Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Vijana wametakiwa kutokubali kutumiwa vibaya na
baadhi ya wanasiasa kwa maslahi ya watu wachache huku hao wanaowatumia
wanasonga mbele kimaendeleo na wao wanazidi kurudi nyuma.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa kijiji cha Kikomolela
kilichopo jimbo la Mchinga na mtaa wa Likotwa uliopo Jimbo la Lindi mjini
waliohudhuria kampeni ya kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na
urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema kuna baadhi ya wanasiasa
wanawatumia vijana kufanya vurugu ambazo hazina faida katika jamii
zaidi ya kuleta hasara kwani wanaharibu miundombinu ikiwa ni pamoja na
barabara, majengo na hivyo kurudisha maendeleo nyuma.
Kuhusu uchaguzi aliwaomba wananchi wote wa maeneo hayo
wakiwemo wanachama wa vyama vya upinzani kuwachagua wagombea wa CCM ambao
watazidi kuwaletea maendeleo kwani Serikali ya CCM imefanya mambo mengi
ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, elimu, maji na
barabara.
“Siku ya uchaguzi ikifika chukua kadi yako ya kupigia kura
wahi mapema kituoni kachague viongozi bora utakaoona watakuletea maendeleo na
viongozi hawa wanapatikana ndani ya CCM. Msiogope! siku hiyo kutakuwa na
usalama wa kutosha”, MNEC huyo alisisitiza.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Mchinga Saidi
Mtanda alisema Serikali ya CCM imefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya umeme na katika eneo
hilo vijiji 40 kati ya 47 vikiwemo vijiji vya Nangaru na Kitomanga karibu
vitawasha umeme kwa gharama ya shilingi 45,000/=.
Mtanda alisema, “Nawaomba wenzetu kutoka vyama vya upinzani
dumisheni hali ya Amani na utulivu iliyopo kwani kuna baadhi yenu mnatoa
kauli za kuwatisha wanachama wa CCM kitendo ambacho siyo kizuri”,.
Naye mgombea Ubunge wa Jimbo la Lindi mjini Kaunje Selemani
aliwaomba wananchi waliohudhuria mkutano huo kumpigia kura ya ndiyo na
kuwaahidi kusimamia Ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo itawaletea
maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo za nishati na madini,
kilimo, elimu, afya, maji, umeme na barabara.
Katika mikutano hiyo jumla ya wanachama watatu walihama
kutoka chama cha Wananchi (CUF) na kujiunga na CCM.
Wakati huo huo akiwa njiani kuelekea kijiji cha Kikomolela
msafara wa Mama Kikwete ulisimama Shule ya Msingi Moka ambapo walimu na
wanafunzi walikuwa wamesimama pembeni ya barabara wakiwa wameshika bango
lililoandikwa SHULE YA MSINGI MOKA TUNAUJUMBE KWA MAMA KIKWETE.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo Abdala Mkanjima
alimuomba Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni Mwalimu awasaidie kufanya wire ring
katika shule yao kwani umeme umepita shuleni hapo.
Mama Kikwete aliahidi kulishughulikia suala la umeme katika
shule hiyo. Pia aliwaasa wanafunzi wasome kwa bidii ili waweze
kujikomboa kimaisha na kuwa viongozi wazuri hapo baadaye ambao
watalisaidia taifa lao na jamii inayowazunguka.
OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YATANGAZA MFUMUKO WA BEI
Na: Veronica Kazimoto Dar es Salaam
08/10/2015
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi
Septemba, 2015 umepungua hadi asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa mwezi
Agosti, 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu Ephraim
Kwesigabo amesema kupungua huko kwa mfumuko wa bei kunamaanisha kuwa, kasi ya
upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2015
imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti,
2015.
“Kupungua kwa Mfumuko wa Bei wa mwezi
Septemba, 2015 kumechangiwa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula
na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Septemba, 2015
zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014”, amesema Kwesigabo.
Aidha, Kwesigabo amefafanua kuwa, mwenendo
wa bei za baadhi ya vyakula zilizoonyesha kupungua mwezi Septemba, 2015
zikilinganishwa na bei za mwezi Septemba, 2014 ni pamoja na bei za ndizi za
kupika kwa asilimia 4.0, matunda (asilimia 2.7), nazi (asilimia 13.3) na
mbogamboga kwa asilimia 3.5.
Ameongeza kuwa baadhi ya bei za bidhaa
zisizo za vyakula zilizoonyesha kupungua mwezi Septemba, 2015 zikilinganishwa
na bei za mwezi Septemba, 2014 ni pamoja na bei za gesi kwa asilimia 4.9,
mafuta ya taa (asilimia 11.7), senti ya sofa (asilimia 5.7), dizeli (asilimia
3.5) na vifaa vya kielektoniki kwa asilimia 1.2.
Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki,
Mfumuko wa Bei nchini una mwelekeo unaokaribiana kwa mfano Mfumuko wa Bei
wa mwezi Septemba, 2015 nchini Kenya umeongezeka kidogo hadi asilimia 5.97
kutoka asilimia 5.84 mwezi Agosti, 2015 na Uganda umeongezeka hadi asilimia 7.2
kutoka asilimia 4.80 mwezi Agosti, 2015.
Kupungua kwa mfumuko nwa bei kwa mwezi
septemba kumesababishwa na Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 159.04 kwa mwezi
Septemba, 2015 kutoka 149.93 mwezi Septemba, 2014. Mfumuko wa Bei wa bidhaa za
Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwezi Septemba, 2015 umepungua hadi asilimia 9.6
kutoka asilimia 10.2 ilivyokuwa mwezi Agosti, 2015.
.
No comments:
Post a Comment