Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linampongeza Amani Ibrahim Makungu kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika
uchaguzi uliofanyika juzi (Juni 30 mwaka huu) kwenye hoteli ya Bwawani,
mjini Zanzibar.
Ushindi
wa asilimia 94 alioupata Makungu ambaye hakuwa na mpinzani katika
uchaguzi huo mdogo unaonesha imani ambayo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
ZFA wanayo kwake katika kukiongoza chama hicho.
Ni
matarajio ya TFF kuwa ushindi huo utatafsiriwa kwa vitendo na wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa ZFA na wadau wa mpira wa miguu Zanzibar kwa kumpa
Makungu ushirikiano wa asilimia 100 ili kuhakikisha Kamati yake ya
utendaji inafanya kile kinachotarajiwa na wengi.
Makungu
si mgeni katika mpira wa miguu, na mchango aliotoa kwa mchezo huo
visiwani kabla ya kuwania nafasi hiyo unatambuliwa na kila
anayefuatilia maendeleo ya mpira wa miguu katika Zanzibar.
TFF
tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ZFA chini ya Makungu kama
ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Ali Ferej Tamim ili kuhakikisha ustawi
wa mpira wa miguu visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
MISRI YAAHIRISHA MECHI DHIDI YA NGORONGORO HEROES
Mechi
mbili za kirafiki kati ya timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye
umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na Misri zilizokuwa zichezwe
mwezi huu zimefutwa.
Chama
cha Mpira wa Miguu Misri (EFA) kimetuma taarifa jana (Julai 1 mwaka
huu) kikiomba kusogezwa mbele hadi mwishoni mwa Agosti baada ya
kushindwa kupata usafiri wa ndege kuwahi tarehe ambazo ilikubaliana na
TFF kwa ajili ya mechi hizo.
Ngorongoro
Heroes ambayo tayari iko kambini ilikuwa icheze mechi hizo Julai 3 na 5
mwaka huu jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya
kuikabili Nigeria katika mechi ya michuano ya Afrika, Julai 29 mwaka
huu.
Mechi
nyingine za kirafiki kwa Ngorongoro Heroes inayofundishwa na Jakob
Michelsen zitachezwa Julai 14 na 16 mwaka huu dhidi ya Rwanda.
RUVUMA YAIFANYIA MAUAJI LINDI 7-2
Timu
ya Ruvuma imethibitisha kuwa mwiba mkali katika michuano ya Copa
Coca-Cola mwaka huu baada ya leo asubuhi (Julai 2 mwaka huu) kuishushia
Lindi kipigo cha mabao 7-2.
Hadi
mapumziko kwenye mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu
mkoani Pwani, washindi ambao kwa matokeo hayo wamejiweka katika nafasi
nzuri ya kucheza 16 bora walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
Waliotikisa
nyavu ni Anthony Christian dakika ya 23 na 50, Edward Songo dakika ya
27, 75 na 86 na Sunday Leonard dakika ya 32 na 60. Mabao ya Lindi
yalifungwa na Salum Mnyamwile dakika ya 18 kwa njia ya penalti na
lingine dakika ya 48 kupitia kwa Mwarami Maundu.
Nayo
Tanga imepata ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya
kuifunga Manyara mabao 2-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa Uwanja
wa Tamco mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na Mbwana Musa
dakika ya 47 na Issa Mwanga dakika ya 60.
Katika
mechi tatu zilizotangulia Tanga ilitoka sare ya mabao 3-3 na Morogoro,
ikapata sare nyingine ya 1-1 dhidi ya Mwanza, na baadaye 1-1 na Tanga.
Kagera
imeendelea kujitutumua katika michuano hiyo baada ya kupata ushindi
wake wa pili katika kundi D kwa kuilaza Kusini Unguja bao 1-0 katika
mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe jijini Dar
es Salaam.
Bao
lake lilifungwa dakika ya 76 na Novati Sebastian. Mechi iliyopita
Kagera iliifunga Tabora mabao 2-0 baada ya kuteleza katika mechi mbili
za kwanza kwa kufungwa na Kilimanjaro na Singida.
Mechi
nyingine ilichezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ambapo
Kinondoni iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mara.
UONGOZI TWIGA STARS WATOA TAMKO
Uongozi
wa Twiga Stars umekana kuwepo vitendo vyovyote vya kinyume na maadili
kwa wachezaji wa timu hiyo ambayo hivi karibuni ilitolewa kwenye mechi
za mchujo za michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC).
Wakizungumza
na waandishi wa habari leo (Julai 2 mwaka huu), Meneja wa Twiga Stars,
Furaha Francis na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Boniface
Mkwasa wamesema hakuna vitendo vya aina hiyo.
Mkwasa
amesema alikaririwa vibaya kuhusu suala hilo wakati akiwa kwenye
mahojiano na kituo cha televisheni cha Star Tv kutokana na swali
alilokuwa ameulizwa kuhusiana na vitendo hivyo.
“Ukifuatilia
mahojiano yangu na Star Tv mimi sikusema kuwa kuna vitendo hivyo.
Tatizo nadhani lilianzia kwa magazeti yaliyonukuu kupitia Star Tv, na
wala kujiuzulu kwangu hakukuhusiana na hilo, nimewajibika kama kocha
kutokana na kutolewa na Ethiopia,” amesema Mkwasa.
Naye
Furaha Francis amesisitiza kuwa hakuna vitu vya aina hiyo katika timu
hiyo, na kama kuna mtu ana ushahidi na hilo ni bora akauonesha badala
ya kuzungumzia uvumi kuliko ukweli.
“Ukweli
ni kwamba si sisi na wachezaji tu ambao hatukufurahishwa kutolewa na
Ethiopia, wapo Watanzania wengi ambao hawakufurahishwa na matokeo yale.
Twiga Stars si timu ya kudumu, haikai na wachezaji kwa muda wote, kila
mchezaji ana timu yake.
“Madai
yanayoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu vitendo hivyo
yametuchafua sana. Tunaomba kama kuna mtu ana ushahidi na hilo atueleze
kuliko kuendelea kutuchafua,” amesema.
No comments:
Post a Comment