
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao
Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri
Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki
(kushoto) kuhusu utendaji wa Wakala hiyo leo wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Angella Kairuki
katika Ofisi za Wakala hiyo leo jijini Dar es salaam.
Na Aron Msigwa MAELEZO
Serikali imepiga marufuku matumizi ya Barua pepe za
kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za Serikali na
kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya
Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la
kuimarisha mawasiliano kwa njia ya Mtandao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angella Kairuki
alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao (
e Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji na ufanisi wa
matumizi ya TEHAMA Serikalini.
“Sasa kuna watumishi 7000 wanaotumia anwani
za Barua pepe za Serikali ,idadi hii ni ndogo lazima iongezeke, hatuwezi
kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali kwa kutumia Barua Pepe nje ya
mfumo huu” Amesisitiza
na kuongeza kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye
mawasiliano binafsi.
Amesema kwa kutambua umuhimu wa uimarishaji wa
mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA katika
utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ipo haja ya kuweka
msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua Pepe za Serikali.
Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa Wakala hiyo
kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa Wizara,
Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa na mfumo rasmi wa Serikali
ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano.
“Katika hili ninatoa siku 60 muhakikishe
kuwa mnakamilisha kwa Taasisi zilizobaki ili kwa wale watakaopuuzia hatua
zianze kuchukuliwa” Ameeleza Mhe. Angella.
Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa Wakala hiyo kuweka
mpango wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo
kazini kwa kujenga utaratibu wa kuwarithisha uzoefu watumishi ili
kuendelea kuimarisha ufanisi na utendaji wa Wakala hiyo.
Mhe. Kairuki amewataka kuwa wabunifu katika kuanzisha
mifumo mipya ya TEHAMA ili kuimarisha dhana ya Serikali mtandao ili
kupunguza gharama hadi kufikia asilimia 5 ya fedha zinazotumika kuendeshea
masuala mbalimbali ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA.
Akizungumzia kuhusu ununuzi wa vifaa vya TEHAMA
serikalini ameitaka Wakala hiyo kutoa ushauri ili kudhibiti mianya ya
ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika kununulia vifaa hivyo kwa
gharama kubwa wakati vinaweza kupatikana kwa bei ya kawaida.
“katika
hili Serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayebainika katika upotevu wa
mapato muhakikise mnazisaidia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika
masuala ya ununuzi wa mifumo na vifaa vya TEHAMA ili mifumo inayonunuliwa iwe
na manufaa kwa wananchi na thamani halisi ya fedha”
Amesema Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma
kupitia mtandao ili wananchi waweze kupata huduma hizo mahali walipo kwa
gharama nafuu na kutoa wito kwa watumishi wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov)
kuwa wabunifu katika kutengeneza programu mbalimbali na mifumo salama
itakayowasaidia wananchi kupata huduma.
Aidha, katika hatua nyingine ameitaka e-Gov
kuendelelea kujenga uwezo katika kudhibiti dharura na majanga mbalimbali
yanayoweza kujitokeza katika matumizi ya TEHAMA na kuitaka Wakala hiyo iendelee
kulifanyia kazi suala la kuwezesha mifumo ya Serikali kuzungumza kati ya
taasisi moja hadi nyingine ili huduma zote ziweze kupatikana katika eneo
moja na kuondoa urudufu wa mifumo iliyopo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali
Mtandao (e-Gov) Dkt. Jabiri Bakari akitoa taarifa ya utendaji wa Wakala hiyo
amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali toka kuanzishwa kwake
Julai 11, 2012 imeendelea kupata ufanisi katika uimarishaji wa Serikali Mtandao.
Amesema kuwa Wakala hiyo inaendelea kuhakikisha kuwa
huduma za Serikali zinawafikia wananchi kupitia mtandao mahali walipo na
kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo la huduma zote za Serikali kupatikana chini
ya dirisha moja.
Aidha amesema kuwa Wakala ya Serikali Mtandao
itaendelea kuhakikisha kuwa usimamizi wa viwango vya matumizi ya TEHAMA katika
Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali vinazingatiwa
.
.
No comments:
Post a Comment