Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, Bahame Tom Nyanduga,
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(THBUB) imepokea tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli alilolitoa Septemba 11, 2017 kuhusu kutotekeleza adhabu ya
kifo wakati wa uongozi wake, kuwa ni tamko lenye kuzingatia haki ya msingi ya
kuishi.
Tume inapenda kuungana na wadau wengine
kumpongeza Rais kwa tamko hilo ambalo limekuja muda mfupi kabla ya Siku ya
Kimataifa ya kuhamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kufuta adhabu ya
kifo, ambayo huadhimishwa Oktoba 3 ya kila mwaka.
Uamuzi wa Rais unaendana na Mkataba
wa Kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa yanayozitaka nchi wanachama kufuta
au kusimamisha utekelezaji wa adhabu ya kifo (abolition/moratorium on the death
penalty).
Tume inatambua kwamba adhabu ya kifo
haijatekelezwa hapa nchini katika kipindi cha takriban miaka 20 iliyopita na
hivyo kudhihirisha kwamba Tanzania ni nchi isiyotekeleza adhabu ya kifo kwa
hiari yake yenyewe pamoja na uwepo wa adhabu hiyo katika sheria za nchi.
Kwa kuzingatia kauli ya Rais pamoja
na mahitaji ya sheria za kimataifa za haki za binadamu, Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora inapenda kuchukua nafasi hii, kuishauri Serikali
iridhie Itifaki ya pili ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa;
Itifaki ambayo inazitaka nchi wanachama kufuta adhabu ya kifo.
No comments:
Post a Comment