Margaret Thatcher, alishinda uchaguzi mkuu mara tatu
nchini Uingereza, na kuwa mama wa kwanza kuwahi kuchaguliwa kuwa Waziri
Mkuu na mmoja wa viongozi waliokuwa na ushawishi mkubwa katika karne ya
ishirini.
Utawala wake umekuwa na athari kubwa katika sera za warithi wake wa chama cha Conservertive na pia chama cha Labour.
Bi. Thatcher, ambaye alikuwa na
msimamo mkali kuhusu masuala mbali mbali na wakati mwingine kuchukua
maamuzi kutokana na hisia zake.
Bi Thather aliongoza Uingereza katika kipindi cha miaka kumi na moja.
Wakati wa utawala wake maelfu ya raia wa Uingereza walianza kushirikishwa katika masuala ya kijamii na kiuchumi.
Serikali yake iliidhinisha sheria ambayo iliwapa raia nafasi kununua nyumba zilizomilikiwa na baraza la miji.
Serikali yake pia ilipunguza hisa za serikali
katika makampuni kadhaa zikiwemo lile la kusambaza gesi British Gas na
kampuni ya mawasiliano ya simu ya British Telkom BT.
Lakini uamuzi wake wa kukataa siasa za
makubaliano ulimfanya kuwa kiongozi ambaye aliwagawanya wengi na
wanasiasa wengi walipinga sera zake na mfumo wa serikali yake hatua
iliyopelekea uasi ndani ya chama na maandamano katika barabara za miji
nchini Uingereza.
Ushawishi wa Babake.
Margaret Hilda Thatcher alizaliwa tarehe 12 mwezi Octoba mwaka wa 1925, katika eneo la Grantham, Lincolnshire.
Baba yake Alfred Robert na mama yake Beatrice Roberts walikuwa waumini wa dini ya Kimethodisti.
Babake alikuwa mmoja wa wahubiri wa kanisa hilo na pia diwani wa eneo hilo.
Robberts alikuwa na ushawishi mkubwa maishani mwa mwanawe na hasa sera ambazo alizitekeleza wakati wa utawala wake.
Bi Thatcher, alisoma katika chuo kikuu cha
Somerville College, Oxford, na kufuzu na shahada ya sayansi na kuwa mama
wa tatu kuwahi kuwa rais wa chama cha Conservative katika chuo kikuu
cha Oxford.
Baada ya kufuzu alihamia eneo la Colchester,
ambako aliajiriwa na kampuni moja inayotengeneza vifaa vya plastiki na
alijihusisha na siasa za eneo hilo za chama cha Conservative.
Mwaka wa 1949, aliteuliwa na chama hicho kuwania
kiti cha ubunge cha Dartford, katika eneo la Kent lakini alishindwa
katika uchaguzi.
Alipojaribu tena kuwania kiti hicho miaka na 1950 na 1951 Bi. Thather vile vile alishindwa.
Hata hivyo kampeini yake iliipa pigo kubwa chama
tawala cha Labour, na kama mgombea wa ubunge mchanga zaidi aliangaziwa
pakubwa na vyombo vya habari.
Mwaka wa 1951, aliolewa na mfanyabiashara Denis
Thatcher, na baada ya wakati huo alirudi chuo kikuu ambako alisomea
taaluma ya sheria kabla ya kufuzu mwaka wa 1953, mwaka ambao mapacha
wake Mark na Carol walizaliwa.
Mwaka wa 1955, kwa mara nyingine alijaribu kuwania kiti cha ubunge lakini alishindwa.
Mwaka wa 1959 akafanikiwa kushinda kiti cha ubunge cha eneo la Finchley.
Baada ya miaka miwili bungeni, Bi Thather
aliteuliwa kuwa naibu waziri na baada ya chama cha Conservative kushinda
uchaguzi wa mwaka wa 1964, aliteuliwa kuwa waziri.
Wakati Sir Alec Douglas-Home alijiuzulu kuwa
kiongozi wa chama cha Conservative, Bi Thatcher alimpigia kura Ted
Heath, katika uchaguzi wa mwaka 1965 na aliteuliwa kuwa msemaji wa
kamati ya bunge kuhusu masuala ya nyumba na ardhi.
Alifanya kampeini kali kuhakikisha kuwa
wapangaji wa nyumba za mabaraza ya miji wanaruhusiwa kununua nyumba hizo
na alikuwa mkosoaji mkubwa wa sera za chama cha Labour ambacho kilikuwa
kinatoza raia ushuru wa kiwango cha juu.
Wakati Ted Heath, alichaguliwa waziri mkuu mwaka
1970, aliteuliwa kuwa waziri wa elimu na kupewa jukumu la kupunguza
matumizi ya wizara hiyo.
Moja ya athari za mpango huo ni kuondolewa kwa
zoezi la kutoa maziwa ya bure kwa watoto wa shule walio na umri kati ya
miaka saba na kumi na moja, mpango uliopingwa na kukosolewa vikali na
wanasiasa wa chama cha Labor, huku wengi wakimwita Bi Thather ''mwizi wa
maziwa''.
Akiwa mmoja wa kina mama wachache katika siasa za Uingereza, kulikuwa na fununu kuwa huenda siku moja akawa Waziri mkuu.
Madai kama hayo pia yalienea kuhusu waziri mwingine wa Labour Shirley Williams.
Lakini kama wanasiasa wengine Bi. Thather alipuuzilia mbali madai hayo.
Katika mahojiano ya Televisheni Bi. Thather alisema haamini uwezekano wa kuwepo kwa Waziri Mkuu mwanamke katika maisha yake.
Kutokana na matatizo mengi, Serikali ya Heath haikudumu kwa muda mrefu.
Baada ya mzozo uliosababishwa na janga la mafuta
mwaka wa 1973, Bwana Heath alilazimika kuweka sheria ya kufanya kazi
kwa siku ili kukabiliana na wachimba migodi ambao walikuwa wamegoma.
Mwaka wa 1974, Februari, serikali ya Bwana Health ikasambaratika.
Mama na mwanasiasa
Bi. Thatcher, aliteuliwa kuwa waziri kivuli wa
mazingira, na kutokana na uamuzi wa bwana Heath, wa kubadili sera za
chama cha Conservertive kuhusu uchumi, Bi. Thatcher alimpinga kama
kiongozi wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka wa 1975.
Wakati alipokwenda kwa ofisi ya Bwana Heath
kumueleza kuhusu uamuzi huo, Bwana Health, hakuwa na muda wa kumtazama
na kisha akamueleza '' utashindwa''
Na kinyume ya matarajio ya wengu Bi Thatcher
alimshinda Bwana Heath katika uchaguzi wa chama, hatua iliyopelekea
kujiuzulu kwake.
Katika duru ya pili ya uchaguzi Bi. Thatcher pia
alimshinda Willie Whitelaw na kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kuongoza
chama cha kisiasa nchini Uingereza.
Tangu wakati huo, Bi. Thatcher alianza kuangaziwa pakubwa na vyombo vya habari.
Mwaka wa sabini na sita, alitoa hotuba kali
iliyokashifu sera za serikali ya Muungano wa Usovieti zilizokandamiza
raia wake na wapinzani wa serikali, hatua iliyopelekea gazeti moja
nchini Urusi kumtaja kama Iron Lady au Mama jasiri, jina ambalo lilimpa
furaha nyingi.
Mara tu alipochaguliwa ushawishi wake ulianza
kuwa mkubwa na mwaka wa 1976, alitoa hotuba ambayo aliyashutumu mataifa
yanayowakandamiza raia wake na upinzani.
Huku akiendelea kuhudumu kama mke na mwanasiasa
anayefahamu uchungu wa kuongezeka kwa gharama ya maisha kwa raia wa
kawaida, Bi. Thatcher alipinga mamlaka ya vyama vya wafanyakazi ambavyo
vilikuwa vikiitisha migomo ya mara kwa mara mwaka wa sabini na tisa.
Wakati serikali ya Bw. Callaghan ilipoanza
kuyumbayumba, chama cha Conservertive kilichapisha stakabadhi zilizokuwa
na kauli mbiu "Labour Isn't Working" yaani chama cha Labour
kimeshindwa.
Jim Callaghan, alipoteza kura ya kuwa na imani naye tarehe 28 Machi mwaka wa 1979.
Uamuzi wa Bi Thatcher, wa kuchukua msimamo
mkali, ulipokelewa na wapiga kura wengi na chama chake cha Conservertive
kilishinda uchaguzi mkuu.
Sera za Kiuchumi.
Kama waziri mkuu Bi. Thatcher alikuwa amejitolea
kulikarabati taifa hilo upya na kupunguza ushawishi wa serikali na
kuimarisha mfumo wa soko huria.
Jukumu kuu la serikali yake lilikuwa ni kupunguza mfumuko wa bei za bidhaa muhimu.
Muda mfupi baada ya kuchukua madaraka alianzisha
mpango wa kubuni sera mpya kuhusu ushuru wa bajeti na pia mpango wa
kupunguza matumizi ya serikali.
Miswada kadhaa iliwasilishwa bungeni ya
kupunguza ushawishi wa vyama vya wafanyakazi, kuvibinafsisha viwanda vya
serikali na kuruhusu wapangaji wa mabaraza ya miji kununua nyumba
wanazoishi.
Mamilioni ya watu ambao hawakuwa na jukumu
lolote katika uchumi wa Uingereza walijipata wakiwa na nyumba zao
wenyewe na walinunua hisa katika kampuni zilizokuwa zikimilikiwa na
serikali.
Sera mpya ya kiuchumi iliufanya mji wa London
kuwa moja ya miji inayokuwa kwa kasi na yenye shughuli nyingi na kuwa
kituo kilichofanikiwa kibiashara na kuwa na mfumo wa fedha thabiti
duniani.
Kampuni zilizokuwa zikitumia mifumo ya zamani
iliyosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira zilifungwa na kampuni mpya
na ya kisiasa zikaanzishwa.
Hali hii ilisababisha zaidi ya watu milioni tatu kukosa kazi.
Sera zake zilianza kuwafinya raia badala ya kuleta mageuzi na wabunge wa chama chake walianzisha vitendo vya uasi.
Baadhi yao walimshurutisha kubadilisha sera zake ili kutoa afueni kwa raia na kuokoa chama hicho kisisambaratike.
Lakini Bi Thatcer alikataa wito huo, mwaka wa
1980 aliambia mkutano mkuu wa chama hicho kuwa, wale wanaosubiri
kubadili sera zake, watasubiri kwa muda mrefu zaidi kwa kuwa hana nia
wala mpango wa kufanya hivyo.
Vita vya Falklands
Kufikia mwaka wa 1981, umaarufu wake ulikuwa
umepungua hadi asilimia 25%, kiwango ambacho ni cha chini zaidi kwa
waziri mkuu yeyote.
Hata hivyo uchumi wa Uingereza ulikuwa umeanza kuonyesha dalili za kuiamarika.
Mwaka wa 1982, uchumi wa Uingereza uliimarika na umaarufu wake miongoni mwa wapiga kura ukapanda juu mara nyingine.
Uamuzi wake pia wa kuidhinisha vita dhidi ya Argentina kuhusiana na umiliki wa visiwa vya Falkland, ulimpa umaarufu mkubwa.
Bi. Thatcher aliagiza jopo maalum la wakuu wa
jeshi kwenda katika kisiwa hicho na tarehe 14 mwezi Juni wanajeshi wa
Argentina walitangaza kuwa wameshindwa katika vita hivyo.
Ushindi katika vita hivyo vya Falkland, na mzozo
ndani ya chama cha Labour, kwa wakati huo kikiongozwa na Michael Foot,
kiliipa chama cha Conservertive ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka
wa 1983.
Mwaka uliofuatia chama cha wafanyakazi wa migodi
waliitisha mgomo wa kitaifa lakini Margaret Thatcher kwa wakati huu
hakutaka kufanya kosa.
Kinyume na ilivyokuwa wakati wa utawala wa
Edward Heath, mwaka wa sabini na tatu, serikali ya Uingereza ilikuwa
imeweka hifadhi ya kutosha ya mkaa katika viwanda vyake vya kuzalisha
umeme, kabla ya mgomo huo kuanza.
Hivyo mgomo huo haukuwa na athari kubwa kwa shughuli za uzalishaji wa umeme na kupelekea mgomo huo kumalizika haraka.
Kulikuwa na makabiliano makali kati waandamanaji na polisi lakini mgomo huo ulimalizika mwezi Machi mwaka uliofuatia.
Tangu wakati huo, jamii nyingi zinazotegemea
uchimbaji wa madini ya makaa zilishindwa kujiimarisha kutokana na athari
za mzozo huo ambao ulichangia pakubwa kusamabaratika kwa secta ya
uchimbaji wa makaa.
Katika eneo la Ireland ya Kaskazini Bi. Thatchet
alikabiliwa na mgomo wa kususia chakula kutoka kwa wafuasi wa chama cha
IRA, na msimamo wake mkali kuhusu kundi hilo uliakasirisha wanasiasa
wasiogemea upande wowote na wakosoaji wake wanadai kuwa uamuzi huo
ulichochea waumini wengi wa kanisa la Katoliki nchini Ireland ya
Kaskazini kujihusisha na Ghasia.
Licha ya kujaribu kuzima uasi uliosababishwa na
mzozo huo, kwa kuwapa viongozi wa Ireland, nafasi ya kuongoza mikakati
ya amani, juhudi hizo zilisambaratika kutokana na upinzani mkali kutoka
kwa vyama vya wafanyakazi.
Mwezi Oktoa mwaka wa 1984, bomu lililotegwa na
wafuasi wa IRA lililipuka katika mkutano wa chama cha Conservertive
uliokuwa ukiendelea katika hoteli moja mjini Brighton.
Watu watano waliuawa na wengine kujeruhiwa vibaya akiwemo waziri wa serikali Norman Tebbit.
Na kama kawaida yake Bi Thatcher, alisisitiza
kuwa atachukua hatua kali kujibu shambulio hilo, wakati wa hotuba yake
kwa wajumbe waliokuwa wakihudhuria mkutano huo, saa chache tu baada ya
kutoka kwa shambulio hilo.
''Shambulio hilo limeshindwa. Juhudi zote za
kushambulia na kuharibu demokrasia yetu kupitia vitendo vya kigaidi
vitashindwa'' Alisema Bi. Thatcher.
Sera yake ya nchi za kigeni, ilinuia kujenga
hadhi na ushawishi wa Uingereza katika mataifa ya ng'ambo, jambo ambalo
aliamini ilishuka sana chini ya serikali iliyotangulia ya Labour.
Bi Thatchter alipata mshirika wa karibu, rais wa Marekani, Ronald Reagan, ambaye alikuwa na sera za kiuchumi sawa na zake.
Vile vile alishirikiana kwa karibu na rais wa
Urussi Mikhail Gorbachev, ambaye alikisiwa kuwa rais aliyeleta
mabadiliko makuu Urusi.
Chama cha Labour ambacho kwa wakati huo kilikuwa
kikiongozwa na Neil Kinnock, hakikuwa kimejinusuru kutoka kwa malumbano
na mizozo kati ya viongozi na wabunge wake, hatua iliyompa Bi. Thatcher
fursa nzuri ya kushinda awamu ya tatu kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza
wakati wa uchaguzi wa mwaka 1987.
Na baada ya kuchaguliwa, kitu cha kwanza
alichofanya ni kuanzisha ushuru unaotozwa kwa nyumba na majengo ambao
ulikuwa sawa kwa kila mtu ili kugharamia shughuli za mabaraza ya miji.
Ushuru huo ulitozwa kulingana na wale wale wanaoishi katika nyumba hizo bila kuzingatia dhamani ya nyumba au uwezo wao..
Mpango huo ulisababisha maandamano mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Uingereza.
Wabunge wa chama chake ambao walihofia kupoteza
viti vyao, kutokana na ushuru huo, hawakuwa na njia mbadala ya kufutilia
mbali sera hiyo huku Bi Thatcher akiwa madarakani.
Mwaka wa 1989 alinusurika jaribio kutoka kwa
wabunge wa chama chake la kumuondoa madarakani, ishara kuwa utawala wake
na chama chake ulikuwa umeanza kukabiliwa na matatizo ya ndani.
Suala la muungano wa ulaya hatimaye ndio lililosababisha kusambaratika kabisa wa serikali yake.
Miaka ya baadaye.
Alipandishwa cheo na kupewa cheo cha Baroness
Thatcher wa kaunti Kesteven katika Kuanti ya Lincolnshire, na
alikabithiwa tuzo hilo mwaka 1995.
Aliandika vitabu viwili kuhusu maisha yake akiwa
siasa, kampeini dhidi ya azimio la Maastricht Treaty na kupinga sera ya
serikali ya Serbian ya kuwaangamiza raia wa nchi hiyo wenye asili ya
Bosnia.
Mwaka wa 1997 alimpendekeza William Hague kuwa
kiongozi wa chama cha Conservative lakini alishindwa kumuunga mkono
mrithi wake, Iain Duncan Smith.
Wakati afya yake ilianza kudhohofika, Bi Thatcher alianza kupunguza shughuli zake za umma kuanzia mwaka wa 2001.
Baada ya kukumbwa na mshtuko wa moyo mara
kadhaa, madaktari wake walimshauri kupunguza shsughuli zake za umma na
hali yake haijakuwa ya kuridhisha.
Bi Thatcher pia aliigua ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu hali iliyoadhiri pakubwa uwezo wake kwa mujibu mwa mwanae Carol.
Wakati mume wake Dennis, ambaye amemtaja kama
nguzo yake kuu, alipoaga dunia mwaka wa 2003 akiwa na umri wa miaka 88,
Bi Thatcher alimlimbikiza sifa chungu nzima.
'' Kuwa Waziri mkuu ni kazi ambayo ina upweke wa
hali ya juu. Katika hali moja hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa kwa kuwa
hauwezi kuongoza ukiwa kwenye umati. Lakini Denis alipokuwa hai sikuwa
peke yanagu. Alikuwa mwanamme kamili na mume na zaidi ya wote alikuwa
rafiki wangu mkuu'' Alisema Bi Thatcher.
Mwaka mmoja baadaye alisafiri nchini Marekani
kumuaga mshirika wake wa Karibu kisiasa, Ronald Reagan katika mazishi
yaliyofanyika mjini Washington juni mwaka wa 2004.
Bi Thatcher aliendelea kujitokeza hadharani, na
tukio kubwa zaidi ni uzinduzi wa sanamu yake mwenyee iliyojengwa katika
Bunge la wawakilishi, kitendo ambacho ni cha kwaza cha iana yake kwa
waziri mkuu wa zamani ambaye angali hai akitunukiwa heshima kama hiyo.
Kwa mara nyingine alirejea tena katika iliyokuwa
ofisi yake iliyoko katika barabara ya Downing hapa London, baada ya
Waziri mkuu Gordo Brown kumualika muda mfupi baada ya kuteuliwa kuwa
waziri mkuu.
Mwaka wa 2010 Bi Thather alirejea tena katika
ofisi hiyo akiwa mgeni wa waziri mkuu David Cameron ambaye alikuwa
kiongozi mpya wa serikali ya muungano.
Wanasiasa wachache sana ambao wamewahi kuwa na
ushawishi sawa na wa Bi Thatcher wakati wa utawala wake na vile vile ni
wanasiasa wachache sana ambao wameweza kuwa na uwezo kama wake.
Kwa wakosoaji wake Bi Thatcher alikuwa
mwanasiasa ambaye aliweka sera ya soko huria kuliko vitu vyote na
alikuwa tayari kuruhusu watu wengine kugharamia sera zake au kuhangaika
ili afanikishe sera zake.
Hii ilijitokeza sana kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wasiokuwa na kazi na pia migomo ya wafanyakazi.
Wafuasi wake nao wanamsifu kwa kupunguza
matumizi ya serikali, kupunguza ushawishi viongozi wa vyama vya
wafanyakazi na kurejesha hadhi ya heshima ya Uingereza Duniani.
Alikuwa mwanasiasa ambaye alikuwa na kipaji cha pekee na ambaye alikuwa tayari kutetea maamuzi yake mazuru au hata mabaya.
Mfumo wake wa kutokubali kushawishiwa ulikuwa ndio nguzo ya nguvu yake kisiasa na upungufu wake mkubwa.
No comments:
Post a Comment