THE
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
Fax: 255-22-2113425
|
![]() |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE
STATE HOUSE,
P.O. BOX
9120,
DAR
ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Burundi
yamtunukia Tuzo Mwalimu Nyerere
Rais
Kikwete apokea Tuzo kwa niaba yake
Taifa
la Burundi limemtunukia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere Tuzo la juu
kabisa ambalo Burundi hutoa kwa watu mbali mbali kutokana na mchango wake
katika kuleta uhuru na baadaye kwa jitihada zake kubwa za kuleta amani katika
nchi hiyo.
Mwalimu
Nyerere alitunukiwa Tuzo hilo – Tuzo la Taifa la Burundi (Order of the National Republic of Burundi) - kwenye Kilele cha Sherehe za Kuadhimisha
Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi zilifanyika jana, Independence Road, pembeni mwa
Uwanja wa Michezo wa Louis Rwagasore mjini Bujumbura na kutangazwa hadharani
kwa maelfu kwa maelfu ya watu waliohudhuria sherehe hizo.
Tuzo
hiyo ya Mwalimu imepokelewa kwa niaba yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alikuwa mmoja wa viongozi sita
wa nchi za nje waliohudhuria sherehe hizo.
Akitangaza
Tuzo hilo, Rais wa Burundi, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza alisema kuwa Burundi
imeamua kumtunuku Mwalimu Nyerere sababu mbili – moja ni ushauri wake muhimu
sana katika kuleta uhuru wa Burundi kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji.
“Kwanza
Mwalimu alikuwa mshauri muhimu sana wa Mwanzilishi wa Taifa letu, Mheshimiwa
Louis Rwagasore na baadaye zilikuwa ni jitihada zake ambazo hatimaye zimeleta
amani na utulivu ambao tunaufurahia katika Burundi kwa sasa,”
Pamoja
na Hayati Mwalimu, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela pia
amepata tuzo hiyo. Mzee Mandela alichukua nafasi ya Mwalimu kama mpatanishi wa
mgogoro wa Burundi kufuatia kifo cha Mwalimu mwaka 1999.
Katika
sherehe hizo, zilizoendelea mfululizo kwa saa saba unusu tokea saa nne asubuhi
hadi saa 11 jioni, Rais Kikwete aliungana na viongozi wenzake wa nchi sita na
wawakilishi wa nchi nyingine nyingi duniani kuhudhuria kilele cha sherehe za
kufana kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi.
Burundi
ilipata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji Julai 2, mwaka 1962 na Rais
Kikwete aliwasili Bujumbura asubuhi ya jana, akitokea Kigali, Rwanda, ambako
pia alihudhuria sherehe kama hizo Kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa
Rwanda iliyopata uhuru Julai Mosi, 1962, kutoka kwa wakoloni hao hao wa
Kibelgiji.
Tofauti
na Rwanda ambako Rais Kikwete alikuwa rais pekee aliyehudhuria sherehe za uhuru
wa nchi hiyo na mgeni rasmi, katika sherehe za Burundi, Mheshimiwa Rais na Mama
Salma Kikwete wameungana na Rais mwenyeji Pierre Nkurunzinza, Rais Mwai Kibaki
wa Kenya, Rais Theodore Obing Nguema wa Equatorial Guinea, Rais Joseph Kabila
wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya
Afrika ya Kati na Rais Shariff Sheikh Ahmed Shariff katika kusherehekea uhuru
wa Burundi.
Walikuwepo
wawakilishi wa nchi nyingine nyingi duniani akiwamo Makamu wa Rais wa Uganda na
Makamu wa Rais wa Nigeria, Mheshimiwa Prince Philip ambaye ni mtoto wa Malkia
wa Belgium, Waziri Mkuu wa Swaziland na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika (AU) anayemaliza muda wake, Mheshimiwa Jean Ping.
Wananchi
wa Burundi wamejitokeza kwa wingi sana kuhudhuria sherehe za uhuru wa nchi yao
ambayo tokea mwaka 1965 yalipotokea mapinduzi ya kijeshi ya kwanza haijapata
kuwa na raha ya kuwa na amani kwa miaka 10 mfululizo ukiondoa sasa.
Moja
ya mambo ambayo yamechukuwa muda mrefu kiasi cha saa tatu ni maandamano ya
wananchi wa Burundi ambayo yameshirikisha vikundi vya wananchi kutoka taasisi
mbali mbali zikiwamo Idara za Serikali, Makampuni Binafsi na Taasisi Zisizokuwa
za Kiserikali.
Askari
wa miavuli wakiwa wamebeba bendera za Taifa la Burundi pia wamekuwa kivutio
kikubwa katika sherehe hizo kama yalivyokuwa maonyesho ya makomando wa Jeshi la
Anga la Burundi (BAF) kutoka kwenye
helikopta iliyosimama angani hadi chini kiasi cha urefu wa mita 150.
Aidha,
ngoma aina ya Rukinzo ilivutia sana wananchi kama lilivyokuwa gwaride la nchi
tano Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambako kila kundi la askari
wakiongozwa na kundi la askari wa Burundi lakini kila kundi likiwa chini ya
kamanda wake lilipita mbele ya viongozi na maelfu kwa maelfu ya wananchi
waliohudhuria sherehe hizo.
Mbali
na ngoma za vikundi vya ngoma za asili na utamaduni wa Burundi zimevutia sana
hisia za wananchi, pia wananchi kwenye
sherehe hizo wameshuhudia gwaride la kuvutia la Jeshi la Burundi likiwa na
vikosi mbali mbali kikiwemo Kikosi cha Kulinda Amani katika nchi mbali mbali
duniani. Aidha, gwaride hilo limeshirikisha Jeshi la Polisi ambalo lilionyesha
vifaa vya huduma mbali mbali ambazo hutolewa na Jeshi hilo kulinda usalama wa raia zikiwamo za usalama
barabarani, huduma za zima moto na huduma za magari ya kubeba wagonjwa.
Jeshi
la Burundi pia limetumia nafasi ya sherehe hizo kuonyesha vifaa vinavyotumiwa
na vikosi vya Jeshi hilo ambavyo ni Jeshi la Ardhini, Jeshi la Maji na Jeshi la
Anga ikiwa ni pamoja na helikopta mbili za kijeshi –helicopter Gun Ships.
Rais
Nkurunziza, mwenyeji wa sherehe hizo, ambaye alianza kuhutubia Taifa la Burundi
kiasi cha saa 10 mchana, alitumia muda wa kutosha kuisifia Tanzania na uongozi
wake wa awamu mbali mbali kwa mchango wake mkubwa katika uhuru wa Burundi na
baadaye katika mazungumzo ya kuleta amani katika Burundi.
Alimsifia
Rais Kikwete kama Rais wa nchi rafiki na jirani na kama “kaka yangu” katika
hotuba hiyo ambako alitangaza kumtunukia medali ya juu kabisa katika Taifa la
Burundi Mwalimu Nyerere kwa mchango wake katika Uhuru wa Burundi na baadaye
katika kuleta amani ya nchi hiyo.
Rais
Kikwete anatarajiwa kuondoka mjini Bujumbura baadaye leo, Jumanne, Julai 3,
2012, kurejea nyumbani.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
3 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment