Waziri Kivuli wa Maji Sabrina Sungura
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI
YA UPINZANI, MHESHIMIWA SYLVESTER MHOJA KASULUMBAYI (MB) WIZARA YA MAJI KUHUSU MAPITIO
YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
mwanzo kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuweza kusimama hapa
mbele yenu hivi sasa na kutoa maoni ya kambi ya upinzani kuhusiana na bajeti ya
wizara ya ya maji kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kwa mujibu wa kanuni za Bunge
kanuni ya 99(7) toleo la mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika,
niwashukuru viongozi wetu. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe kwa imani kubwa kwetu na kututeua kuwa wasemaji wa wizara hii muhimu kwa
maendeleo ya nchi yetu; aidha nimshukuru , Mh. Zitto Zuberi Kabwe (Mb), Naibu
Kiongozi wa Upinzani na Mheshimiwa Tundu
Lissu (Mb), Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Tunawashukuru kwa
kutuongoza vema kutimiza majukumu yetu kwa wananchi wetu wote. Pia nawashukuru
wote waliotoa mchango wao katika kuandaa hotuba hii muhimu sana.
Mheshimiwa Spika,
sambamba na hilo niwashukuru wananchi wa mkoa wa kigoma kwa ujumla kwa
ushirikiano wanaotupatia katika kutimiza majukumu yetu sisi wabunge tutokao
mkoani humo. Nasema asanteni sana nanina waahidi kuendelea kuwasemea juu ya
kero zenu kwa kipindi chote nitakachokuwa
bungeni. Pia naishukuru familia yangu kwa ushirikiano wote wanaonipa kwa
kipindi chote cha majukumu yangu na kwa wakati huu ambapo nafanya shughuli za
uwakilishi wa wananchi bungeni. Nawakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika,
mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa, nakupongeza wewe binafsi kuweza kuongoza
vyema Bunge hili la Kumi lenye changamoto nyingi.
2.0 MAPITIO YA BAJETI YA
MAENDELEO KWA MWAKA 2011/2012 NA MAPENDEKEZO KWA MWAKA 2012/2013.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Maji ni kuwa wananchi wanaopata huduma ya
maji safi na salama ni asilimia 86 katika miji mikuu ya mikoa na asilimia 57.8
vijijini. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam upatikanaji wa maji safi ni
asilimia 55 tu. Taarifa hizi zinatia wasiwasi kwani nchi yetu ina rasilimali za
maji za kutosha ila tatizo ni vipaumbele vyetu katika kutumia rasilimali
zilizopo.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa Dar es Salaam hali hii haikubaliki kwani vyanzo vya maji kwa
ajili ya jiji la Dar es Salaam vimepatikana na maji mengi chini ya ardhi
yamegunduliwa kwenye maeneo ya Kimbiji na Mpera. Ila mpaka leo hii vyanzo hivi
havijatumika kikamilifu katika kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuweza kupata
maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, Bunge
liliidhinisha fedha za ndani kwa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/2012
kiasi cha shilingi bilioni 41.6 fedha za ndani, na fedha za nje shilingi bilioni 387.1. Kwa hali hii, ni dhahiri kuwa serikali imeamua
kuachia jukumu la kutoa huduma ya maji kwa wananchi wake kwa kutegemea fedha za
wafadhili na wahisani wa nje badala ya kutenga fedha za ndani za kutosha ili
kuweza kuokoa wananchi ambao wanaathirika kutokana na kukosa maji safi na
salama kutokana na miradi hii ya wafadhili kutokutekelezwa kwa wakati na mfano
ni mradi wa maji wa Benki ya Dunia kila wilaya.
Mheshimiwa Spika,
kazi ya kutoa huduma za kijamii duniani kote ni kazi ya Serikali inayokusanya
kodi. Kitendo cha Serikali kutegemea mashirika ya nje kugharamia huduma za
kijamii kama maji kwa wananchi wetu si sahihi kwa sababu ama mashirika hayo
huchelewesha misaada hiyo au misaada haiji kabisa, kwa mwaka 2011/2012 fedha za
nje zilikuwa shilingi bilioni 387.1 wakati za ndani zilikuwa shilingi bilioni
41.6, mwaka huu 2012/2013 fedha za nje ni shilingi bilioni 325.7 za ndani ni
shilingi bilioni 140.
Kambi ya Upinzani,
inaitaka serikali iondokane na utaratibu
huu wa kutegemea wafadhili kwenye huduma muhimu kama ya maji; badala yake
zitengwe fedha za ndani za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wananchi wetu
wanapata maji safi na salama, na hasa ikizingatiwa kuwa kwa mujibu wa tafiti
mbalimbali maji ndio yameonekana kuwa kero kuu kwa wananchi wetu .
Mheshimiwa Spika,
takwimu zinaonyesha kuwa mradi wa programu ya maji vijijini kwa mwaka 2011/2012
ulitengewa jumla ya shilingi bilioni
50.8 wakati program ya maji safi na maji taka mijini ilitengewa jumla ya
shilingi bilioni 313.55.
Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka huu wa fedha, 2012/2013, programu ya maji vijijini imetengewa fedha za ndani jumla ya shilingi bilioni 9.6
na fedha za nje shilingi bilioni 27.2 na program ya maji safi na maji taka ni
shilingi bilioni 126.8 za ndani na shilingi bilioni 245.2 fedha za nje.
Mheshimiwa Spika,
upangaji mipango na ugawaji wa raslimali fedha usiozingatia uwiano wa hali
halisi ya mahitaji ni kosa kubwa ambalo litaendelea kukandamiza jamii ziishizo
vijijini. Takwimu zinatuonyesha kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi
vijijini (31,809,808) na ndio wenye shida kubwa ya maji ikilinganishwa na wale waishio
mijini. (Chanzo;
Randama ya Wizara ya Maji, mpango wa bajeti ya kwa mwaka 2012/2013)
Mheshimiwa Spika,
pamoja na tatizo kubwa la maji mijini lakini hali ni mbaya zaidi vijijini na
hili linathibitishwa na kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge Juma Nkamia kuwa
kwa sasa wananchi kwenye moja ya vijiji vilivyopo jimboni mwake wanabadilishana
kati ya debe la mahindi na ndoo ya maji. Hali hii haikubaliki kwa taifa ambalo
lina vyanzo vya kutosha vya maji kama vile mito, maziwa na chemichemi nyingi za
asili na za kutosha.
Kwa sababu hiyo basi,
Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali
kuanzia bajeti hii kuanza kuangalia ugawaji
wa fedha kwa uwiano kati ya programu ya maji vijijini na programu ya maji safi
na maji taka mijini ili kuwawezesha wananchi wa vijijini kupata huduma ya maji,
kwani kwa hali ilivyo ni kuwa uwiano wa mgawanyo wa fedha za miradi ya
maendeleo baina ya mijini na vijijini ni 1:10 .
3.0 HALI YA SEKTA YA MAJI
3.1 Uhaba wa Wataalamu wa Maji.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni kuwa wataalamu wa maji waliopo wengi ni wale
ambao walisomeshwa wakati wa miaka ya 70 wakati wa kutekeleza mpango kabambe wa
maji wa miaka 20 , kwani Julai 1974, Chuo cha Maji kilianzishwa rasmi kikiwa na
wanafunzi 30 na wakafuatiwa na wanafunzi wengine 60 mwezi Machi 1975.
Mheshimiwa Spika,
kozi za wanafunzi zilikuwa ni Hydrolojia, Hydrojiolojia na Ujenzi na
zilikuwa ni za miaka mitatu kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne. Kila
aliyemaliza alipata stashahada ya Water Resources Engineering kwa
fani hizo. Ilitarajiwa kuwa Chuo kingedahili wanafunzi 250 kila mwaka, lakini
kiwango cha juu kilicho fikiwa ni wanafunzi 128 tu waliodahiliwa mwaka 1983.
Mheshimiwa Spika,
wanafunzi 129 walipelekwa nchini India kwa mafunzo ya Shahada ya Uhandisi wa
Maji katika Chuo Kikuu cha Roorkee, chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden
ikishirikiana na Serikali za India na Tanzania.
Mheshimiwa Spika,
sekta ya maji imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa wataalam wa
kutosha katika fani mbalimbali za masuala ya maji. Kwa sasa kwa mujibu wa
taarifa za wizara ni kuwa mahitaji ya watalaam hao ni: Sekretariati ya Mikoa
zinahitaji wataalam 63, wanatakiwa wahandisi 560 na mafundi sanifu katika fani
za maji zaidi ya 1,700 katika ngazi za Halmashauri ya Wilaya. Kwa upande wa
usimamizi wa rasilimali za maji, changamoto kubwa iliyopo ni kukosa wataalamu
wa ngazi ya juu kutokana na wengi wao kumaliza kipindi chao cha utumishi kwa
wakati mmoja.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu ni kwanini serikali iliamua kuachana na
utaratibu wa kusomesha vijana wetu kwa kuwapa ufadhili haswa kwenye sekta ya
maji ili kuiweza kukabiliana na changamoto hii. Aidha, tunataka kujua mwaka huu
wa fedha wizara inajiandaa kusomesha vijana wangapi ili kuweza kukabiliana na
changamoto ya upungufu wa wataalamu hawa? Kwani taarifa zilizopo ni kuwa wengi
wamestaafu na hakuna waliokuwa wameandaliwa kuchukua nafasi.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
imejaliwa kuwa na vyanzo vya kutosha vya maji kuweza kutosheleza mahitaji ya
watanzania wote kwa kipindi chote cha mwaka, vyanzo hivyo ni maji yaliyo juu ya
uso wa ardhi na yaliyochini ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, matumizi
ya maji kwa nchi yetu kwa takwimu za mwaka 2002 yalikadiriwa kuwa ni mita za
ujazo milioni 5,142. Kati ya hizo kilimo kilitumia mita za ujazo milioni 4,624
(karibu asilimia 90 ya maji yote) kati ya ujazo huo, mita za ujazo
milioni 4,417 zilitumika kwa umwagiliaji
na mita za ujazo milioni 207 kwa
ajili ya mifugo, kiasi kilichobaki cha
mita za ujazo milioni 493 ndicho
kilitumika kwa matumizi ya viwandani na majumbani.
Mheshimiwa Spika,
uzalishaji wa maji umefikia mita za ujazo 304,443 kwa siku kwa mwaka 2011
japokuwa mahitaji ya maji ni mita za ujazo 468,051 kwa siku hii maana yake ni
kuwa kuna upungufu wa uzalishaji wa maji kulingana na mahitaji ya kiasi
kinachohitajika kwa matumizi kwa siku.
Mheshimiwa Spika, mchango
wa sekta ya maji katika pato la taifa kwa mwaka 2011 ulipungua na kuwa asilimia
0.3 kwa kulinganisha na asilimia 0.4 kwa mwaka 2010. Hii maana yake ni kwamba shughuli nyingi za uzalishaji
zinazotegemea maji ili kutoa tija, zilishindwa kuzalisha kwa kadri ya uwezo
wake kutokana na sababu mbalimbali nyingine zikiwa ni ukosefu wa mipango na
mikakati thabiti.
Mheshimiwa Spika,
mchango wa fedha za ndani katika bajeti ya maendeleo kwenye sekta ya maji kwa kipindi cha miaka minne (2007 hadi
2011), takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2005/2006 mchango wa fedha za ndani
kwenye bajeti ya maendeleo ya sekta ya maji ilikuwa 57% na mwaka 2008/2009
ikawa 33% na kwa bajeti ya 2011/2012 ilikuwa ni 10%. (Chanzo: taarifa ya utafiti wa umasikini na maendeleo ya binadamu ya
mwaka 2011 uk wa 99).
Mheshimiwa
Spika, kushuka huku kwa mchango wa Serikali kwenye fedha za maendeleo ya
miradi ya maji maana yake ni kuwa jukumu la msingi la Serikali kuwahudumia
wananchi wake katika kupata huduma za msingi na haswa maji linaelekea kuishinda
Seriakali kadiri siku zinavyozidi kwenda, jambo hili linapelekea Serikali
kukosa uhalali wa kuendelea kuongoza nchi hii kama inashindwa kutekeleza wajibu
wake wa msingi kama huu ile hali wakijua kuwa maji ni uhai na kama hakuna maji
hakuna maisha.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kutoa sababu za kina na za kimsingi ni kwanini haitilii maanani upatikanaji wa maji na haswa kwa kutenga fedha zetu za ndani za kutosha kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu na kuondoa tatizo la akinamama kuhangaika usiku na mchana kutafuta maji na kuacha kufanya shughuli nyingine za kuongeza uzalishaji.
Aidha tunaitaka serikali kuwasilisha mpango mahususi wa kutatua kero ya
maji haswa vijijini ili tuweze kupunguza umaskini kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika,
takwimu zinaonyesha kuwa hata fedha zinazotolewa na wadau wa maendeleo toka nje
katika kutekeleza program ya maendelelo ya sekta ya maji (WSDP) kwa mwaka 2011
hadi juni takribani asilimia 62 ya fedha zote walizoahidi zilikuwa zimetolewa
kwa ajili ya kutoa usawia wa miradi ya maji nchini kote.
Mheshimiwa Spika,
tafiti mbalimbali zinaonyesha kutokuwepo kwa usawa kwa Serikali katika ugawaji
wa fedha hizo kwa miradi ya maji safi na salama kati ya maeneo ya mijini na
vijijini. Na hii ni kutokana na ukweli kuwa Mgawo kwa maeneo ya vijijini ni
asilimia 36 ya fedha zote na maeneo ya mijini ni asilimia 64 ya fedha
zilizotolewa.
Mheshimiwa Spika,
hii maana yake ni kuwa kila shilingi mia moja zilizotolewa na wafadhili kwa
ajili ya miradi ya maji maeneo ya vijijini yalipata mgawo wa shilingi 36 ile
hali maeneo ya mijini walipewa mgawo wa shilingi 64. Hii ni pamoja na ukweli kwamba
katika nchi yetu watanzania waishio vijijini ni takribani asilimia 77.
Mheshimiwa
Spika, taarifa hizi
kuhusiana na fedha zilizotengwa sio njema na haswa kutokana na ukweli kuwa Wananchi
wengi waishio katika mikoa yenye ukame ni wafugaji na asilimia kubwa ya mifugo
ipo vijijini. Mifugo hiyo inahitaji maji ya kunywa ya wastani wa lita 25 kwa
ng’ombe wa kawaida kwa siku. Ili kuhakikisha kuwa mifugo inapata maji ipasavyo,
Sera ya Maji inaelekeza kujenga mabwawa makubwa na madogo au kuchimba visima
virefu na vifupi katika maeneo ya wafugaji na usanifu wa miradi yote ya maji
vijijini uzingatie mahitaji ya mifugo.
Kambi ya Upinzani
tunahoji kutokana na mgawo wa aina hii ni lini tatizo la maji vijijini
litamalizika? Kuna mkakati gani wa kumaliza tatizo la maji vijijini?
3.2 Matumizi Bora ya Rasilimali
za Maji.
Mheshimiwa
Spika, kwa kuwa sheria
inayolinda raslimali za maji, inayohusu Usimamizi wa
Rasilimali za Maji [The Water Resources Management
Act] Na. 11 ya Mwaka 2009 inahusika na usimamizi wa rasilimali za maji - vyanzo
vya maji juu na chini ya ardhi. Imetungwa na Bunge tar 28/4/2009, imesainiwa na
Mhe. Rais tar 12/5/2009 na kuanza kutumika rasmi tar 1/8/2009 baada ya
kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GN 235 LA 10/7/2009).3
Mheshimiwa
Spika, kwa mujibu wa
kifungu cha 11 cha sheria utunzaji wa Raslimali za maji, matumizi ya Maji Chini ya Ardhi
kinasema kuwa “Endapo katika ardhi
anayoishi mtu kihalali yatapatikana Maji chini ya ardhi, ataruhusiwa kujenga
kisima cha mkono kwa ajili ya kutumia Maji kwa matumizi ya nyumbani bila kuwa
na kibali cha kutumia Maji kwa viwango vya uchimbaji vitakavyotangazwa katika
kanuni zinazoidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya Maji”.
Mheshimiwa
Spika, aidha, kifungu cha 54 (1)
kinasema kuwa “Mtu yeyote anayetarajia kujenga, kuchimba, kuongeza ukubwa au kina cha
kisima katika eneo lililotangazwa kuwa la hifadhi ya maji chini ya ardhi
anapaswa aombe kibali cha maji chini ya ardhi .Maombi ya Kibali cha Maji ya Chini ya Ardhi yatachukuliwa kama ni
maombi ya matumizi ya maji yatakayochukuliwa kutoka kwenye kisima husika na
kwamba Bodi ya Maji ya Bonde ina mamlaka ya kufanya ukaguzi, kifungu. 54(2) na (3)]”.
Mheshimiwa Spika,
ni dhahiri kuwa vipo viwanda na makampuni mbalimbali ambao wameamua kuchimba
visima virefu na vifupi kwa ajili ya kupata maji kwa matumizi ya shughuli
mbalimbali kwenye viwanda na Makampuni husika.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze watanzania ni kwa vipi inathibiti
matumizi ya maji ya chini ya ardhi na kupata mapato stahiki kutoka kwenye viwanda vikubwa kama vile kiwanda cha bia,
kiwanda cha sigara, kiwanda cha kibuku, kiwanda cha cement, kiwanda cha mafuta
ya kupikia, viwanda cha nguo, n.k
Mheshimiwa Spika,
viwanda vyote tajwa hapo juu vimechimba visima vya maji kwa ajili ya matumizi
ya viwanda vyao, na wachimbaji wa visima binafsi wanaongezeka kwa kadri mahitaji
ya maji kwa matumizi ya majumbani na viwandani yanavyozidi kuwa shida, hasa
maeneo ya mijini. (chanzo; Drilling and Dam Construction Agency, 2001).
Mheshimiwa Spika, Kambi
ya Upinzani inaitaka Serikali kufuatilia kwa makini uchimbaji huu wa visima na kuhakikisha
kuwa fedha ambazo wamiliki binafsi wa visima wanatakiwa kulipa walipe na visima
hivyo viwe chini ya uangalizi wa mamlaka husika kwa lengo la kuzia usababishwaji
visima hivyo vya maji safi na salama kutokubadilika na kuwa na maji yasiyokuwa
na ubora kwa mujibu wa sheria na viwango vya kimataifa.
3.3 Upatikanaji wa Maji na
Matumizi yake.
Mheshimiwa Spika,
maji yatokayo ardhini kwa matumizi ya nyumbani kwa maeneo yote ya mijini na
vijijini yanakadiriwa kuwa ni mita za
ujazo 755,000 kwa siku(60% ya matumizi yote), wakati mahitaji ni ni mita za
ujazo milioni 0.8 hadi 3.4 kwa siku.
Mheshimiwa Spika,
umwagiliaji kwenye mashamba ya miwa, maua, matunda, hutumia mita za ujazo 130,000 kwa siku (10%), wakati
matuzi ya viwandani na migodini hutumia takribani mita za ujazo 30,000 kwa
siku(2%). Mifugo na matumizi mengine kama vile ufugaji wa samaki kwenye maeneo
yasiyo na maji hutumia mita za ujazo 350,000 kwa siku (28%). Matumizi ya jumla
kwa maji yatokayo ardhini yanakadiriwa
kuwa ni mita za ujazo milioni 1.265 kwa siku, ambayo ni sawa na asilimia 12 ya
rasilimali yote ya maji ya ardhini ya mita za ujazo milion 11 kwa siku.
Mheshimiwa Spika,
matumizi ya maji ya ardhini kwa uzalishaji viwandani yamejikita zaidi kwa
maeneo ya mijini, hasa Dar es Salaam, ambapo takribani 80% ya viwanda vyote
nchini vipo.
Matumizi haya ya maji ya ardhini kwa
viwanda yanatokana na kushindwa kwa mamlaka inayotoa huduma hiyo kwa mkoa wa
Dar es Salaam kutoa maji ya kutosha kwa ajili ya viwanda.
(chanzo, Taarifa ya
Utafiti wa Dr. Josephat
Kashaigili wa SUA kwa INTERNATIONAL
WATER MANAGEMENT INSTITUTE –IWMI Desemba 2010)
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya
Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kiasi gani cha fedha kinashindwa
kukusanywa kutokana na viwanda kuchimba visima vyao binafsi na hivyo kuacha kutumia
maji ya DAWASCO? Je, matumizi ya maji haya yanayofanywa na viwanda ni endelevu
kwa sekta ya maji?
3.4 Huduma za Maji Mijini na
Vijijini
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka 2011 sekta ya maji ilishuka kwa kiwango cha asilimia 4.0 ikilinganishwa
na asilimia 6.3 mwaka 2010. Hata hivyo, mchango wa shughuli za usambazaji maji
katika pato la taifa ulipungua kutoka asilimia 0.4 mwaka 2010 hadi asilimia 0.3
mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika,
taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa
mwaka 2011 sura ya 18 uk. wa 245 inaonyesha kuwa uzalishaji wa maji mijini kwa
mwaka 2011 ulipungua hadi kufikia mita za ujazo milioni 116.45 kutoka mita za
ujazo milion 116.55 kwa mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa upungufu huu unasababishwa na kuwepo kwa
miundombinu chakavu kwa ajili ya usambazaji wa maji mijini na hasa kutokana na
kukaa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo au ukarabati na hivyo kusababisha
upotevu mwingi wa maji .
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa za serikali ni kuwa Mamlaka za Majisafi na Majitaka
katika miji mikuu ya mikoa hutoa huduma ya maji bila gharama kwa kaya
zisizokuwa na uwezo kwa kuzisaidia lita 160 kwa siku sawa na lita 5,000 kwa
mwezi.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya maji kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru
inaonyesha kuwa hadi sasa jumla ya kaya 1,466 zinapata huduma ya maji bure
kutoka Mamlaka za maji katika miji mbalimbali hapa nchini.
Kambi ya Upinzani,
inataka kupata majibu kuhusiana na masuala yafuatayo:
i.
Je, ni katika miji gani huduma hii
hutolewa na ni utaratibu gani unaotumika katika kuzitambua kaya hizo?
ii.
Je, ni utaratibu gani unaopaswa
kufuatwa na kaya husika ili wananchi waweze kufuatilia na kupata huduma hii?
iii.
Je. ni kwa nini kaya masikini za
vijijini zinasahaulika kutokana na kukosekana kwa utaratibu kama huu na
ikizingatiwa kuwa kiwango cha umaskini ni kikubwa zaidi vijijini kuliko mijini
?.
3.5 Mradi wa maji wa visima
virefu Kimbiji na Mpera.
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka uliopita Serikali ililieleza Bunge kuwa tayari imekwishatoa fidia kwa wananchi kwa maeneo ya
kuchimba visima virefu 20 vya uzalishaji
wa maji wa kutoa mita za ujazo 260,000 kwa siku, kwenye maeneo ya Kimbiji na
Mpera kwa ajili ya kusambaza maji Jiji la Dar Es Salaam.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwa mwaka wa fedha uliopita 2011/2012
mpango huo ulitakiwa kutengewa kiasi cha shilingi. bilion 22.4, na mwaka huu wa
fedha 2012/2013 mradi huo ulitakiwa kutengewa kiasi cha shilingi. bilioni 39.2.
Mheshimiwa Spika, taarifa
zilizopo kwenye randama zinaonyesha kuwa bajeti iliyopangwa kwa mradi huo kwa
mwaka huu wa fedha ni Tshs. Billioni 1 kama fedha za ndani na Tshs. Billioni
29.992 kama fedha za nje. Tofauti ya fedha zilizopangwa katika mpango wa miaka
mitano kwa mradi huo na bajeti iliyotengwa ni Tshs.Billioni 9.208.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaona kuwa tofauti hiyo ni kubwa kiasi kwamba inaweza
kukwamisha utekelezaji wa mradi huu na ni kinyume cha utekelezaji wa mpango wa
maendeleo wa miaka mitano na hivyo wananchi watachelewa kupata huduma ya maji
safi katika Jiji la Dar es Salaam.
Aidha,
fedha nyingi zilizotengwa ni fedha za nje na kwa uzoefu wetu katika miradi
mbalimbali iliyokuwa inategemea fedha kutoka nje imekwama kukamilika kwa muda
mrefu sana.
3.6 Mradi wa Maji Bwawa la
Kidunda
Mheshimiwa Spika, Serikali
haionyeshi kuwa ina nia ya dhati ya kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka
mitano uliopitishwa na Bunge hili kwani Mpango wa maendeleo unaelekeza kuwa kwa
mwaka huu wa fedha zitengwe shilingi billioni 46 kwa ajili ya mradi huu lakini kwa
mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi Bilioni 3.398 fedha za ndani na shilingi
bilion 1.824 fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, Kambi
ya Upinzani tunataka maelezo ya kina kuhusiana na mradi huu na haswa
ikizingatiwa kuwa fedha zinazopaswa kutengwa ni nyingi ila zilizotengwa ni
kidogo sana , na ni dhahiri kuwa serikali haina nia ya dhati ya kuutekeleza
mradi huu.
Na
hii ni kutokana na ukweli kuwa jumla ya mabwawa 568 tu yalijengwa sehemu mbalimbali nchini tangu Uhuru mpaka mwaka
2011.
4.0 MAJI JIJI LA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika,
Mkoa wa Dar es Salam unapata maji kutoka mito na visima kwa matumizi ya
nyumbani, viwanda, bustani, mifugo, usafi na mazingira. Eneo kubwa linalopata
maji linahudumiwa na Kampuni ya DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage
Company). Maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka visima
vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, taasisi na watu binafsi.
Mheshimiwa Spika,
vyanzo vikuu vya maji ni mitambo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini, Mtoni na visima
virefu 1,100 na vifupi 238 vilivyopo katika mkoa. Vyanzo vyote hivi huzalisha
lita milioni 353 kwa siku wakati
Jiji lina mahitaji ya lita milioni 469.3
kwa siku, ambapo ni sawa na upungufu wa lita milioni 116 kwa siku. Aidha kuna maji ambayo yanapotea wakati wa usambazaji
yakiwa njiani kutokana na uchakavu wa mitambo na miundombinu.
Mheshimiwa Spika,
changamoto zinazoathiri utoaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam
ni pamoja na uzalishaji mdogo wa maji ukilinganisha na mahitaji, uhaba wa
vyanzo vya maji, ubadhirifu, uwezo mdogo wa watumia maji kulipia gharama, na
uchakavu wa miundombinu ya usambazaji maji ambayo husababisha upotevu mkubwa
sana wa maji.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na changamoto hizo jiji huwa na ukosefu mkubwa wa maji na kitaifa ni
jiji la mwisho kwa upatikanaji wa maji hapa nchini kwani ni asilimia 55 tu ya
wakazi wa Jiji ambao wanapata maji ikilinganishwa na Majiji na Miji mingine
nchini ambayo wastani wake ni asilimia 75.
Mheshimiwa Spika,
kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na
upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo
ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP)
uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao
wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.
Mheshimiwa Spika, majukumu
ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam yanahusu pia Mamlaka ya
Majisafi na Majitaka (DAWASA) ambayo ni mmiliki, mkodishaji na msimamizi wa
utoaji wa huduma ya majisafi na maji taka katika jiji la Dar es salaam kwenye
wajibu wa kupanga na kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu,
kuiendeleza na kugharamia matengenezo ya dharura na makubwa.
Kambi ya upinzani,
tunaitaka serikali kutoa majibu kuhusiana na mambo yafuatayo:
i.
Kuna mkakati gani wa kuhakikisha
kuwa maji yanapatikana kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na hasa kwenye
maeneo ya ujenzi wa makazi mapya kama vile Kimara, Changanyikeni, Msakuzi,
Mbezi, Kigamboni, Kilungule, Tabata, Kinyerezi na kwingineko?
ii.
Kuna mpango gani wa kuhakikisha kuwa
maji yanayozalishwa hayapotei yakiwa njiani na hasa kutokana na uchakavu wa
miundombinu ya maji?
iii.
Wizara itakamilisha lini miradi ya
maji iliyopangwa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji
Jijini?
iv.
Serikali iwasilishe bungeni Mpango
Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la
Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa,
kutengewa bajeti ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na
kusimamiwa.
v.
Mpango wa dharura wa kupunguza kero
ya maji ulianza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA
kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika
Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kuwa Oktoba 2012 katika maeneo
ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
vi.
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) afanye ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa
Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar
es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and
Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit)
uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
vii.
EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance
audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na
serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali
lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, EWURA
iharakishe kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa
upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.
viii.
Serikali ieleze imefikia hatua gani
katika kutekeleza mapendekezo ya taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi
wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the
management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012.
Mheshimiwa Spika,
katika Jiji la Dar es Salaam miaka ya hivi karibuni kumejitokeza na kushamiri
tabia ya wananchi kuharibu na kuiba miundombinu ya miradi ya maji na kuiuza
kama chuma chakavu. Vifaa vinavyoibwa sana ni mifuniko ya mashimo ya maji taka,
mabomba ya maji, mita za maji na vifaa vinginevyo.
Kambi ya Upinzani,
inaamini kuwa serikali inafahamu kunakouzwa vyuma hivi chakavu kwa kuwa ndio
imetoa leseni kwa biashara hii. Tunaitaka kuwachukulia hatua wale wote ambao
wanafanya biashara hii ya kuhujumu miundombinu yetu ya maji.
Mheshimiwa Spika,
huduma ya uondoaji wa majitaka jijjini Dar es Salaam si ya kuridhisha kutokana
na uwekezaji mdogo unaofanywa na Serikali katika eneo hili. Hadi sasa ni
asilimia 18 tu ya wakazi mijini ndio wameunganishwa kwenye huduma hii. Jambo
hili limewafanya wakazi wengi wa mijini kutumia vyoo vya mashimo, makaro
(septic tanks) na vyoo vya shimo ambavyo huchangia uchafuzi wa maji yaliyoko
chini ya ardhi.
Kambi ya Upinzani,
tunaitaka serikali kuhakikisha kuwa inawekeza vya kutosha ili kuweza
kukabiliana na hali hii na hasa ikizingatiwa kuwa kama hatua zitachelewa
kuchukuliwa uchafuzi huu utaendelea kuathiri wananchi kiafya.
4.1. Mtandao wa Maji Safi na
Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam:
Mheshimiwa Spika,
uchakavu wa miundombinu kutokana na mabomba kutokarabatiwa ipasavyo pamoja na
uharibifu katika mitandao ya maji wa kujiunganishia kinyemela na kiholela
umesababisha ongezeko kubwa la upotevu wa maji mpaka kufikia kati ya asilimia
40 hadi 45.
Mheshimiwa Spika,
hali hii imesababisha ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa kipato cha
chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo wanaonunua maji kwa
madumu hununua bei ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata huduma
ya maji ya bomba.
Mheshimiwa Spika,
mtandao wa uondoaji wa maji taka ni chini ya asilimia 10 tu ya makazi ndiyo
yaliyounganishwa na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo
yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam mitandao ya
maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa licha ya ongezeko kubwa la watu.
Kampuni ya Majisafi na Majitaka (DAWASCO) ambaye ni mwendeshaji mwenye wajibu
wa kuendesha shughuli za kutoa huduma ya maji, kutoa ankara kwa wateja,
kukusanya maduhuli, kutekeleza matengenezo makubwa yanayogharamiwa na DAWASA na
kutekeleza uunganishaji wa maji kwa wateja wapya kwa kutumia mfuko wa maji.
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iongeze mtandao wa maji safi na maji taka
hasa kwa maeneo mapya kama tulivyoyataja hapo juu.
5.0. PROGRAMU YA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI
Mheshimiwa Spika, taarifa
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu miradi inayochangiwa
na nchi wahisani iliyotolewa Juni 2011, sura ya 3 Uk. wa 13-15 inaonyesha fedha
zilizotolewa na Serikali pamoja na
nchi washirika wa Maendeleo zilikuwa jumla ya shilingi 226,913,350,139
kwa ajili ya miradi ya maji. Aidha katika Programu hiyo ilikuwa na bakaa ya shilingi
68,332,741,760 na hivyo kufanya mwaka huo wa fedha kuwa na Jumla ya shilingi 295,246,091,899 na Hadi kufikia mwisho
wa mwaka wa fedha kulikuwa na fedha zisizotumika kiasi cha shilingi 72,582,156,680.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia 30Juni, 2011 vitabu vya
Halmashauri mbalimbali vilikuwa vinaonyesha kuwa kiasi cha shilingi 32,240,623,989.47 zilikuwa kama bakaa
ambayo ilikuwa ni sawa na 58% ya fedha za miradi ya maji, Kwa maoni ya Mkaguzi
kiasi hiki kikubwa ni kutokana na kushindwa kwa Halimashauri kutekeleza miradi
ya maji kwa mujibu wa mipango.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze ni kwanini fedha hizi zinashindwa
kutumika wakati tatizo la maji ni kubwa mno kwa wananchi. Mfano ni halimashauri
ya Wilaya ya Mbozi ambayo miaka yote toka enzi za (Mhe Simpasa, Luka Siyame,na sasa
Mhe.Godfrey Zambi na mhe.David Silinde) imekuwa na tatizo kubwa la
maji, lakini takwimu zinaonyesha kuwa Halimashauri ilishindwa kutekeleza mpango
wake wa miradi ya maji na mwisho wa mwaka wa fedha ilibakiza fedha za miradi ya
maji kiasi cha shilingi milioni 865.7. Hizi ni fedha nyingi kwa wananchi ambao
wanatatizo la maji.
Mheshimiwa Spika,
Tatizo kama hili lilizikumba Halimashauri za Wilaya Karagwe, Kondoa, Musoma,
Mbeya Vijijini, Ngorongoro, Iringa, Meatu, Temeke na Ilala ambazo ziliacha
kiasi kikubwa sana cha fedha bila kutumika. Aidha Halimashauri ya Wilaya ya
Iramba ilishindwa kutekeleza miradi ya maji kwa kipindi hicho na kubakiza fedha
kiasi cha shilingi 894,376,237.15
Mheshimiwa Spika, kutokana
na taarifa hizi ni dhahiri kuwa miradi mingi ya Maji imekuwa ikishindwa
kutekelezwa na fedha nyingi kubakia bila kutumika ile hali wananchi wetu
wakiteseka kutafuta huduma za maji.
(chanzo: taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, ukaguzi wa
miradi inayochangiwa na wafadhili-(donor funded projects) ya 30 Juni, 2011)
Kambi ya upinzani,
tunataka maelezo ya kina kuhusiana na fedha hizi kutokutumika ni sababu gani
zilipelekea hali hiyo kujitokeza? Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa
miradi hii inatekelezwa?
6.0 MIGOGORO YA MAJI
6.1 Mgogoro wa wananchi na Mamlaka za Maji Mbalizi.
Mheshimiwa Spika,
kumekuwa na taarifa mbalimbali za migogoro baina ya wananchi na wakala
mbalimbali wa usambazaji maji kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini , na hali
hiyo imetokana na ama wananchi kutokuhusishwa kwenye kupanga bei mpya za maji
au huduma kuwa chini ya kiwango ile hali wananchi wakiwa wanapaswa kulipia
huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika,
mnamo tarehe 29/10/2011, Wananchi wa Mbalizi walifunga Ofisi za Mamlaka ya
Majisafi Mbalizi kutokana na huduma
wanayopata ni duni, vilevile mradi wa maji ni wao na hivyo walipaswa kuuendesha
mradi wao wenyewe, bei ya maji ya
shilingi 10,000 kwa mwezi ni kubwa na walitaka ipungue hadi shilingi 7,000 kwa
mwezi na Meneja wa Mamlaka pamoja na
Mafundi hawatakiwi kuonekana Ofisini.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na madai ya wananchi hawa kuwa sahihi Mkuu wa Wilaya aliitisha mkutano
wa hadhara mnamo tarehe 09.11.2011 na kuzungumza na wananchi hao lakini
walimueleza wazi kuwa hawatakuwa tayari kufungua ofisi kama madai yao ya msingi
hayatapata ufumbuzi, na hadi anaondoka kwenye mkutano huo walikuwa
hawajakubaliana .
Mheshimiwa Spika,
wananchi walikubali kufungua ofisi hizo mnamo tarehe 17.11.2011 na hii ni baada
ya madai yao kukubaliwa ikiwemo Meneja
wa Mamlaka aliyekuwepo kuhamishiwa Kituo chake cha awali cha kazi Ofisi ya
Mkurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya
mafundi waliokuwa wanalalamikiwa kusimamishwa kazi na bodi mpya ya mamlaka
kuundwa ikiwa na wajumbe saba.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na mtafaruku huu uliipelekea Mamlaka ya maji Mbeya kuzuia huduma ya
maji kwa wananchi wa Mbalizi na hivyo kuwafanya wananchi kukosa huduma ya maji
kwa muda mrefu tangu mwezi Oktoba 2011 hadi mwezi Juni mwaka huu ilikuwa
haijarejeshwa.
Aidha
tunataka kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya meneja na mafundi wote ambao
walikuwa wanalalamikiwa na wananchi , na ni lini huduma hii ya maji itarejeshwa
katika mji wa Mbalizi?
6.2. Mgogoro baina ya wananchi na Mamlaka ya Maji
Manispaa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, mkoa wa Kigoma unatoa huduma ya maji kwa kutumia
teknolojia mbalimbali, kwa mfano kusukuma maji kwa mashine, chemichemi, skimu
za maji ya mtiririko, visima vifupi na virefu vyenye pampu za mkono, pamoja na uvunaji
maji ya mvua.
Mheshimiwa Spika, ukosekanaji wa mita hususani kwa wakazi wa manispaa ya Kigoma ujiji, mamlaka ya maji mkoani Kigoma imeshindwa kutekeleza kabisa maagizo ya ewura ya kutaka wananchi wapewe mita ili waweze kujua wanatumia maji kiasi gani na kulipa kulingana na kiasi cha maji wanayotumia.
Mheshimiwa Spika, Waziri ameshindwa kujibu barua aliyoandikiwa na manispaa baada ya kumteua Diwani mmoja ili awe mjumbe Wa bodi ya maji na muwakilishi Wa wananchi katika bodi hiyo lakini Mpaka dakika hii waziri hajajibu kwahiyo idara ya maji inapanga itakavyo gharama za maji ilianza na shilingi 5,200 ikaenda shilingi 17,500 hadi shilingi 19,500 na sasa wanataka kupandisha Ankara hadi shilingi 23,000 kwa mwezi, huku ni kuwakomoa watu wa kigoma ,huu ni udhalilishaji na dharau kwa wananchi na wakazi wa mkoa wa Kigoma, Mpaka sasa hatua zilizochukuliwa ni kwamba wenyeviti wa mitaa 68 wamechanga pesa kwa ajili ya kuishtaki body ya maji ya mkoa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina juu ya utaratibu wa kupandisha
bei za maji bila kuwashirikisha wadau ambao ni wananchi, kwani huku ni kwenda
kinyume na sera ya maji.
6.3. Mgogoro wa Maji-Goba
Mheshimiwa Spika, migogoro
katika miradi ya maji ya wananchi haipo tu maeneo ya vijijini bali pia katika
maeneo ya mijini ikiwemo katika Jiji la Dar es salaam. Mfano wa migogoro hiyo
ni wa mradi wa wananchi wanaotumia maji katika kata ya Goba uliodumu kwa zaidi
ya miaka mitano, na kusababisha wananchi kukosa huduma ya maji.
Vyanzo
vya matatizo hayo ni pamoja na uendeshaji mbovu wa mradi wa maji chini ya
kamati za maji unaosababisha kuibuka kwa tuhuma za mara kwa mara za ufisadi,
malimbikizo ya madeni na kuharibika kwa miundombinu. Aidha, chanzo kingine
kikubwa ni uwezo mdogo wa miradi hiyo ya maji ukilinganisha na ongezeko la
idadi ya watu katika mitaa ya kata hiyo ambayo awali ilikuwa vijiji.
Mheshimiwa Spika, ili
kushughulikia kasoro hizo tarehe 24 Oktoba 2011 Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kinondoni aliandikiwa barua ili achukue
hatua za dharura kutatua mgogoro huo na kuwezesha wananchi kupata huduma ya
maji; taarifa ya suala hilo ilifikishwa Wizara ya Maji, hata hivyo mgogoro huo
umedumu mpaka hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya
Maji kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka kufuatilia
kwa dharura kuhakikisha maji yanarejeshwa Goba. Hatua hii iende sambamba na
kupanua wigo wa maji Goba kwa kutekeleza kwa haraka upatikanaji wa maji kutoka
pia mradi wa maji toka Madale Kisauke. Wizara ya Maji ishirikiane na Manispaa
kuhakikisha matatizo yaliyopo yanatatuliwa kwenye miradi ya maji inayoendeshwa
na manispaa pamoja na kamati za wananchi au vyama vya watumia maji katika
maeneo mbalimbali.
7.0
UCHAFUZI
WA VYANZO VYA MAJI
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina vyanzo vikuu vya maji ambavyo ni mito mikubwa, maziwa, chemichemi
na maji chini ya ardhi. Maji ya vyanzo hivyo ndiyo yatumikayo majumbani,
viwandani, mashambani na kwa ajili ya mifugo. Maji yanayotumika toka ziwa
Viktoria kwa kiasi kikubwa yanachafuka kutokana na viwanda kama vile vya
kusindika kahawa, pamba, mafuta ya kula na viwanda vya sabuni na manukato bila
kusahau viwanda vya samaki ambapo uchafu toka viwanda hivyo huelekezwa ziwani,
au uchafu huelekezwa kwenye mito ambayo inaingiza maji yake ziwani.
Mheshimiwa
Spika, matumizi ya madawa
ya kuchenjulia dhahabu yanayotumiwa na wachimbaji wadogo kwenye mito ambayo
wakati wa masika maji hutiririka hadi ziwa Viktoria na mahali pengine kwenye
mito mikubwa ambayo ni vyanzo vya maji ambayo maji yake yanatumika kwa matumizi
ya majumbani.
Mheshimiwa
Spika, kilimo cha matumizi
ya mbolea na madawa ya viwandani kinachoendeshwa katika maeneo yaliyo karibu na
vyanzo vikuu vya maji ni mojawapo ya vyanzo vya uchafuzi mkubwa wa vyanzo vyetu
muhimu vya maji.
Mheshimiwa
Spika, kutokana na uvamizi
wa vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira vipo vyanzo vya maji ambavyo
vilikauka, kupungua maji na vingine kuchafuka na kutokufaa kama vile Ziwa
Chala, Ziwa Jipe, mto Umba na ziwa Manyara.
Mheshimiwa
Spika, Kambi ya Upinzani
inaitaka Serikali katika hili la matumizi ya mbolea za viwandani, katika
uchafuzi wa vyanzo vya maji, suluhu ya hilo ni kuingia katika matumizi ya
mbolea za asili kama vile mboji au
mbolea za na marejea na mimie kama hiyo
hasa kwa wakulima ambao wanafanya shughuli zao karibu na vyanzo vya maji.
Aidha, tunaitaka serikali kuweka mkakati mahususi
wa kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinalindwa kikamilifu dhidi ya uchafuzi
wowote na kama ikitokea viwanda vinahusika basi sheria ya mazingira itumike ili
wahusika wawajibishwe.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kutoa maoni hayo kwa niaba
Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.
……………………………………………
Sabreena Hamza Sungura (Mb)
k.n.y Msemaji Mkuu wa Kambi ya
Upinzani-Wizara ya Maji.
09.07.2012
No comments:
Post a Comment