Ndugu John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa Oktoba 29, mwaka
1959 katika kijiji cha Chato, Wilayani Biharamulo katika Mkoa wa Kagera. Hivi
sasa Chato ni Wilaya katika Mkoa wa Geita. Ndugu Magufuli ni Daktari wa Falsafa
(PhD) ya Kemia. Ana mke na watoto saba. Alichaguliwa kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba, 2015 kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (C.C.M). Aliapishwa na kuanza rasmi majukumu yake ya kuiongoza
Tanzania tarehe 5 Novemba, 2015.
Tangu ameingia madarakani, Rais Dkt. Magufuli, ameonesha
kuwa ana sifa zote muhimu za uongozi. Ana dira, maono na malengo kuhusu
anakotaka Taifa liende. Ana mikakati ya kutekeleza dira na maono yake. Haogopi
kufanya maamuzi makini. Ana kiu ya kuona Taifa linapata maendeleo.
Amejipambanua kuwa yeye ni mtetezi wa wanyonge na dhamira yake kubwa ni kuona
wananchi wanapata huduma bora za jamii na kero zao zinaondoka.
2.0. ELIMU NA MAFUNZO
Rais Dkt. Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya
msingi Chato mwaka 1967 na kumaliza mwaka 1974. Mwaka 1975 alianza masomo ya
sekondari katika Shule ya Seminari ya Katoke Mkoani Kagera. Mwaka 1977
alihamia shule ya sekondari ya Lake iliyopo Mkoani Mwanza na kuhitimu
kidato cha Nne mwaka 1978. Kuanzia mwaka 1979 hadi 1981 alifanya masomo ya
kidato cha Tano na Sita katika shule ya Sekondari ya Mkwawa Mkoa wa
Iringa .
Mwaka 1981 hadi 1982 alisoma Chuo cha Ualimu Mkwawa na
kuhitimu Stashahada ya Ualimu ya Masomo ya Kemia na Hisabati. Mwezi Julai
hadi Disemba mwaka 1983, Dkt. Magufuli alipata mafunzo ya kijeshi katika
Jeshi la kujenga Taifa kikosi cha Makutupora mkoa wa Dodoma. Mwezi
Januari hadi Machi 1984 alihamishiwa kikosi cha mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa
Makuyuni, Arusha. Mwezi huo wa Machi alihamia kikosi cha Jeshi la Kujenga
Taifa Mpwapwa Dodoma na kumaliza mafunzo mwezi Juni 1984.
Mwaka 1985 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusoma
Shahada ya kwanza ya Sayansi na Ualimu akijikita katika masomo ya Kemia na
Hisabati. Alitunukiwa Shahada hiyo mwaka 1988. Mwaka 1991 hadi 1994
alisoma na kutunukiwa Shahada ya Uzamili katika fani ya Kemia iliyotolewa na
Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo Kikuu cha Salford cha Uingereza. Mwaka
2006 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya Shahada ya
Uzamivu katika Fani ya Kemia na kufanikiwa kuhitimu mwaka 2009.
3.0. UZOEFU WA NDANI YA SERIKALI
Baada ya kuhitimu masomo yake ya Stashahada ya Ualimu, mwaka
1982 hadi 1983 Dkt. Magufuli alikuwa Mwalimu katika shule ya Sekondari ya
Sengerema iliyopo Mkoani Mwanza akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1989 alijiunga na Chama Cha Ushirika cha Nyanza Mkoani Mwanza, ambapo
alifanya kazi kama Mkemia Mkuu hadi mwaka 1995.
Mwaka 1995 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo
Mashariki Mkoa wa Kagera. Baada ya Uchaguzi, Rais wa Awamu ya Tatu,
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya
Ujenzi nafasi ambayo aliitumikia hadi mwaka 2000. Mwaka 2000
alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki
lakini mara hii akipita bila kupingwa. Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa
Waziri kamili wa Wizara ya Ujenzi hadi mwaka 2005.
Mwaka 2005 Rais Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya tatu
kuwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki, kwa mara nyingine akipita bila
kupingwa. Baada ya uchaguzi, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2008 ambapo alihamishiwa Wizara ya Mifugo
na Maendeleo ya Uvuvi hadi hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 Dkt. Magufuli alichaguliwa kwa mara ya nne
kuwa Mbunge lakini, kufuatia mgawanyo wa majimbo uliofanyika, mara
hii katika Jimbo jipya la Chato. Baada ya uchaguzi, aliteuliwa kuwa
Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015.
Wakati akiwa Mbunge na Waziri, Dkt. Magufuli amefanya
shughuli na kushika nyadhifa kadhaa ndani na nje ya nchi. Mwaka 2014, Dkt.
Magufuli alishiriki katika Bunge Maalum la Kutunga Katiba Mpya akiwa ni
Mjumbe wa Bunge hilo. Aidha, wakati akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi aliweza kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza (Co-Chair) wa Mkutano wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Makazi (UN-Habitat).
Tarehe 25 Oktoba, 2015 Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tarehe 5 Novemba,
2015 aliapishwa kushika rasmi wadhifa huo.
4.0. UZOEFU WA UONGOZI NDANI YA CHAMA
Rais Dkt. Magufuli alijiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
mwaka 1977. Amekuwa Mwanachama mwaminifu na ameshika nafasi mbalimbali za
uongozi ndani ya Chama. Nafasi alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Mjumbe wa
Kamati ya Siasa ya Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya, Mjumbe wa
Mkutano Mkuu wa Wilaya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, Mjumbe wa Mkutano
Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Sambamba na kushika nafasi mbalimbali za uongozi, Dkt.
Magufuli mara zote alijitoa kukitetea Chama na kuhakikisha kinapata ushindi.
Alishiriki kikamilifu kuwafanyia kampeni wagombea wa CCM katika Chaguzi Ndogo
zilizofayika katika majimbo ya Busanda, Biharamulo Magharibi na Igunga na
kupata ushindi. Katika Mkutano Mkuu wa CCM wa tarehe 11 – 12 Novemba
mwaka 2012, Dkt. Magufuli alikuwa miongoni mwa Mawaziri wachache waliopata
fursa ya kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya
Mwaka 2010 – 2015. Alielezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani, hususan katika
sekta ya miundombinu.
Tarehe 11 mwezi Julai, 2015 Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM
ulimchagua na kumteua Dkt. Magufuli kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Aliinadi vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM (2015) na
kukiwezesha Chama kupata ushindi mkubwa. Tarehe 25 Oktoba, 2015 alichaguliwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nafasi hiyo imemwezesha
kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa.
5.0. UFANISI KATIKA UONGOZI
Dkt. Magufuli ni kiongozi mnyenyekevu, aliye na hofu ya
Mungu, mkweli, mtekelezaji wa ahadi, mwadilifu, shupavu, mahiri, mbunifu,
mtafiti, mchapakazi na mtetezi wa wanyonge. Ni kiongozi mpenda haki na mchukia
dhuluma, rushwa, ufisadi na ubaguzi wa aina yoyote ile. Ni kiongozi
mwenye msimamo na mtetezi wa yale anayoyaamini.
Katika nyadhifa zote alizopata kutumikia alifanya kazi kwa
uadilifu na umahiri mkubwa. Amejidhihirisha na kujipambanua kuwa ni mfuatiliaji
na msimamizi wa sheria. Akiwa Mwalimu Sengerema Sekondari aliwezesha wanafunzi
wote wa darasa lake kufaulu masomo ya Hesabu na Kemia aliyokuwa akiyafundisha.
Akiwa Mkemia Mkuu wa Chama cha Ushirika cha Nyanza alisimamia vyema ubora wa
uzalishaji wa mafuta ya Pamba na kuifanya Kampuni ya Nyanza kuwa mzalishaji
mzuri wa mafuta ya Pamba.
Akiwa Waziri wa Ujenzi anakumbukwa kwa kubuni na kusanifu
miradi ya ujenzi wa barabara, kusimamia vizuri matumizi ya fedha na kuhakikisha
miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na kwa wakati uliopangwa. Uwezo wake
katika kubuni na kusanifu miradi ya barabara uliigwa na nchi majirani, ikiwemo
Kenya. Ameondoka Wizara ya Ujenzi akiwa amesimamia ujenzi wa zaidi ya Kilometa
17,000 za barabara za lami, madaraja makubwa zaidi ya 14 na madaraja madogo
madogo zaidi ya 7,000 na vivuko. Aidha, alisimamia vizuri taasisi mbalimbali za
Makandarasi, Wahandisi, Wabunifu na Wakadiriaji Majengo.
Dkt. Magufuli pia anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kuweka
kumbukumbu ya kazi zake. Akiwa Wizara ya Ujenzi aliweza kutaja majina ya
barabara zilizojengwa au zilizokuwa katika hatua za ujenzi, urefu wake, majina
ya wakandarasi pamoja na gharama za ujenzi bila kusoma mahali popote.
Wakati wa Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa alimwita “Askari wa
Mwavuli”.
Akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
alisimamia upimaji wa ardhi za vijiji na viwanja vya makazi, na kushughulikia
migogoro mingi ya ardhi iliyowahusu wananchi wa maisha ya chini. Wakati akiwa
Waziri wa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi alikuwa maarufu wa kutambua na
kutaja idadi ya mifugo, kama vile samaki, ngómbe, mbuzi, kondoo,
kuku, mbwa n.k. Kitendo cha kukamata meli ya kichina iliyokuwa ikivua samaki
kwa wizi ndani ya Bahari Kuu ya Hindi eneo la Tanzania kilidhihirisha uzalendo
kwa Taifa lake. Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Kikwete alimpachika
jina maarufu la “Tingatinga”.
Sifa hizi nzuri ameendelea nazo hata baada ya kuchaguliwa
kuwa Rais. Katika miezi michache ya uongozi wake amethibitisha anatekeleza
ahadi. Aliahidi kutoa elimu bila malipo na kuanzisha Mahakama ya Mafisadi.
Ameweza kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma kwa kuondoa watumishi hewa na
kuchukua hatua dhidi ya watumishi wa umma wasio waaminifu, wala rushwa, wazembe
na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Ameweza kudhibiti matumizi
mabaya ya fedha za umma na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Kwa
hakika Dkt. Magufuli anaakisi uongozi bora unaopaswa kuigwa na viongozi wengi
Barani Afrika na Dunia.
6.0. DHIMA YA UONGOZI WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO 2015 –
2020) NA MALENGO YAKE MAHSUSI
Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020
inazielekeza serikali zake kutumia nguvu zake zote kuendelea kupambana na
changamoto kubwa nne;- Kwanza kuondoa umaskini, Pili, kupunguza tatizo la
ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, Tatu, kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na
ubadhirifu wa mali ya umma, na Nne, kuendelea kudumisha amani, ulinzi na
usalama wa maisha ya Watanzania na mali zao.
Sambamba na kutekeleza mambo hayo makubwa manne, kipindi cha
Kampeni na wakati akizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tarehe 20 Novemba, 2015 Rais Dkt. Magufuli alitaja malengo mahsusi ya Serikali
ya Awamu ya Tano. Malengo hayo ni haya yafuatayo:
· Kudumisha Muungano, Amani na Umoja wa
Tanzania. Serikali haitamwonea aibu mtu mwenye nia ya kuvunja Muungano na
kuvuruga amani na mshikamano katika nchi. Hili alilidhihirisha vizuri wakati wa
uchaguzi wa marudio huko Zanzibar, kwani Uchaguzi ulifanyika kwa amani na
utulivu.
· Kujenga Uchumi wa Viwanda ili kufikia azma ya
kuwa nchi ya uchumi wa kati kulingana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya
Taifa 2025. Viwanda vinalengwa ni vyenye kutumia nguvu kazi kubwa,
malighafi za ndani ya nchi, kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje
ya nchi. Nia ni kukabiliana na tatizo la ajira na umasikini;
· Kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya
kiuchumi, hususan miundombinu ya usafiri na nishati;
· Kuimarisha huduma za jamii, hususan elimu,
Afya na Maji. Lengo ni kuhakikisha huduma hizo zinapatakana sio tu kwa urahisi
bali pia kwa ubora unaostahili ili kukabiliana na maadui ujinga, umaskini na
maradhi;
· Kusimamia uwajibikaji wa utumishi wa umma na
kuondoa urasimu ndani ya Serikali. Lengo ni kuhakikisha watumishi wa umma
wanafanya kazi kwa ueledi, uadilifu na kujituma ili kuwawezesha wananchi kupata
huduma kwa wakati;
· Kuimarisha usimamizi wa rasilimali za
nchi, ikiwemo kuhifadhi mazingira na kuzidisha vita dhidi ya ujangili. Lengo ni
kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha watu wote wa kizazi cha sasa na
kijacho. Aidha, ukusanyaji wa mapato ya Serikali na udhibiti wa matumizi ya
Serikali nao utaimarishwa;
· Kusimamia utawala bora unaozingatia
sheria na haki za binadamu. Jitihada za makusudi zitaelekezwa katika kuzidisha
mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, dhuluma na uonevu wa aina yoyote. Aidha,
maslahi ya makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo wanawake, wazee, watu wenye
ulemavu na watoto yatalindwa. Kwa upande mwingine, wananchi watahimizwa
kuheshimu na kufuata sheria za nchi;
· Kulinda usalama wa raia na mali zao
kwa kupambana na uhalifu, ikiwemo wizi, ujambazi, tatizo la dawa za kulevya
n.k.
· Kudumisha na kuendeleza ujirani
mwema, mahusiano mema na Mataifa mengine duniani pamoja na Mashirika ya
Kimataifa na Kikanda;
· Kuendeleza na kusimamia vizuri
shughuli za michezo, sanaa, burudani na utamaduni, ikiwemo kukuza lugha ya
Kiswahili.
HITIMISHO
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi na
kuwataka watanzania washiriki kufanya kazi kwa bidii na maarifa
ndani ya falsafa ya HAPA KAZI TU. Dhamira hii inakusudia kuwezesha Taifa
letu kufikia Uchumi wa Kati uaoongozwa na Viwanda ili kutimiza malengo ya Dira
ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment