Tamasha la muziki la kimataifa ambalo hufanyika Juni 21 kila
mwaka la ‘World Music Day’ linafanyika kesho (Ijumaa) katika viwanja vya posta
Kijitonyama jijini Dar es Salaam ambapo wanamuziki Kala Jeremiah, Ben Paul,
bendi ya Twanga pepeta na wengineo wanaotamba katika tasnia ya muziki nchini
watalipamba tamasha hilo.
Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Umoja wa Ulaya wa taasisi
za utamaduni (EUNIC) zikiwamo Aliance France-Dar es Salaam, Goethe
Institut-Tanzania na British Council linalenga kutoa fursa kwa wanamuziki
wakongwe na wachanga kukutana katika jukwaa hilo la kimataifa ambapo mashabiki
wataingia bure.
Mratibu wa Tamasha hilo Abel Shuma ambaye pia ni Mratibu wa
Shughuli za Utamaduni Alliance France Dar es Salaam, anawataja wanamuziki
wengine watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo kuwa ni pamoja na Godzila, Barnaba
na bendi yake, mwanamuziki mkongwe wa Reggae Jhiko Man bila kusahau ngoma za
asili kutoka kwa kundi la Super Maya Baikoko na Makini Kids.
Kala Jeremiah analielezea onyesho hilo kama mazao ya kazi
nzuri aliyoifanya katika muziki wake “Nimepata faraja sana kualikwa kutumbuiza
kwenye world music day, inaonyesha ni kwa jinsi gani muziki wangu unakubalika
na kutambulika kitaifa na kimataifa”
Shirika la ndege la FasJet kupitia
kwa Afisa Masoko Mtendaji Lucy Mbogoro linajivunia kudhamini tamasha hilo likitumia
nafasi hiyo kurejesha shukran kwa Watanzania kwa mchango wao mkubwa katika
shirika hilo kwa kuchagua kutumia huduma zake za usafiri wa anga.
Mbogoro anasema “World Music Day ni fursa nzuri ya kukutana
na wadau wetu kwakuwa tamasha litawakutanisha watu wa mataifa mengi watapata
kujua huduma zetu katika wakati huu tunaoelekea kuanzisha safari za ndege za
kimataifa katika nchi za Afrika Kusini, Zambia na Rwanda”
Tamasha hilo ambalo limedhaminiwa na Fastjet, Pepsi, Total na
balozi za Ujerumani na Ufaransa.
No comments:
Post a Comment