Manchester United imetwaa rasmi
ubingwa wa 20 wa taji la ligi kuu soka nchini England kwa ushindi wa mabao
matatu ya aina yake dhidi ya Aston Villa,Mabao yaliyofungwa kwa ustadi mkubwa
na mshambuliaji wa kimataifa wa Uholanzi Robin Van Persie ambaye sasa atakuwa
akiongoza safu ya wafungaji kwa kufikisha mabao 24 huku Luis Suarez akifuatia
akiwa na mabao 23.
Van Persie alifunga mabao yote
matatu ndani ya dakika 31 za kipindi cha kwanza katika mchezo uliofanyika
kwenye uwanja wa Old Traford na kuwafanya United kufikisha pointi tofauti ya 16
na waliokuwa mabingwa watetezi majirani zao Manchester City,huku wakiwa na
michezo minne kibindoni.
Mkongwe Ryan Giggs alianza kwa
kumtengenezea nafasi ya goli la kwanza Van Persie dakika mbili baada ya mchezo
kuanza kabla ya Wayne Rooney kumpa nafasi nyingine nzuri Van Persie dakika ya
13 na kufunga moja kati ya mabao bora kabisa msimu huu kwa mguu wake wa kushoto
na kufanya United kuwa mbele kwa mabao mawili ndani ya dakika 15 za kwanza za
mchezo.
Alikuwa ni Giggs kwa mara nyingine
aliyempa pande Van Persie na kufunga bao la tatu dakika ya 33 ya kipindi cha
kwanza na kufanya uwanja wa Old Traford kulipuka kwa shangwe za mashabiki,kwani
ilikuwa dhahiri wamekwisha jihakikisha ubingwa msimu huu.
Hii imekuwa mara ya nne kwa
Manchester United kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka nchini Uingereza kwenye
uwanja wa Old Traford,baada ya kufanya hivyo mwaka 1999,2002 na 2009. Mara ya
mwisho United kutwaa ubingwa wa ligi kuu huku wakiwa na michezo mingi
iliyosalia ilikuwa mwaka 2001 baada ya kutangazwa mabingwa huku wakiwa na
michezo mitano kibindoni.
Huu ni ubingwa wa 13 wa taji la ligi
kuu ya Uingereza kwa kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson tangu
alipoanza kuifundisha timu hiyo mwaka 1986.
Kwa matokeo hayo Aston Villa
watasalia kwenye nafasi ya 17 wakiwa na pointi zaidi ya timu ambazo zipo kwenye
hatihati ya kuteremka daraja.
Manchester United wikiendi ijayo watapambana na
Arsenal kwenye uwanja wa Emirates wakati wakisubiri kukabidhiwa kombe lao la
ligi kuu katika mchezo wao mwisho kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Old Traford
hapo May 12 watakapokuwa wakicheza na Swansea
No comments:
Post a Comment