MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Thursday, April 11, 2013

TAARIFA YA WAZIRI WA UCHUKUZI KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ONGEZEKO LA NAULI LILILOTANGAZWA NA MAMLAKA YA UDHIBITI, USAFIRI WA NCHI KAVU NA MAJINI (SUMATRA)






Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Kuhusu kulidhia upandishwaji wa nauli uliotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)  hivi karibuni. Katikati ni Mwenyekiti, Ayoub Omar na Kulia ni Oscar KikoyoKatibu Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).


Kwa kipindi cha wiki mbili hivi, kumekuwa na malalamiko mengi kupitia vyombo mbalimbali vya habari (magazeti, redio, luninga na mitandao ya kijamii) kuhusu viwango vipya vya nauli vilivyotangazwa na SUMATRA tarehe 28 Machi, 2013 ambavyo vinatarajiwa kuanza kutumika kesho Ijumaa tarehe 12 Aprili, 2013. Viwango vipya vya nauli vinavyolalamikiwa vinahusu mabasi yatoayo huduma mijini, maarufu kwa jina la daladala; mabasi  ya masafa marefu; na usafiri wa treni kwa reli ya kati. Vilevile SUMATRA ilitangaza tozo mpya za kuhudumia Meli bandarini, tozo ambazo haziwahusu kabisa abiria, kinyume na taarifa za kupotosha tunazozisikia.

Ndugu Wanahabari,

Serikali imeyapa uzito mkubwa malalamiko hayo na imechukua hatua ya kuvihoji vyombo vilivyohusika katika mchakato wa kuridhia viwango hivyo vilivyotangazwa vya nauli. Lengo la Serikali ni kujua msingi wa mabadiliko hayo na kama taratibu za kisheria zilifuatwa katika kufikia uamuzi huo, kwani sheria inasisitiza ushirikishwaji wa wadau na uwepo wa sababu za msingi kuruhusu mabadiliko ya nauli.

Tumevihoji vyombo vikuu viwili ambavyo vipo kisheria katika mchakato wa aina hii: SUMATRA na  Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na SUMATRA yaani SUMATRA Consumer Consultative Council.

Katika mahojiano hayo na uchambuzi wa taarifa za wadau mbalimbali, Serikali imebaini yafuatayo:

Kwanza, maombi ya kupandisha viwango vya nauli za daladala Jijini Dar es Salaam, yaliwasilishwa na watoa huduma wa daladala tarehe 12 Aprili, mwaka uliopita wa 2012 . Maombi yalikuwa ni kupandisha nauli kutoka shilingi 300 hadi shilingi 872 kwa njia yenye urefu wa kilomita 15 sawa na shilingi 58.13 kwa abiria kwa kilomita. Pendekezo hilo lilikuwa sawa na  ongezeko la shilingi 572 kwa nauli za sasa  (au ongezeko la asilimia 149).

Sababu zilizotolewa na wamiliki wa daladala ni kuwa nauli ya sasa ya sh. 300 kwa njia yenye urefu wa kilomita 15, imepitwa na wakati kwani tangu ianze kutumika mwezi Machi, 2011 (yaani miaka 2 iliyopita), gharama za ununuzi wa vipuri, mataili, mafuta, vilainishi n.k. na uendeshaji kwa ujumla zilikuwa zimepanda sana kuhalalisha nauli ya sh. 872 badala ya sh. 300 kwa abiria moja.

Hakuna anayeweza kupinga kuwa gharama za uendeshaji zimepanda sana: kwa mfano mwanzoni mwa 2011 lita ya dizeli ilikuwa inauzwa kwa sh.1,783.85 na sasa ni sh.2,092.37; taili la viwango aina ya Good Year lilikuwa linauzwa sh.400,000 na sasa ni sh.752,000.

Lakini, Ndugu Wanahabari, ni busara vilevile wamiliki wa daladala kutambua kuwa gharama hazijapanda kwao tu na magari yao bali vilevile hata kwa wananchi katika maisha yao ya kila siku; wananchi ambao kipato chao hakijapanda kuendana na mfumuko wa bei.

Hivyo Serikali imeliona pendekezo la wamiliki wa daladala la sh. 872 badala ya sh. 300 kuwa kubwa mno. Serikali imeona haja ya kugawana kidogo hayo maumivu ya kupanda kwa gharama kwa kuridhia nyongeza ndogo ya nauli kwa sh. 100 na kuwa sh. 400 badala ya 300. Nauli ya sh. 400 ndiyo tunayoitumia kwa treni kutoka stesheni hadi Ubungo Maziwa na wananchi wanalipa nauli ya sh.500 kutoka Mwakanga mpaka stesheni ya TAZARA, bila malalamiko. Kwa upande wa wanafunzi, ongezeko ni la sh. 50 kuwa sh. 200 badala ya sh. 150 kwa umbali wowote ule.

Tumechunguza kama vyombo husika vilifuata sheria, yaani Kanuni za Tozo na Gharama za  SUMATRA, 2009. Taratibu hizo ni pamoja na kuitisha mikutano ya wadau ili kupokea maoni yao kuhusu maombi yaliyowasilishwa na watoa huduma. Tumejiridhisha kama Serikali kuwa wadau mbalimbali walihusishwa kupitia mikutano ya wazi wakiwemo Baraza la Watumiaji Huduma zinazodhibitiwa na SUMATRA, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, vyama vya watoa huduma, vyama vya madereva, vyama vya kutetea abiria, Waandishi wa Habari, wananchi kwa ujumla na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali. Wito wa kuhudhuria mikutano hiyo ulitolewa kupitia vyombo vya habari: magazeti, redio na luninga.

Kulikuwa na mvutano mkubwa sana, wamiliki wakitaka nauli waliyopendekeza iridhiwe, na wawakilishi wa abiria wakitaka nauli ibaki ileile ya 2011. Ndipo maamuzi ya nyongeza ndogo ya sh. 100 kwa abiria wa kawaida na sh. 50 kwa wanafunzi ikafikiwa. Wawakilishi wote wa abiria waliambiwa kuwa kama ongezeko hilo dogo hawaridhiki nalo, sheria inawaruhusu kukata rufani kwenye Baraza la Ushindani, Fair Competition Tribunal. Hakuna aliyefanya hivyo na kama kawaida ya Watanzania, tumeishia kulalama na kunung'unika nje ya taratibu.

Mimi kwa upande wangu, kama Waziri wa Uchukuzi, sina tatizo na ongezeko hili dogo la nauli za daladala, tatizo langu ni tabia yetu Watanzania tulio wengi kukacha vikao halali vinavyojadili mambo yanayotuhusu na kusubiri kuja kulalamika baadaye.

Vilevile, kinachonisumbua si hii nyongeza ndogo ya sh. 100 kwa abiria wa kawaida na sh. 50 kwa wanafunzi, bali ni tabia yetu ya kukaa kimya tunaponyanyaswa kwa bei isiyo halali tukisubiri  Serikali ichukue hatua bila kuambiwa au kulalamikiwa! Mimi najua, wananchi wengi kwa muda mrefu sana wanatozwa nauli kubwa ya sh.500 mpaka 1,000 badala ya sh. 300, lakini wamekuwa kimya. Wanasubiri nauli zikipanda kihalali walalamike kwenye luninga na magazeti. Tuwe wakweli!

Waandishi wa habari mnahudhuria vikao hivi vya nauli, lakini siwasikii wala kuwasoma mkiwasahihisha wananchi wakisema hawakuhusishwa! Ndugu Wanahabari, mnaelewa kuwa sekta hii ya usafiri wa abiria imetawaliwa na sekta binafsi, Serikali haina mabasi yake ili kuweka nauli elekezi. Hivyo Serikali haina budi  kusikiliza kilio cha wamiliki vilevile, ingawa nao wanashindwa kuibua hoja za msingi za kuendeleza sekta hii, wanakimbilia nyongeza ya nauli tu. Kwa mfano, nchi nyingi zinazotuzunguka zimeondoa au kupunguza sana ushuru wa mabasi na mataili, lakini kwa ushawishi uliokwenda shule wa wadau. Ushawishi wa aina hiyo bado sijauona kutoka kwa wamiliki wa daladala au mabasi!

Pili, kati ya Septemba, 2012 na Oktoba, 2012 SUMATRA ilipokea vilevile maombi ya wasafirishaji abiria wa masafa marefu wakitaka ongezeko la nauli  kwa mabasi ya kawaida kutoka shiling 30.67 kwa abiria kwa kilomita hadi shilingi 42.70. Aidha, kwa basi la hadhi ya kati (semi-luxury) watoa huduma waliomba kuongeza nauli kutoka shilingi 45.53 hadi shilingi 67.61 kwa abiria kwa kilomita sawa na ongezeko la asilimia 48.5. Viwango vitumikavyo sasa viliwekwa Machi, 2011.

Baada ya mvutano mrefu, kama nilivyoelezea kwa upande wa daladala, SUMATRA ilikataa ongezeko la hadi asilimia 48.5 badala yake SUMATRA ikaridhia ongezeko dogo la kati ya asilimia 13.23 na 20.28. Kwa mfano, kiwango cha nauli kilichoombwa kwa basi la daraja la kawaida kwa njia ya lami kilikuwa shilingi 42.70 kwa abiria kwa kilomita na SUMATRA ikaridhia shilingi 36.89. Mfano halisi: nauli ya Dar es Salaam - Arusha kwa basi la Kawaida ilikuwa inapendekezwa iwe shilingi 26,300 kutoka nauli ya sasa ya shilingi 18,900. SUMATRA imeridhia shilingi 22,700.

Tarehe 21 Februari, 2012 SUMATRA ilipokea maombi kutoka Kampuni ya Reli (TRL) ikiomba nauli ya abiria wanaotumia huduma za usafiri wa reli ya kati kuongezwa kwa asilimia 25 kwa daraja la kwanza na la pili, na asilimia 50 kwa daraja la tatu. Viwango vilivyopo sasa vilianza kutumika miaka minne iliyopita yaani toka Februari, 2009.

TRL iliomba ongezeko la asilimia 50% ya nauli za abiria wa daraja la tatu na SUMATRA ikaridhia asilimia 44.1. Kwa ongezeko hili kwa mfano, nauli ya daraja la tatu kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma itakuwa shilingi 27,500 badala ya shilingi 19,084 ya sasa.

Ndugu Wanahabari, naomna nimalizie kwa kuwaomba Watanzania kujenga utamaduni wa kuhudhuria vikao vinavyowahusu kama hivi vya nauli. Vilevile, tusidharau kugombea nafasi kwenye vyombo hivi vya kutetea walaji kama vile Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na SUMATRA. Vyombo hivi vina umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kila siku. Kwa mfano mwaka 2009, Baraza hili liliweza kuishawishi SUMATRA kushusha viwango vya nauli za mabasi ya mijini kwa asilimi 12 na mabasi ya masafa marefu kwa asilimia 11 kufuatia kutokea kwa unafuu wa bei ya mafuta nchini. Na pale barabara imekuwa ya lami, Baraza hili huisukuma SUMATRA kushusha viwango vya nauli.

Namalizia kwa kuwaonya wamiliki wa mabasi kuheshimu sheria kwa sababu najua wataendelea na nauli wanazozijua wenyewe, nje kabisa ya nyongeza hii ndogo. Nawaagiza SUMATRA kuendesha kampeni nchi nzima, bila kusahau vijijini ambako wananchi wananyanyaswa sana, kuhakikisha kuwa sheria inafuatwa na wakorofi tunawafungia kabisa lesenina kubeba abiria. Wanaasa wananchi vilevile, ukinyanyaswa ukakaa kimya, unajitakia mwenyewe hasara unayobebeshwa.


Wizara ya Uchukuzi
Dodoma
11 Aprili, 2013

No comments:

Post a Comment