Marehemu Bi Kidude
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo,
Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia taarifa za kifo cha Msanii Mkongwe
hapa nchini, Marehemu Fatma Binti Baraka Hamisi ambaye alijulikana sana kwa
jina la kisanii la Bi. Kidude aliyefariki dunia tarehe 17 Aprili, 2013 akiwa
nyumbani kwake katika eneo la Bububu, Zanzibar kutokana na kusumbuliwa na
maradhi ya Kisukari kwa muda mrefu.
“Nimepokea kwa
masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Msanii Mkongwe na Mwimbaji Mashuhuri wa
Nyimbo za Mwambao hapa nchini, Marehemu Fatma Binti Baraka Hamisi maarufu kwa
jina la Bi Kidude aliyefariki tarehe 17 Aprili, 2013 akiwa nyumbani kwake eneo
la Bububu, Zanzibar kutokana na ugonjwa wa Kisukari”, amesema Rais
Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Katika salamu
hizo, Rais Kikwete amesema alimfahamu Bibi Fatma Binti Baraka enzi za uhai wake
kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya nchi yetu katika nyanja za
Sanaa na Utamaduni ambapo alimudu kuitangaza vyema nchi yetu kupitia kipaji
chake cha uimbaji kwenye matamasha mbalimbali aliyowahi kuhudhuria na uimbaji
wake kuwa kivutio kikubwa kwa watu wengi waliowahi kuhudhuria matamasha hayo,
kuyasikiliza kwenye Radio na kuyatazama kupitia matangazo ya Televisheni.
“Kwa hakika Fani
ya Sanaa na Utamaduni imempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake ulikuwa bado
unahitajika sana katika kuinua zaidi kiwango cha uimbaji wa Muziki wa Mwambao
ambao umejizolea sifa nyingi”, amesema Rais Kikwete katika Salamu
zake na kuongeza,
“Kufuatia taarifa hizo za kusikitisha,
ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt.
Fenella Mukangara Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Wasanii
nguli wa Muziki wa Mwambao hapa nchini”.
“Vilevile
naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa Wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu
Bibi Fatma Baraka Hamisi kwa kupotelewa na mhimili madhubuti wa familia. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema
aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu. Amina”, amesema Rais
Kikwete.
Aidha Rais
Kikwete amewapa pole Wasanii wote hapa nchini ambao kwa hakika watakuwa
wameguswa sana na kifo cha Bibi Fatma Baraka ambaye alichangia vilivyo katika
kuitangaza sanaa kupitia uimbaji wa Muziki wa Mwambao. Amesema “kwa wao,
njia bora ya kumuenzi Bi. Kidude ni kuendeleza zaidi sanaa ya uimbaji wa Muziki
wa Mwambao na kuyaenzi yote mema na mazuri aliyolifanyia Taifa letu.”
Rais Kikwete
amewahakikishia wanafamilia, ndugu na jamaa wa Marehemu Fatma Baraka kuwa yuko
pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa.
No comments:
Post a Comment