Na Anna Nkinda – Addis
Ababa
Umoja wa wake
wa Marais wa Afrika wa Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi (OAFLA) umetakiwa
kutotegemea fedha za wafadhili katika kujiendesha bali wabuni miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulipaji wa
michango yao ya kila mwaka.
Wito huo umetolewa jana
na aliyekuwa Rais wa Umoja huo Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehupifo Pohamba wakati
akifungua mkutano wa 12 uliofanyika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini
Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mama Pohamba alisema
kuwa hadi sasa umoja huo umefanikiwa kuimarika kimawasiliano ya ndani kwa ndani
baina ya wanachama wake na hivyo kuweza kuendesha kampeni ya kuondoa na
kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya
Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambayo yanasababisha vifo .
“Ninawashukuru
wanachama ambao wameanza kampeni ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya
Ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) katika nchi zao, kwa
kutoa elimu kwa jamii hii itasaidia
kupatikana kwa kizazi ambacho hakina maambukizi ya Ugojwa huu na kupunguza vifo
vya kina mama wajawazito na watoto”, alisema Mama Pohamba.
Akiwakaribisha wake hao
wa Marais katika mkutano huo mke wa
waziri Mkuu wa nchi hiyo Mama Roman Tesfaye
alisema kuwa umoja huo ni mzuri kwani unawaunganisha na kuwa kitu kimoja
huku wakitimiza majukumu yao katika
jamii kutokana na malengo waliyojiwekea.
Mama Tesfaye alisema
kuwa tatizo kubwa linaloukabili umoja huo ni upatikanaji wa rasilimali kwani
wanategemea fedha kutoka kwa wafadhili lakini kuna baadhi ya wanachama
wanaojitahidi kwa hali na mali kuhakikisha kuwa umoja huo unafanya kazi zake
bila ya kutetereka.
Wakati huo huo Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete aliwahimiza wake
hao wa marais kuunga mkono kampeni ya Shirika la kimataifa la AMREF ya
kuwasomesha wakunga 15000 barani Afrika
ili kupata wataalamu wengi zaidi ambao watawahudumia kina mama wajawazito
wakati wa kujifungua na hivyo kupunguza vifo vyao na vya watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi.
Kampeni hiyo ambayo
ilizinduliwa katika nchi mbalimbali Duniani
nchini Tanzania ilizinduliwa na Mama Kikwete mwishoni mwa mwaka jana
katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar Salaam.
Wakiongea kwa nyakati
tofauti wakati wakisaini kuonyesha kuwa wanaiunga mkono kampeni hiyo wake hao
wa marais walisema kuwa kampeni hiyo ni nzuri kwani kama kutakuwa na wakunga wa
kutosha vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinavyotokana na tatizo la
uzazi vitapungua barani Afrika.
Katika mkutano huo pia
ulifanyika uchaguzi wa kumchagua Rais na Makamu Rais wa Umoja huo ambapo Mke wa
Rais wa Chadi Mama Hinda Deby Itno alichaguliwa kuwa Rais na Mke wa Rais wa
Rwanda Mama Janeth Kagame alichaguliwa kuwa makamu Rais.
Mkutano huo wa wake wa
marais wa Afrika ambao ulihudhuriwa na mke wa Rais Mama Salma Kikwete ulienda
sambamba na mkutano wa 21 wa wakuu wa nchi na viongozi wa Serikali wa Afrika
unaomalizika leo mjini Addis Ababa.
No comments:
Post a Comment