Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kesho, Jumatatu, Aprili
15, 2013, anaanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika Ufalme wa
Uholanzi kwa mwaliko wa HM Malkia Beatrix wa nchi hiyo.
Rais Kikwete akiambatana
na Mama Salma Kikwete na ujumbe wake ameondoka nchini mchana wa leo, Jumapili,
Aprili 14, kwenda Uholanzi tayari kwa ziara hiyo ambako pia ataandamana na
Mawaziri wanne wa Serikali.
Mawaziri hao ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe,
Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dr. Abdallah Kigoda, Waziri wa Nishati
na Madini Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Maji, Ardhi, Nishati
na Maendeleo ya Makazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Ramadhan
Shaaban.
Katika siku ya kwanza
ya ziara yake kesho, Rais Kikwete atafanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati
ya Tanzania na Uholanzi kwenye Makazi Rasmi ya Waziri Mkuu. Mazungumzo hayo
rasmi yatakuwa kati ya Rais Kikwete na ujumbe wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Uholanzi Mheshimiwa Frans Timmermans.
Baada ya mazungumzo
hayo rasmi, Rais Kikwete atakutana kwa mazungumzo na HRH Princes Maxima, Mke wa
Mfalme Mtarajiwa wa Uholanzi, Prince of Orange Willem Alexander ambaye
anatarajiwa kurithi kiti cha Ufalme kutoka kwa Mama yake, Malkia Beatrix,
mwishoni mwa mwezi huu, Aprili 30, 2013.
Baadaye, Rais Kikwete
na ujumbe wake atakutana na kufanya mazungumzo na Her Majesty Malkia Beatrix wa
nchi hiyo ambaye anastaafu rasmi Aprili 30 mwaka huu kumwachia nafasi hiyo
mwanawe, Prince Willem Alexander.
Miongoni mwa shughuli
zake nyingine za kesho, Rais Kikwete atakutana na uongozi wa Kampuni ya Rijk
Zwaan Netherlands Limited, atakula chakula cha mchana cha kazi na wawakilishi
wa Jumuia ya Biashara ya Uholanzi na baadaye atakutana kwa mazungumzo na
viongozi wa Chama cha Wenye Viwanda na waajiri wa nchi hiyo.
Keshokutwa, Jumanne,
Rais Kikwete atatembelea Bandari ya Rotterdam, moja ya bandari maarufu zaidi
duniani, atakutana kwa mazungumzo ya faragha kati yake na Waziri Mkuu wa nchi
hiyo, Mheshimiwa Mark Rutte ambaye pia watakula naye chakula cha mchana.
Mchana, Rais Kikwete
atatembelea Kampuni maarufu ya mafuta duniani ya Shell na kukutana na jumuia ya
Watanzania wanaoishi Uholenzi.
Rais Kikwete na
ujumbe wake anatarajiwa kurejea nchini Jumatano, Aprili 17, 2013.
No comments:
Post a Comment