. Tayari Makampuni ya Simu na Mawasiliano ya hapa Nchini yameunganishwa kwenye Mkongo hatua ambayo imewezesha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano katika eneo kubwa zaidi na kwa gharama nafuu. Sambamba na hatua hiyo, Serikali imeanza ujenzi wa Mfumo wa Kuratibu Huduma za Mawasiliano Nchini (Traffic Monitoring System). Mfumo huo utasaidia kuhakikisha mapato yanayotokana na huduma katika Sekta ya Mawasiliano yanajulikana ili Makampuni ya Mawasiliano Nchini yalipe kodi stahiki kwa Serikali.

69.         Mheshimiwa Spika, Tanzania pamoja na Nchi zote Duniani kupitia Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) zimekubaliana kusitisha matumizi ya teknolojia ya utangazaji kutoka Mfumo wa Analojia na kuanza Matumizi ya Teknolojia ya Dijitali ifikapo Juni 2015. Hapa  Nchini, usitishaji wa matumizi ya mfumo wa mitambo ya analojia umeanza kutekelezwa tarehe 31 Desemba 2012 kwa awamu kwa kuanzia  na  Jiji  la  Dar es Salaam  na  kufuatiwa  na  Mikoa ya Dodoma, Tanga na Mwanza. Matangazo ya analojia yataendelea  kusitishwa  katika Mikoa mingine Nchini kulingana na ratiba iliyowekwa. Natambua kwamba kuna changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa zoezi hilo la mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha mawasiliano na kuiwezesha Nchi  yetu  kuendana  na hali halisi ya mabadiliko ya  teknolojia  Duniani. Katika mazingira ya sasa, sisi kama Taifa siyo  vyema kubaki kama kisiwa wakati  tumeunganishwa  na  mifumo  ya  teknolojia ya kidunia.

Hivyo, ni busara tuendelee na mabadiliko hayo sasa kuliko kusubiri na hatimaye tukajikuta tuko nyuma na nje ya mstari. Natoa wito kwa Watanzania wote kuyaona mabadiliko hayo kwa mtazamo chanya na kuyakubali kama hatua kubwa sana ya maendeleo ya teknolojia Nchini.

Sayansi na Teknolojia

70.         Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya jitihada kubwa za kuendeleza Sayansi na Teknolojia kama njia ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Jitihada hizo ni pamoja na kutenga fedha za kutosha kila mwaka kwa ajili ya utafiti na maendeleo ya kisayansi. Serikali pia, imekamilisha ujenzi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela iliyopo Mkoani Arusha ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 2 Novemba 2012.  Kukamilika kwa ujenzi wa Taasisi hiyo kumeongeza udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu kutoka wanafunzi 83 mwaka 2011/2012 hadi wanafunzi 135 mwaka 2012/2013. 

71.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake katika maeneo mbalimbali Nchini na Nchi jirani. Vilevile, Serikali itaendelea na zoezi la kuhama kutoka katika mfumo wa analojia kwenda dijitali na kupanua na kuboresha Mtandao wa Huduma za Mawasiliano ya simu na intaneti Nchini.

Barabara na Madaraja

72.         Mheshimiwa Spika, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa  katika  kujenga, kukarabati na kuboresha mtandao wa Barabara Kuu, za Mikoa, Wilaya pamoja na za Vijijini ili zipitike wakati wote wa mwaka. Lengo ni kuwa na mtandao bora wa barabara utakaowezesha Wananchi, hasa Wakulima kusafirisha  mazao  yao  hadi  kwenye  Masoko ya ndani na nje ya Nchi. Katika mwaka 2012/2013, Serikali  imejenga  jumla ya Kilometa 294.4  za  kiwango  cha  lami  katika Barabara  Kuu  na za Mikoa  na  kukarabati   kwa  kiwango  cha lami jumla  ya Kilometa 111.8 katika barabara  hizo. Aidha, kazi za ujenzi na ukarabati wa Barabara Kuu na za Mikoa zenye urefu wa Kilometa 179 kwa kiwango cha lami unaendelea katika maeneo mbalimbali Nchini.

73.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imedhamiria kujenga na kukamilisha ujenzi wa Madaraja makubwa na ya kisasa mawili ambayo ni Daraja la Mto Malagarasi  na  Daraja  la  Kigamboni.  Ujenzi wa Daraja la Mto Malagarasi unaojumuisha ujenzi wa Daraja kubwa lenye urefu wa Meta 200 na Madaraja mengine madogo katika Bonde la Mto Malagarasi  unaendelea vizuri. Hadi mwezi Machi 2013, Mkandarasi amekamilisha ujenzi kwa  Asilimia 85. Sambamba na hatua hiyo, taratibu zimekamilika za kupata mkopo wa nyongeza kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Korea kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiungo za Daraja hilo zenye urefu wa Kilometa 37 kwa kiwango cha lami.

74.         Mheshimiwa Spika, kwa upande  wa Daraja la Kigamboni lenye urefu wa Meta  680 linalojengwa kuunganisha eneo la Kurasini na Kigamboni katika Bahari ya Hindi, tayari Mkandarasi  amekamilisha  kazi za maandalizi kwa Asilimia 90. Kazi ya ujenzi wa Daraja la Kudumu na Barabara zake inatarajiwa kuanza wakati  wowote  kuanzia  sasa.  Daraja  hili linajengwa  kwa  Ubia kati ya Serikali na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Lengo ni kukamilisha ujenzi wa Daraja hilo mwanzoni mwa mwaka 2015.

75.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Serikali itajenga Barabara Kuu kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Kilometa 495 na kukarabati Barabara zenye urefu wa Kilometa 190 na Madaraja 11. Serikali pia, itajenga barabara za Mikoa za lami zenye urefu wa Kilometa 54.3 na kukarabati Kilometa 855 kwa kiwango cha changarawe na Madaraja 36. Aidha, matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum ya Barabara Kuu na za Mikoa yataendelea kufanyika katika kipindi kijacho.

Usafiri wa Barabara katika Jiji la Dar es Salaam

76.         Mheshimiwa Spika, msongamano wa magari katika barabara za Jiji la Dar es Salaam ni moja ya changamoto ambayo Serikali inaendelea kuifanyia kazi. Jitihada zinazofanyika kupunguza msongamano wa magari barabarani ni pamoja na kujenga miundombinu zaidi ya barabara mpya za kuingia na kutoka katikati ya Jiji; kuanzisha usafiri wa Treni ya Abiria; kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART); na kuimarisha usimamizi wa Sheria za Usalama Barabarani.

77.         Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa barabara mpya za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam, hadi Machi, 2013 ujenzi wa Barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa 6.4 kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo - Kigogo hadi mzunguko wa barabara ya Kawawa imekamilika na barabara yenye urefu wa Kilometa 2.7 kutoka barabara ya Kawawa – Bonde la Msimbazi hadi Makutano ya Jangwani na Twiga imekamilika kwa Asilimia 70. Aidha, ujenzi wa Barabara yenye urefu wa Kilometa 10.3 kutoka Jet Corner - Vituka hadi Davis Corner imekamilika kwa Asilimia 90. Vilevile, utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka unaendelea ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa barabara za DART na za magari mchanganyiko na baiskeli katika Barabara ya Morogoro, na  ujenzi wa Miundombinu ya Mifumo ya Maji, Vituo vya Mabasi na Madaraja. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara nyingine za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam pamoja na ujenzi wa miundombinu ya DART.

 

HALI YA UCHUKUZI


Huduma za Usafiri wa Reli Jijini Dar es Salaam

78.         Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba 2012, Serikali ilianzisha huduma ya usafiri wa treni ya abiria Jijini Dar es Salaam kupitia Kampuni ya Reli (TRL) na TAZARA kwa lengo la kukabiliana na tatizo la msongamano wa magari na abiria. Wastani wa idadi ya Abiria wanaosafiri kwa Treni ya TAZARA ni 4,500 kwa siku na TRL ni Abiria 5,000. Takwimu zinaonesha kuwa, Abiria 9,500 wanaosafiri kila siku kwa njia ya treni wangehitaji kutumia mabasi zaidi ya 380 yenye uwezo wa kubeba Abiria 25 kila moja. Kwa ujumla mwitikio wa wananchi wa kutumia  huduma ya treni ya abiria ni mkubwa ikilinganishwa na uwezo wa kutoa huduma hiyo. Kwa kuzingatia mahitaji hayo makubwa, Serikali imeunda Kamati maalum ya wadau wa usafiri Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuchambua, kuanisha na kushauri mipango na mikakati ya baadaye ya kuboresha huduma hiyo ili iwe endelevu na salama. Ni mategemeo yangu kwamba Kamati hiyo itaandaa Mpango mzuri zaidi wa kupanua huduma hiyo muhimu kwa Jiji la Dar es Salaam ambalo kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 lina idadi ya watu Milioni 4.36, sawa na Asilimia 10 ya Wakazi wote wa Tanzania Bara. Ongezeko hilo ni kubwa na hivyo linahitaji Mpango Kabambe wa usafiri na usafirishaji.

Usafiri  wa Reli ya Kati na TAZARA

79.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya reli ya kati kwa kujenga na kukarabati maeneo mbalimbali ili kuiwezesha kupitika wakati wote. Pamoja na ukarabati huo, usanifu wa kina wa Mradi wa Uendelezaji na Ujenzi wa Reli kutoka Dar es Salaam - Isaka - Keza - Kigali na Keza - Musongati kwa kiwango  cha   Kimataifa   umekamilika  mwezi  Februari  2013. Serikali pia, imekamilisha mchakato wa kumpata Mshauri mwelekezi atakayefanya upembuzi yakinifu wa kuinua kiwango cha reli kuwa katika kiwango cha kimataifa kutoka Tabora hadi Kigoma, Kaliua hadi Mpanda na Isaka hadi Mwanza. Lengo ni kuwezesha reli hiyo ifanane na inayotarajiwa kujengwa kutoka Dar es Salaam-Isaka-Kigali/Musongati. Upembuzi Yakinifu wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi na kutoka Arusha hadi Musoma unatarajiwa kuanza mwaka 2013/2014.

80.         Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mwezi Machi 2012, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  zilitia  saini  Itifaki ya 15 ya kuboresha Reli ya TAZARA.
Tayari Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 38.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyo chini ya Itifaki hiyo ambayo inajumuisha kufanya upembuzi yakinifu wa kuboresha reli hiyo,  kukarabati njia ya reli, kununua vichwa vipya vya treni na kukarabati mabehewa ya abiria. Hatua hizi zikikamilika zitaboresha kwa kiwango kikubwa usafiri wa Reli ya TAZARA.

Bandari

81.         Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuongeza uwezo na ufanisi wa bandari zake kwa kutekeleza Mpango Kabambe wa Mamlaka ya Bandari. Baadhi ya Miradi inayotekelezwa chini ya Mpango huo ni Upembuzi Yakinifu kwa ajili ya kuimarisha na kuongeza kina cha maji katika Gati Namba 1 hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam na  kuanza  awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa matanki ya kuhifadhia mafuta. Mradi mwingine ni kufanya Upembuzi Yakinifu wa ujenzi wa kituo kikubwa cha kuhifadhia mizigo ya kwenda Nchi jirani katika eneo la Kisarawe.

82.         Mheshimiwa Spika, kutokana na nafasi ya Nchi yetu kijiografia na ongezeko kubwa la biashara na uingizaji wa mizigo ya hapa Nchini na Nchi jirani ambazo hazina bandari, uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhimili ongezeko hilo unapungua. Pamoja na jitihada zinazoendelea za kupanua miundombinu ya bandari hiyo, Serikali imeona umuhimu wa kuwa na Bandari mpya ya Bagamoyo ili isaidiane na Bandari zilizopo kukabiliana na ongezeko hilo. Tarehe 24 Machi 2013, Serikali ya Tanzania na China zimetia saini makubaliano ya kujenga Bandari mpya ya Bagamoyo ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati. Makubaliano hayo yanajumuisha pia ujenzi wa eneo huru la biashara na miundombinu mingine muhimu ikiwemo reli itakayounganisha Bandari ya Bagamoyo na Reli ya Kati na ya TAZARA pamoja na barabara ya lami kutoka Bagamoyo hadi Mlandizi. Huu ni mradi mkubwa na wa kimkakati ambao utabadili kabisa mfumo wa uendeshaji wa Bandari na usafirishaji Nchini.



Usafiri wa Anga

83.         Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza kwa mafanikio Awamu ya Kwanza ya Uboreshaji na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Tabora, Kigoma na Bukoba. Ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami katika kiwanja cha Ndege cha Tabora umekamilika na kazi za ujenzi zinazoendelea katika kiwanja cha Kigoma zinatarajiwa kumalizika mwezi Juni 2013. Kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Bukoba, ukarabati wa njia ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami unaendelea. Aidha, Kiwanja kipya cha Kimataifa cha Songwe, Mbeya kilianza kutoa huduma tarehe 13 Desemba, 2012. Kiwanja hicho ambacho kijiografia kipo karibu na Nchi za Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Nchi nyingine za Kusini mwa Afrika ni kichocheo muhimu cha shughuli za uchumi na kijamii zikiwemo utalii na kilimo hasa cha matunda, mbogamboga na maua kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Ni muhimu sana wananchi wa maeneo hayo na mengine wahamasishwe na kujipanga kutumia fursa za kiuchumi zitakazoambatana na kukamilika kwa kiwanja hicho.

84.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Upanuzi na Uboreshaji wa Viwanja vya Ndege. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na Upembuzi Yakinifu na usanifu wa kina wa ukarabati kwa kiwango cha lami wa njia za kuruka na kutua ndege kwa viwanja vya Iringa, Kilwa Masoko, Ziwa Manyara, Musoma, Mtwara, Njombe, Songea, Singida na Tanga.

 

MAENDELEO YA SEKTA YA ELIMU


Elimu ya Msingi

85.         Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kutekeleza Programu kubwa za kuendeleza elimu Nchini mwaka 2001 kwa lengo la kuongeza idadi ya Wanafunzi wa rika lengwa wanaojiunga na shule na kuboresha elimu. Utekelezaji wa Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM I & II) umeleta mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, kuandikisha Wanafunzi wa rika lengwa na kupunguza pengo la uandikishaji kati ya Wanafunzi wa Kike na wa Kiume. Mafanikio hayo yaliambatana na  changamoto za upungufu wa Walimu, Vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja  na  madawati.  Kwa  kutambua  changamoto hizo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 inaelekeza Serikali kulinda mafanikio yaliyopatikana pamoja na kuweka msisitizo mkubwa katika ubora wa elimu. 

86.         Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza kasi tuliyoanza nayo, Serikali inatekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM III) unaolenga kuboresha elimu kwa kuongeza idadi ya Walimu, vitabu vya ziada na kiada na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.  Jitihada za Serikali za kuajiri walimu zinaendelea ambapo Walimu wapya 13,568 wameajiriwa katika Shule za Msingi mwaka 2012/2013. Serikali itaendelea kuweka msisitizo katika kuboresha Elimu ya Msingi Nchini kwa kuzingatia manufaa makubwa yanayopatikana katika ngazi hiyo muhimu ya elimu.

 

Elimu ya Sekondari

87.         Mheshimiwa Spika, mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi Nchini ambayo ni pamoja na kuongezeka  kwa  idadi  ya wahitimu wanaofaulu ngazi hiyo, yameongeza mahitaji ya nafasi zaidi katika Shule za Sekondari.  Kutokana na hali hiyo, Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) mwaka 2006. Mpango huo umesaidia sana kukabiliana na changamoto ya nafasi  zaidi katika Shule za Sekondari kwa kujenga Shule nyingi za Sekondari na hivyo kuwa na wanafunzi wengi zaidi. Ni dhahiri kuwa ongezeko hilo   la  Wanafunzi   lilihitaji  Walimu  wengi  zaidi,  Maabara, Vitabu na Vifaa vingine muhimu. Aidha, Serikali iligatua usimamizi wa Shule za Sekondari kutoka Serikali Kuu kwenda katika Mamlaka za  Serikali za Mitaa ili kuboresha usimamizi wa shule hizo pamoja na kuanzisha programu kabambe ya kufundisha walimu zaidi ili wafundishe katika shule zinazoongezeka. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imeajiri jumla ya Walimu 12,969 ambao watafundisha katika Shule mbalimbali za Sekondari Nchini. Hatua hizo zote ni uwekezaji mkubwa ambao matokeo yake yatawezesha kuboresha elimu Nchini hatua kwa hatua.

88.         Mheshimiwa Spika, sote tumehuzunishwa sana na matokeo yasiyoridhisha ya mtihani wa Kidato cha Nne kwa mwaka 2012.  Matokeo hayo siyo tu kwamba yamewahuzunisha wazazi ambao wamewekeza rasilimali kwa Watoto wao bali pia Serikali ambayo imetumia rasilimali nyingi kwenye Sekta ya Elimu.  Huu siyo wakati wa kulaumiana ama kutafuta mchawi wa matokeo hayo yasiyoridhisha. Ni lazima tutafute  suluhisho, kusonga mbele na kubuni mikakati na hatua za haraka za kusaidia Watoto hao ambao wamepata matokeo mabaya. Tumeanza kwa kuunda Tume yenye Watu makini ambayo itachunguza chanzo cha matokeo hayo mabaya na kutoa mapendekezo ya namna ya kutatua tatizo hilo katika muda mfupi,  kati na mrefu na pia kupendekeza suluhisho la haraka kwa wale waliopata daraja la IV na sifuri. Napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba, matokeo ya Tume hiyo yatawekwa bayana na hatua zitakazopendekezwa zenye lengo la kuimarisha elimu Nchini zitachukuliwa.  Hata hivyo, ni vyema tukumbuke kwamba, sote tuna wajibu wa kutoa mwongozo na mapendekezo yatakayosaidia kutoka hapa tulipo. Wazazi, Wanafunzi na Jamii nzima wana nafasi yao pia katika kuboresha elimu ya Nchi hii. Hili siyo suala la Serikali pekee.

Elimu Maalum

89.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuweka msukumo  wa  kipekee katika  kutoa  Elimu Maalum  kwa watu wenye  Ulemavu  wakiwemo  wenye  Ulemavu  wa  Ngozi, Uoni Hafifu na Usikivu. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imeandaa Mwongozo wa kufundishia Wanafunzi wenye Ulemavu wa Ngozi na Uoni Hafifu. Aidha, Serikali imenunua na kusambaza vifaa maalum na visaidizi vya kufundishia na kujifunzia kuanzia ngazi ya Elimu ya Awali hadi Chuo Kikuu. Kazi nyingine zilizofanyika ni kukarabati na kujenga majengo rafiki kwa walemavu katika Chuo cha Ualimu Patandi. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa Elimu Maalum hususan baada ya kupata takwimu sahihi za walemavu kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

 

Elimu ya Juu

90.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Juu kwa kupanua na kuongeza Taasisi za Elimu ya Juu za Serikali na Binafsi. Katika kipindi takribani cha miaka 8 idadi ya wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Elimu ya Juu Nchini imeongezeka kutoka 40,993 mwaka 2005/2006 hadi 166,484 mwaka 2012/2013, sawa na ongezeko la Asilimia 306.  Serikali pia, inatoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu vya Umma na vile vya Mashirika ya Dini na vya Sekta Binafsi. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imetoa mikopo ya Shilingi Bilioni 345 kwa wanafunzi 98,772 ikilinganishwa na mikopo ya Shilingi Bilioni 291 kwa wanafunzi 93,784 mwaka 2011/2012.

91.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya Mikopo ya Elimu ya Juu na kuimarisha usimamizi wa  urejeshaji wa mikopo ili wanafunzi wengi zaidi waweze kunufaika. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wale wote walionufaika na mikopo ya elimu ya juu kulipa mikopo hiyo yenye masharti nafuu sana ili wanafunzi zaidi waweze kunufaika nayo.  Aidha, waajiri watimize wajibu wao kwa kuwataka waajiriwa walionufaika kulipa mikopo hiyo. Vilevile, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iongeze kasi ya kukusanya madeni na kuchukua hatua stahiki kwa wale wasiolipa kwa mujibu wa Sheria.

 

MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA


Vituo vya Utoaji wa Huduma za Afya Nchini

92.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba Vituo vya Utoaji wa Huduma za Afya katika ngazi zote Nchini vinapatiwa dawa muhimu na vifaa vya Teknolojia ya kisasa vya kuchunguza na kutibu magonjwa. Katika mwaka 2012/2013, Serikali imenunua Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na vitendanishi na kuvisambaza kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zote za Serikali Nchini. Serikali pia, imeongeza uwezo wa ndani wa kutibu maradhi mbalimbali. Mathalan, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imewezeshwa kutoa huduma za Afya za ubingwa wa juu ikiwa ni pamoja na upasuaji wa moyo ambapo hadi sasa zaidi ya Wagonjwa 450 wamepatiwa huduma hiyo. Vilevile, huduma ya usafishaji damu kwa Wagonjwa wa figo na Upasuaji kupitia tundu dogo pamoja na uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia mashine za kisasa unafanyika hapa Nchini. Hatua hiyo imewezesha Serikali na Wananchi kuokoa fedha nyingi zinazotumika kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya Nchi. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Madaktari, Wauguzi na Wataalam wengine wa Afya kwa kuliwezesha Taifa letu kupiga hatua kubwa katika kutibu magonjwa hayo na mengine yanayohitaji utaalam na ubingwa wa hali ya juu.

93.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma ya tiba ya saratani Nchini kwa kukamilisha ujenzi wa Jengo la kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na hivyo kuongeza uwezo wake kutoka vitanda 120 hadi 270. Aidha, Serikali imesogeza huduma ya tiba ya saratani karibu na Wananchi kwa kukamilisha ujenzi wa Jengo Maalum la kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Bugando. Hatua hiyo itapanua wigo wa kutoa huduma ya tiba ya saratani na kupunguza msongamano wa Wagonjwa wa saratani kutoka Mikoa mbalimbali waliokuwa wanalazimika kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road Jijini Dar es Salaam. 

Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria na UKIMWI

94.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012, Serikali ilifanya Utafiti kuhusu Viashiria vya UKIMWI na Malaria. Taarifa ya matokeo ya utafiti huo inaonesha kuwa kiwango cha Malaria Nchini kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kimepungua kutoka Asilimia 18 mwaka 2007 hadi Asilimia Tisa mwaka 2012. Hali hii imechangiwa zaidi na ongezeko kubwa la matumizi ya Vyandarua vilivyowekwa Viuatilifu vya muda mrefu ambapo zaidi ya Vyandarua milioni 34 vimesambazwa katika Kaya zenye Watoto walio na umri chini ya miaka mitano na Wanawake Wajawazito. Kutokana na usambazaji huo, matumizi ya Vyandarua yameongezeka kutoka Asilimia 26 mwaka 2007 hadi Asilimia 72 mwaka 2012 kwa Watoto wenye umri chini ya miaka Mitano. Kwa Wanawake Wajawazito, matumizi ya Vyandarua yameongezeka kutoka Asilimia 27 mwaka 2007 hadi Asilimia 75 mwaka 2012. Ni dhahiri kupungua kwa kiwango cha Malaria Nchini ni jitihada za kipekee za Serikali ya Awamu ya Nne kwa kushirikiana na Wananchi na Washirika wa Maendeleo kupitia Kampeni mbalimbali za Kudhibiti Malaria.

95.         Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Wananchi na Wadau wote walioshirikiana na Serikali katika kupata mafanikio haya ambayo yanatokana na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria Nchini na Mpango wa Hati Punguzo kwa Wanawake Wajawazito  ulioanza  kutekelezwa mwaka 2008 hadi 2012. Natoa wito kwa Wananchi wote kuendeleza juhudi za Kujikinga na Malaria, hususan kwa kutumia Vyandarua vyenye Viuatilifu vya muda mrefu na kutokomeza Mazalia ya Mbu.

96.         Mheshimiwa Spika, juhudi  za  Serikali  za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI Nchini pia zimeanza kuzaa matunda. Kwa mujibu wa Utafiti wa mwaka 2011 - 2012 wa Viashiria vya Malaria na UKIMWI, maambukizi ya Virusi vya UKIMWI yamepungua kutoka Asilimia 5.7 mwaka 2007/2008 hadi Asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 kwa wanawake na wanaume wa umri wa miaka 15 - 49. Ili kuendelea kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI Nchini, Serikali inaendelea kutoa elimu  ya  UKIMWI;  kutoa  ushauri nasaha na kuhamasisha upimaji wa hiari. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaanza kutekeleza Mkakati Mpya wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013 hadi 2017 unaolenga kuwa na Sifuri tatu, yaani Kutokuwa na Maambukizi Mapya; Kukomesha Vifo Vitokanavyo na UKIMWI na Kuondoa Kabisa Unyanyapaa na Ubaguzi.  Lengo hilo litatimia iwapo sote tutabadili tabia zinazosababisha maambukizi mapya.

 

Lishe

97.         Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua thabiti za kupambana na utapiamlo hususan udumavu unaoathiri watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Katika hotuba yangu ya mwaka 2012/2013 nilieleza kwamba Serikali imezindua Mkakati wa Kitaifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015. Mkakati huo umeanza kutekelezwa kwa kuandaliwa Mpango wa Utekelezaji ulioainisha gharama na majukumu ya kila mdau katika kupunguza Utapiamlo Nchini. Pamoja na mambo mengine, Mpango huo umesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu lishe bora hasa kwa mama wajawazito na watoto wachanga, kuongeza viini lishe kwenye vyakula pamoja na kuingiza masuala ya lishe kwenye Sera na Mipango mbalimbali ya Serikali. Tayari hatua zimechukuliwa ambapo masuala ya lishe yameingizwa kwenye Mpango wa Taifa wa Uwekezaji katika Kilimo na Chakula (Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan - TAFSIP). Vilevile, Serikali inaendelea na zoezi la kuhuisha Sera ya Usalama wa Chakula na Lishe ya mwaka 1992 ili iendane na Mkakati wa Taifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011  hadi 2014/2015.

98.         Mheshimiwa Spika, tunayo kazi kubwa mbele yetu ya kupambana na tatizo la lishe duni katika maeneo yote Nchini. Takwimu zinabainisha kwamba, hakuna tofauti kubwa ya kiwango cha udumavu katika Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi na ile yenye uhaba wa chakula.  Napenda kusisitiza tena kwamba hali ya udumavu humtokea mtoto katika siku elfu moja za kwanza za uhai wake, yaani tangu kutungwa mimba hadi umri wa miaka miwili. Hivyo, tunahitaji kuimarisha utoaji elimu ya lishe kwa Wajawazito na Mama wanaonyonyesha ili wapate mlo kamili na kunyonyesha watoto wao kikamilifu hususan miezi sita ya mwanzo tangu kuzaliwa. Natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge zaidi kujiunga na Kikundi cha Wabunge kinachohamasisha umuhimu wa Lishe Bora ili kuongeza kasi na chachu ya kutoa elimu ya lishe katika maeneo yetu ya uwakilishi.

 

HALI YA UPATIKANAJI MAJI NCHINI


Huduma ya Maji Vijijini

99.         Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa maji ya uhakika na ya kutosha kwa wananchi Vijijini bado ni changamoto inayohitaji nguvu zaidi na mbinu mpya kwa kuzingatia ongezeko kubwa la watu pamoja na mabadiliko ya Tabianchi. Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imetenga na kupima maeneo ya vyanzo vya maji na kuyawekea mipaka ili kuzuia uchafuzi na uharibifu wa vyanzo hivyo.  Aidha, Vituo mbalimbali vya kuchotea maji vimeainishwa katika Halmashauri 122 na kuwekwa kwenye ramani ili vifahamike. Ujenzi wa miradi mipya, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji Vijijini pia umefanyika katika maeneo mbalimbali ili kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya Wananchi wanaoishi Vijijini ambao wanapata huduma ya majisafi, salama na ya kutosha karibu na makazi imeongezeka kutoka watu Milioni 16.3 mwaka 2006 hadi Milioni 20.6 mwaka 2012.

 

Huduma ya Maji Mijini

100.      Mheshimiwa Spika, huduma ya Maji Mijini inasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka 19 za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa, Mamlaka 109 katika ngazi  za  Wilaya,  Miji  Midogo  na  Miradi  ya  Maji  ya  Kitaifa. Serikali kupitia Mamlaka hizo imeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Miji hiyo kutoka Asilimia 84 mwaka 2010/2011 hadi Asilimia 86 mwaka 2011/2012. Katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali inaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa kupanua uwezo wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini ambapo ujenzi umefikia Asilimia 85. Kazi ya kulaza bomba  kuu  la  pili  lenye  kipenyo  cha  Meta 1.8  na  urefu  wa km 55.5, kutoka Ruvu Chini hadi kwenye matanki ya kuhifadhia maji yaliyopo eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2014.  Aidha, kazi ya usanifu wa Mradi wa Kuchimba Visima Virefu 12 katika maeneo ya Kimbiji na Visima 8 katika eneo la Mpera imekamilika  na   Wananchi   waliohamishwa  wamelipwa  fidia. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kukarabati na kujenga miradi ya maji Mijini na Vijijini pamoja na kujenga mabwawa kwa ajili ya matumizi ya majumbani na mifugo hususan katika maeneo kame.

 

TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA


Uanzishaji wa Maeneo Mapya ya Utawala

101.      Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha taratibu za kuanzisha Halmashauri Mpya 31 ili kusogeza huduma karibu na Wananchi. Halmashauri hizo ni Jiji la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Lindi na Halmashauri za Miji ya Kahama, Masasi, Makambako, Geita na Bariadi. Vilevile, imeanzisha Halmashauri za Wilaya ya Kalambo, Busega, Nsimbo, Bumbuli, Mlele, Ushetu, Msalala, Momba, Mbogwe, Kyerwa, Busokelo na Buhigwe. Halmashauri nyingine zilizoanzishwa ni Nyangh’wale, Wanging’ombe, Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Kakonko, Itilima, Uvinza, Ikungi na Kaliua. Serikali itaendelea kuzipatia Halmashauri mpya vitendea kazi, Watumishi pamoja na kujenga miundombinu muhimu hatua kwa hatua.

 

MASUALA MTAMBUKA


Vita Dhidi ya Rushwa

102.      Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kwa kuelimisha Umma  kuhusu athari za Rushwa, kuziba mianya ya  rushwa  na  kuwasihi  Wananchi  kujiepusha  na vitendo vya rushwa. Aidha, Vyombo vya Dola vimechunguza tuhuma za  makosa  ya  Rushwa  na kuwafikisha watuhumiwa mbele ya Vyombo vya  Kisheria. Hadi  kufikia  Desemba 2012, tuhuma 2,911 zilichunguzwa ambapo uchunguzi wa tuhuma 390 umekamilika na Kesi 121 zimefunguliwa Mahakamani.  Katika mwaka 2013/2014, TAKUKURU itaendelea na uchunguzi wa tuhuma zilizopo na mpya zitakazojitokeza, kuendesha Kesi nyingine zilizopo Mahakamani na zitakazoendelea kufunguliwa kutokana na kukamilika kwa chunguzi mbalimbali. Serikali pia itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za rushwa.

 

Maafa

103.      Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyoikumba Nchi yetu kwa  mwaka 2012/2013 ni ukame uliosababisha upungufu mkubwa   wa  Chakula   katika   baadhi   ya   maeneo Nchini. Kutokana na hali hiyo, Serikali ilifanyaTathmini za kina za Hali ya Chakula na Lishe Nchini na kubaini kwamba Watu 1,615,440 katika Halmashauri 47 Nchini wanahitaji msaada wa chakula. Katika kukabiliana na hali hiyo, kuanzia mwezi Julai 2012 hadi Machi 2013, Serikali imetoa Tani 69,452 za chakula cha msaada chenye thamani ya Shilingi Bilioni 26.39 kwa walengwa katika maeneo yenye upungufu. Serikali pia imetoa Shilingi Bilioni 4.6 kwa ajili ya usafirishaji wa chakula hicho.

104.      Mheshimiwa Spika, katika kurejesha hali ya kawaida kwa waathirika wa Mabomu eneo la Gongolamboto, Serikali imekamilisha ujenzi wa Nyumba 36 eneo la Msongola Wilayani Ilala  na  Nyumba  moja  eneo  la  Mbweni  Wilayani Kinondoni. Zoezi hilo kwa ujumla limegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.75. Nyumba hizo ambazo zimewekewa huduma za msingi za maji na umeme zilikabidhiwa kwa walengwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 11 Desemba 2012.

105.      Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba mafuriko yaliyotokea Dar es Salaam mwezi Desemba  2011 yalisababisha Kaya 1,007 za  waathirika waliokuwa wanaishi katika maeneo hatarishi zaidi kuhamishiwa katika eneo la Mabwepande Wilayani Kinondoni. Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea  kuwapatia huduma mbalimbali za kijamii na  kuwajengea  miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji, umeme,  shule,  zahanati na  Kituo  cha  Polisi. Aidha, hivi karibuni Serikali imetoa Mifuko 100 ya Saruji kwa kila Kaya ili kuziwezesha kujenga nyumba bora na za kudumu. Napenda kutoa wito kwa Wananchi ambao bado wanaishi mabondeni kuhama ili kuepuka athari zinazoweza kuwapata. Aidha,  Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini ziendelee kutenga maeneo yenye usalama kwa ajili ya kuwahamisha wananchi wanaokaa katika maeneo hatarishi.

 

Dawa za Kulevya

106.       Mheshimiwa Spika, biashara na matumizi ya Dawa haramu za Kulevya bado ni tatizo Nchini. Hali hii inadhihirishwa na idadi kubwa ya watumiaji walio mitaani na wale wanaojitokeza kupata tiba. Hata hivyo, kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kwa kutumia Kikosi Kazi Maalum cha Kitaifa cha Udhibiti wa Dawa za Kulevya, jumla ya Kilo 255 za Heroin na Kilo 151 za Cocaine zilikamatwa mwaka 2012 na Watuhumiwa 45 walikamatwa. Vilevile, jumla ya Ekari 184 za Mashamba ya Bangi na Kilo 3,200 za Bangi kavu ziliteketezwa na Kilo 4,840 za mirungi zilikamatwa. Katika kipindi hicho, Waathirika wa Dawa za Kulevya wapatao 20,426 walijitokeza katika Vituo mbalimbali vya tiba. Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe imekuwa ikipokea wastani wa Waathirika 400 kila mwaka.

107.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali itakamilisha Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini na kuandaa Mkakati wake wa Utekelezaji. Serikali pia itaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya Dawa za Kulevya na kupanua huduma za matibabu kwa waathirika wa Dawa za Kulevya. Wito wangu kwa jamii nzima ni kuendelea kupambana kwa nguvu zote na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kunusuru vijana wetu. Wasafirishaji na watumiaji wa dawa hizo tunaishi nao mitaani na ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwabaini na kutoa taarifa katika Vyombo vya Dola.

Ustawishaji Makao Makuu Dodoma

108.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2012/2013, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya Manispaa ya Dodoma kwa kujenga barabara zenye jumla ya Kilometa 20.6 kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu na Area A. Aidha, imekarabati mtandao wa maji wenye urefu wa Kilometa 17.5 na kusambaza umeme wa msongo mkubwa wenye urefu wa Kilometa 13.5 katika eneo la uwekezaji la Njedengwa. Vilevile, Viwanja 1,098 vimepimwa katika maeneo ya Ndachi, Ilazo C-centre, Nala Mizani, Mwangaza, Ipagala, Kizota Relini pamoja na lyumbu New Town Centre.

109.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu na Area A. Vilevile, itaendelea na ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami, usambazaji wa umeme wa msongo mkubwa pamoja na usambazaji wa mabomba ya maji safi katika eneo la Uwekezaji la Njedengwa. Pia, itapima Viwanja vipya 4,476 katika maeneo ya Nzuguni, Mkonze, Ndachi na maeneo ya Viwanda. Pamoja na kazi hizo, kazi iliyoanza ya kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma itaendelea.

 

HITIMISHO

110.      Mheshimiwa Spika, nimeelezea kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali imetekeleza kwa kipindi kilichopita. Aidha, nimetoa Mwelekeo wa Kazi zitakazofanyika mwaka 2013/2014. Kwa kuhitimisha, napenda kusisitiza mambo machache yafuatayo:

a)            Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 yameonesha kuna ongezeko la watu Milioni 10.1 kutoka watu Milioni 34.4 mwaka 2002 hadi Milioni 44.5 mwaka 2012, sawa na ongezeko la Asilimia 30. Ni dhahiri ongezeko hilo kubwa linahitaji juhudi za pamoja kati ya Serikali, Sekta Binafsi, Wadau wa Maendeleo na Wananchi kwa ujumla kuongeza uwekezaji katika huduma mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Rai yangu kwenu ni kuzitumia takwimu hizo kikamilifu katika kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.

b)            Tumebakiza miaka takribani 12 kabla ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, miaka miwili kufikia malengo ya Maendeleo ya Milenia na miaka miwili ya kukamilisha utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano. Mfumo mpya ulioanzishwa na Serikali wa kufuatilia na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kipaumbele na kufanya tathmini ya mara kwa mara ya kupima matokeo utasaidia kuharakisha kufikiwa kwa malengo hayo mapema. Serikali itahakikisha kwamba Mfumo huo unaimarisha uwajibikaji na kuleta matokeo makubwa na ya haraka katika kipindi kifupi.

c)            Jitihada za Serikali ya Awamu ya Nne katika kuvutia uwekezaji katika kilimo hususan katika Ukanda wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) zimeleta mwamko na matumaini makubwa. Azma ya Serikali ni kuona kwamba Wawekezaji wakubwa wanashirikiana kwa karibu na wakulima wadogo ili waweze kuondoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha kisasa chenye tija na cha kibiashara. Nawahakikishia Watanzania wote kwamba upatikanaji wa ardhi iliyopimwa kwa ajili ya Mkulima mdogo ndicho kipaumbele cha Serikali.


d)            Mchakato wa kuandaa Katiba Mpya umeingia katika  hatua ya kuunda Mabaraza ya Katiba katika ngazi mbalimbali yatakayopitia Rasimu ya Katiba Mpya na kutoa maoni. Tume baada ya kuzingatia maoni ya Mabaraza itaandaa Rasimu ya Katiba Mpya itakayowasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba. Natoa wito kwa wananchi watoe ushirikiano kwa Tume iweze kukamilisha zoezi hilo muhimu kwa ufanisi na kwa wakati.

e)            Amani iliyopo Nchini imetujengea heshima kubwa katika Bara la Afrika na Duniani kote. Sote tuna wajibu wa kuienzi na kuisimamia isitoweke. Serikali ya awamu ya Nne itahakikisha kwamba Amani na umoja wa Kitaifa vinadumishwa ili kuwawezesha Wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo bila hofu. Serikali haitavumilia kuona mtu au kikundi cha watu wenye dhamira mbaya wakivuruga Amani, Umoja na Mshikamano uliopo Nchini kwa kisingizio chochote. Sote tuna wajibu wa kuheshimu utawala wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
           
111.      Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza Hotuba yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelezo ya Mapitio ya Kazi zilizofanyika katika mwaka 2012/2013 na Mwelekeo  wa Kazi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2013/2014.

 

SHUKRANI

112.      Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano walionipa katika kipindi hiki. Aidha, nawashukuru Watumishi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi  Ombeni Yohana Sefue kwa kusimamia Shughuli za Serikali vizuri. Nawashukuru Watanzania wote na Washirika wetu wa Maendeleo kwa michango yao ambayo imewezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi.

113.       Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kuwashukuru Mheshimiwa  Dkt.  Mary  Michael  Nagu, Mbunge wa Hanang, Waziri wa Nchi (Uwezeshaji na Uwekezaji); Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Mbunge wa Ismani, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge); Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mheshimiwa  Aggrey Joshua Mwanry, Mbunge wa Siha, Naibu Waziri, Ofisi  ya  Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge wa Ruangwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu)  kwa  ushirikiano  walionipa katika  utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri  Mkuu. Nawashukuru  pia  Wakuu  wa  Mikoa na Wilaya  kwa jitihada walizoonesha katika kipindi  hiki. Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu, Bwana Peniel Moses Lyimo na Kaimu Katibu Mkuu, Bwana Jumanne Abdallah Sagini kwa kazi nzuri wanayoifanya. Niwashukuru Naibu Makatibu Wakuu, Bwana Charles Amos Pallangyo, na Bwana Alphayo Japan Kidata kwa ushauri wao wa Kitaalam ambao wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Nawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/2014.

114.        Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  uongozi wake mahiri na maelekezo anayonipatia katika  kutekeleza majukumu yangu. Pia ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushirikiano wao mkubwa. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wote wa Kitaifa na wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Niwashukuru sana Wapiga Kura wangu wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano wanaonipa katika kuleta maendeleo ya Jimbo letu. Nawashukuru sana!

115.        Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee, naomba uniruhusu kutumia fursa hii kumshukuru sana Mama Tunu Pinda na Familia yangu yote kwa kunitia moyo, kunivumilia kwa kila hali na kunipa nguvu katika utekelezaji wa majukumu yangu ya Kitaifa. Nawashukuru sana!!

 

MAKADIRIO YA  MATUMIZI  YA  FEDHA  YA OFISI  YA  WAZIRI MKUU, OFISI  YA  WAZIRI MKUU - TAWALA  ZA  MIKOA  NA  SERIKALI  ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE  YA MWAKA 2013/2014

 

MUHTASARI

116.       Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2013/2014 ya jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Ishirini na Tatu, Milioni Mia Nne na Moja, na Hamsini na Tisa Elfu (123,401,059,000); kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, na jumla ya Shilingi Trilioni Nne, Bilioni Mia Mbili Ishirini na Sita, Milioni Mia Moja Ishirini na Tatu, Mia Tisa Hamsini na Nne Elfu na Mia Nane na Mbili (4,226,123,954,802) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake.

117.       Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo yanafafanua kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.

118.      Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja.

No comments:

Post a Comment