Na.
Rodney Thadeus - China.
Jina la Rais Dk John
Magufuli limekuwa gumzo nchini
China kutokana na Serikali yake kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya
rushwa na ufisadi.
Aliyekuwa Balozi wa China nchini
Tanzania Lu Youqing pamoja na baadhi ya
wafanyabiashara wakubwa wa China ambao wanataka kuwekeza nchini Tanzania,
wamemuelezea Magufuli kama Rais aliyeonesha ushujaa kupambana na rushwa ambayo
imekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa nchi za Afrika.
Rais Magufuli alielezewa
katika majadiliano maalum yaliyoandaliwa kuwakutanisha wafanyabiashara wa
Tanzania na China kujadili fursa za kibiashara, ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya
Kimataifa ya Canton yaliyofanyika katika jiji la Guangzhou nchini China.
“Tangu Rais Magufuli aingie
madarakani kuna mambo makubwa yamefanyika katika mapambano dhidi ya rushwa.
Serikali ya China itaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli kupambana na
rushwa,” alieleza Balozi Lu Youqing.
Balozi Lu alieleza wazi
kwamba msimamo wa Rais Magufuli wa kutovumilia vitendo vya rushwa, utajenga
misingi imara ambayo itasaidia Tanzania kutimiza malengo yake ya kuwa nchi ya
uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Pamoja na kusifu juhudi
zinazofanywa na Serikali kudhibiti rushwa nchini Tanzania, Balozi Lu amewaeleza
wafanyabiashara wa China wanaotaka kuwekeza nchini kuwa Tanzania ni nchi yenye
mazingira bora ya uwekezaji kutokana na uimara wa ukuaji wa uchumi ambao
umekuwa ukikua kwa zaidi ya asilimia saba kwa mwaka na kuwa nchi inayoongoza
kwa ukuaji wa uchumi Afrika Mashariki.
“Tanzania ni nchi yenye
amani na utulivu wa kisiasa na kuleta matumaini katika uwekezaji. Napenda
kuwashauri wafanayabiashara na makampuni yanayowekeza Tanzania kumuunga mkono
Rais katika vita ya rushwa,” alieleza Balozi Lu huku akisisitiza kuendelezwa
kwa ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Pia katika mkutano huo,
Makamu wa Rais Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo wa China kwa nchi za Afrika (CAD
Fund) ambao unasaidia makampuni kuwekeza Afrika, Wang Yong alieleza kuwa
Tanzania ni nchi muhimu kwa uwekezaji miongoni mwa nchi za Afrika hasa katika
kilimo, madini na nishati.
“Nazishukuru Serikali za
Tanzania na China kupitia Balozi Kairuki na Balozi Lu kwa kuwezesha makampuni
ya kutoka China kuwekeza nchini Tanzania,” alishukuru Yong.
Mkutano wa kibiashara kati
ya wafanyabiashara wa Tanzania na China ambao ulienda sambamba na Maonesho ya
Kimataifa ya Canton katika jiji la Guangzhou nchini China, ulilenga
kuwakutanisha wafanyabiashara hao na kufungua fursa mbalimbali za kibiashara
huku Watanzania wengi walionekana kuvutiwa zaidi na biashara ya muhogo ambapo
kampuni ya Sino Light International Holdings ilionesha nia ya kununua tani
100,000 za muhogo mkavu kutoka Tanzania kila mwezi.
Baadhi ya wafanyabiashara
kutoka Tanzania wakifuatilia mada katika mkutano wa kujadili fursa mbalimbali
za biashara na uwekezaji baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa China
wakati wa maonesho ya Kimataifa ya Bisashara ya Canton yaliyomalizika hivi
karibuni jijini Guangzhou, China. Picha
zote na Rodney Thadeus-MAELEZO
Aliyekuwa Balozi wa China
nchini Tanzania, Balozi Dkt. Lu Youqing
akizungumza wakati wa majadiliano ya kibiashara baina ya wafanyabiashara wa
Tanzania na China ambayo yalienda sambamba na maonesho ya Kimataifa ya Biashara
ya Canton jijini Guangzhou, China.
No comments:
Post a Comment