MHARIRI Msanifu wa Gazeti la
Mtanzania, Khamis Mkotya (35) juzi alitangaza rasmi nia ya kugombea ubunge
katika Jimbo la Chemba, lililopo Mkoa wa Dodoma.
Mkotya ambaye kitaaluma ni
mwandishi wa habari na kijana msomi mwenye Shahada ya Siasa na Uongozi,
alitangaza nia hiyo mbele ya waandishi wa habari, katika ukumbi wa Dodoma
Hotel.
Mkotya ambaye ni kada wa Chama Cha
Mapinduzi ni miongoni mwa waandishi wa habari za Bunge, ambaye amekuwa mstari
wa mbele katika kuwatetea wananchi wa Chemba kupitia taaluma yake.
Akizungumza katika mkutano huo,
Mkotya ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Mirijo Chini wilayani Chemba, alisema changamoto
za jimbo hilo ndizo zilizomsukuma kuwania nafasi hiyo.
Katika mkutano huo, Mkotya alisema kwa
muda mrefu ametumia taaluma yake kupiga kelele kuibua matatizo na kero za
wananchi wa Chemba na baadhi kupatiwa ufumbuzi, hivyo umefika muda kuomba
ridhaa yao ili aweze kuwatumikia kimamlaka zaidi.
Uzoefu wake katika masuala ya Bunge
kama mwandishi wa habari za Bunge, pia utakuwa chachu na msaada mkubwa kwake
katika kutimiza dhana ya uwakilishi ndani ya Bunge.
Ndugu zangu sijakurupuka katika kufikia
uamuzi huu, nimekaa, nimetafakari na kujipima mwenyewe na kubaini kwamba
ninatosha. Uwezo wa kutekeleza majukumu ya kibunge ninao, nia ya kuwatumikia
wananchi wa Chemba ninayo na sababu za kugombea ninazo.
No comments:
Post a Comment