Na Adili Mhina, Kigoma
Serikali imewaonya
watumishi wasio waaminifu katika kusimamia na kuratibu miradi inayotekelezwa
kwa fedha za washirika wa maendeleo kuepukana na vitendo vya rushwa na
ubadhirifu kwani Serikali ya Awamu ya Tano haina huruma wala msamaha kwa watu
wa aina hiyo.
Onyo hilo limetolewa
mwishoni mwa juma na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machura
wakati akifunga mafunzo ya maandalizi ya miradi ya maendeleo kwa ajili ya
ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa mkoa wa Kigoma yaliyofanyika mjini hapa
na kuendeshwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Tume ya Mipango
kwa ufadhili wa Serikali ya Ubelgiji.
Mafunzo hayo
yalishirikisha Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Makatibu tawala wa
wilaya, Wakuu wa Idara za Mipango, Wachumi, Maafisa Mipango na Watakwimu ambao
wana majukumu ya usimamizi na uratibu wa miradi katika sekretarieti ya Mkoa wa
Kigoma na Halmashauri zake zote.
Machura alieleza kuwa Serikali
ya sasa haina nafasi ya kuwalea watendaji ambao wanaweka maslahi yao mbele
badala ya kuangalia wananchi katika kutekeleza miradi inayofadhiliwa na
washirika wa maendeleo kitu kinachopelekea miradi mingi kutekelezwa chini ya
kiwango bila kuzingatia thamani ya fedha.
Alieleza kuwa baadhi ya
watumishi walifikia hatua ya kuandaa maandiko ya kuomba fedha za ufadhili wa
miradi ya maendeleo ya wananchi lakini fedha hizo zikipatikana walikuwa
wanagawana na kuzitumia katika shughuli zao binafsi badala ya kuzingatia
malengo ya fedha hizo.
“Tulifika pabaya sana,
watu walikuwa wanaandika proposal (andiko) kwa wafadhili ili wapate fedha za
kutekeleza miradi ya wananchi lakini cha ajabu unakuta fedha zikipatikana
wanagawana bila aibu kwa kuwa zimetoka nje, katika serikali ya sasa watu wa
aina hiyo hawana nafasi kwenye utumishi wa umma,” alieleza Bw. Machura.
Alisisitiza kuwa
viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa hawana budi kuzingatia mafunzo
waliyopata kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kusimamia miradi na kuleta
maendeleo katika maeneo yao ya utawala ili wafadhili waendelee kuamini kuwa
fedha zote wanazotoa zinatekeleza miradi iliyokusudiwa.
“Tukifanya hivyo
Serikali ya Ubelgiji pamoja na wadau wengine wa maendeleo watakuwa tayari
kuongeza michango yao katika kuusaidia mkoa wetu kujikomboa kutoka katika
umaskini hususan kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo”,
alisistiza.
Kwa upande wake mratibu
wa mafunzo hayo ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia Klasta ya
Biashara za Kimataifa na Mahusiano ya Uchumi Tume ya Mipango, Bw. Paul Sangawe
alibainisha kuwa kuna baadhi ya watendaji ambao hawatoi taarifa za matumizi ya
fedha za miradi ya ufadhili kwa wakati, kitu ambacho kinarudisha nyuma jitihada
za washirika wa maendeleo katika kufadhili miradi.
Kutokana na hali hiyo,
Sangawe alishauri uongozi wa Ofisi ya Mkoa wa Kigoma kujiwekea utaratibu wa
kukaa na halmashauri zake mara kwa mara ili kuangalia maendeleo ya miradi
inayotekelezwa kwa fedha za washirika wa maendeleo na kuhakikisha utekelezaji
wake unakwenda sambamba na malengo husika.
Aidha, Sangawe
alisisitiza kuwa ni lazima mamlaka zinazohusika katika kufanya makubaliano ya
mikataba na wafadhili kuwa makini na kuzingatia kuwa miradi inayotaka
kufadhiliwa ni ile yenye tija kwa wananchi na ambayo inaharakisha kufikia
malengo ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati.
“Tusisite kukataa miradi
ambayo haina tija kwa wananchi wetu, hata kama fedha ni zao lakini lazima
ufadhili wao uendane na vipaumbele tulivyojiwekea kama Taifa. Tusipo zingatia
hilo tutajikuta tunatekeleza miradi isiyo na faida kwa wananchi na kupelekea
Serikali kupata hasara,” alisisitiza Sangawe
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kigoma, Daniel Machura
akitoa hotuba ya kufunga mafunzo ya miradi
ya maendeleo kwa ajili ya ufadhili wa washirika wa maendeleo kwa Mkoa wa
kigoma. Kulia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Dk Wilhelm Ngasamiaku
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kushoto ni Mratibu wa mafunzo hayo, Paul Sangawe kutoka Tume ya Mipango.
Mratibu wa Mafunzo, Paul Sangawe akitoa
muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa
siku tano. Katikati ni Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma Daniel Machura na kulia ni mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Dk Wilhelm Ngasamiaku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Mchumi kutoka Wizara ya Fedha
na Mipango - Tume ya Mipango, Senya Tuni akionesha kitabu cha Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21) kwa washiriki wakati akiwasilisha mada juu ya Mpango huo.
Washiriki wakifanya mazoezi ya kanuni
zinazotumika kuchagua miradi sahihi kwa ajili ya kupata ufadhili kutoka kwa
washirika wa maendeleo. Mazoezi hayo yalifanyika mapema kabla ya kuhitimishwa
kwa mafunzo hayo
Mmoja wa washiriki akichangia
mada kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki akichangia
mada kabla ya kuhitimishwa kwa mafunzo hayo
No comments:
Post a Comment