Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameshtushwa na kuhuzunishwa na kifo cha aliyekuwa mbunge mkongwe na Waziri wa
miaka mingi katika Serikali za Awamu mbali mbali za uongozi wa Tanzania,
Mheshimiwa Jackson Makweta ambacho kimetokea jioni ya jana, Jumamosi, Novemba
17, 2012, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Katika
salamu zake za rambirambi kwa familia ya Mzee Jackson Makwete, Rais Kikwete
amemwelezea Mzee huyo kama mtumishi wa umma aliyejali sana ustawi wa jamii
yake, mwanasiasa mkweli na mwadilifu, mbunge aliyeleta matumaini kwa
aliowawakilisha na waziri aliyetoa mchango mkubwa katika Serikali
alizozitumikia.
Rais
Kikwete ameiambia familia hiyo ya Mzee Makweta: “Nimepokea kwa mshtuko na huzuni
kubwa taarifa ya kifo cha Mzee Jackson Makweta ambacho nimejulishwa kuwa
kimetokea jioni ya leo. Kwa hakika Tanzania imempoteza mtumishi wa umma wa
mfano na aliyejali sana ustawi wa jamii yake na mwanasiasa mkweli na
mwadilifu.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Tutaendelea kumkumbuka Mzee Makweta kama mbunge ambaye alileta
matumaini na kuongoza jitihada za wananchi wa Njombe Kaskazini kujiletea
maendeleo na Waziri ambaye alitoa mchango mkubwa katika Serikali za Awamu mbali
mbali za uongozi wa nchi yetu. Alikuwa kisima cha busara na mzoefu wa uongozi
na ameondoka wakati bado tunahitaji sana uongozi na busara zake.”
“Nawatumieni
nyinyi wanafamilia salamu zangu za rambirambi kwa kuondokewa na kiongozi na mhimili
wa familia. Naelewa machungu yenu katika kipindi hiki. Naungana nanyi katika
msiba mkubwa na majonzi mengi. Namwomba Mwenyeji Mungu, Mwingi wa Rehema, awape
subira na uvumilivu ili muweze kuvuka kipindi hiki kigumu. Aidha, naungana
nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi pema roho ya Marehemu
Jackson Makwete. Amina.”
Imetolewa
na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
No comments:
Post a Comment