SIMBA, WAGANDA SASA KUCHEZA JUMAPILI
Mechi
ya Simba na URA ya Uganda kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati
(Kombe la Kagame) iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa
itafanyika Jumapili (Julai 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Baraza
la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefanya
mabadiliko hayo kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa
ichezwe kwenye uwanja huo kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Kutokana
na mabadiliko hayo, mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10
kamili jioni, mechi nyingine Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti
itachezwa saa 8 kamili mchana Uwanja wa Chamazi.
Pia
siku hiyo hiyo ya Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi
nyingine itakayoanza saa 10 kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha
timu za Azam ya Tanzania Bara na Mafunzo kutoka Zanzibar.
Mechi
za ufunguzi wa mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi
ya kwanza saa 8 mchana itakuwa kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya
Sudan Kusini wakati saa 10 kamili jioni Yanga itaoneshana kazi na
Atletico ya Burundi.
VIINGILIO MICHUANO YA KAGAME 5,000/- KWA 2,000/-
Viingilio
vya chini katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza Jumamosi
(Julai 14 mwaka huu) vitakuwa sh. 5,000 kwa mechi za Yanga na Simba, na
sh. 2,000 kwa mechi ambazo hazihusishi timu hizo. Yanga ni bingwa
mtetezi wakati Simba ni makamu bingwa mtetezi.
Kwa
upande wa mechi zinazohusisha Yanga na Simba viingilio vitakuwa kama
ifuatavyo; viti vya bluu na kijani sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa
sh. 7,000, viti vya VIP C sh. 10,000, viti vya VIP B sh. 15,000 na viti
vya VIP A ni sh. 20,000.
Siku
ambazo Simba na Yanga hazichezi, viingilio vitakuwa sh. 2,000 kwa viti
vya rangi ya chungwa, bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya VIP C, sh.
10,000 kwa viti vya VIP B na sh. 15,000 kwa viti vya VIP A. Mshabiki
akikata tiketi moja anaona mechi zote mbili; mechi ya saa 8 na ile ya
saa 10.
Timu
za El Salam Wau ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zimewasili Dar
es Salaam jana usiku (Julai 11 mwaka huu) tayari kwa mashindano hayo
wakati nyingine zote zilizobaki kutoka nje zinawasili leo katika muda
tofauti.
TEMEKE, MWANZA ZAVAANA NUSU FAINALI COPA 2012
Temeke
na Mwanza zinapambana kesho (Julai 13 mwaka huu) katika nusu fainali ya
kwanza ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 itakayochezwa saa 2.30
asubuhi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali ya pili itaanza saa 9.30 mchana kwenye uwanja huo huo ikizikutanisha timu za Morogoro na Tanga.
Mechi
ya kutafuta mshindi wa tatu na fainali ya michuano hiyo zitachezwa
Jumapili (Julai 15 mwaka huu). Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 5
asubuhi na kufuatiwa na fainali ambayo itafanyika kuanzia saa 9 kamili
alasiri.
Mwanza
ilipata tiketi ya nusu fainali kwa kuifunga Kinondoni 3-1 huku Temeke
ikitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Mjini Magharibi.
Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mara ndiyo ulioipa Morogoro tiketi ya
nusu fainali wakati Tanga yenyewe iliilaza Dodoma bao 1-0.
TWIGA STARS YASAIDIWA VIFAA VYA MIL 1.3/-
Kampuni
ya bima ya Maxinsure imetoa vifaa vya mazoezi kwa timu ya Taifa ya
mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) vyenye thamani ya sh. milioni
1.3.
Vifaa
hivyo ambavyo ni jezi, bukta na soksi 20, vizibao (bibs) 20 na mipira
miwili vimekabidhiwa leo (Julai 12 mwaka huu) kwa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) na Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Amisa Juma.
Akikabidhi
vifaa hivyo, Amisa amesema wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya mchango
wao kwa jamii lakini vilevile wameamua kuiunga mkono timu hiyo ambayo
wanajua haina mdhamini kutokana na vipaji na uwezo ambao umekuwa
ukioneshwa na wachezaji wake.
Pia
amezitaka kampuni, taasisi, watu binafsi na Serikali kuiunga mkono timu
hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali inayotarajia
kushiriki.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment