Serikali Mkoani Kagera imevikopesha vikundi mbalimbali
vya maendeleo vya vijana kupitia Vyama Vya Kuweka Akiba na Kukopa
(SACCOS) zaidi ya shilingi milioni 83 katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita ili kuwawezesha vijana waweze kujiajiri wenyewe na kujikwamua kiuchumi .
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Fabian Massawe wakati akisoma taarifa fupi ya mkoa kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara aliyepo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Kanali Mstaafu Massawe alisema kuwa Serikali inasimamia
utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana kwa kuratibu shughuli za
mifuko ya vijana na kufuatilia utoaji na urejeshaji wa mikopo,
kuhamasisha vijana na kufufua moyo wa kujitolea na kukuza na kuendeleza
vipaji mbalimbali walivyonavyo vijana ili kuwawezesha kujiajiri kupitia
mafunzo yanayohusu stadi za kazi na maisha
“Changamoto tunazokabiliana nazo
katika kuwakopesha vijana ni mahitaji makubwa ya mkopo ukilinganisha na
uwezo wa SACCOS au wakopeshaji wengine, urejeshaji hafifu wa mikopo
kutoka kwa wakopaji, ukosefu wa ajira, uvivu na uzurulaji, vijana kutaka
mafanikio kwa haraka na matumizi ya madawa ya kulevya kwa baadhi ya vijana”, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aliendelea
kusema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali ngazi ya mkoa
inafuatilia kwa karibu ili kuona kwamba matamko ya sera ya Taifa ya
Maendeleo ya vijana yanazingatiwa na kuingizwa katika maendeleo
ya Halmashauri lengo kuu ni mkoa kuwa na vijana wenye ari ya kuwajibika
na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii, wazalendo, wenye
maadili na kupenda nchi yao.
Kwa
upande wake waziri Dk. Mukangara alisema kuwa hivi sasa Serikali
inaangalia uwezekano wa kuongea mkopo kwa SACCOS zinazolenga shughuli za
maendeleo ya vijana kutoka shilingi milioni tano hadi kumi kwani mahitaji ni makubwa na hayakidhi haja.
Dk. Mukangara alisema kuwa vijana watumie
fursa zinazowazunguka na kutambua kwamba ni wajibu wao na siyo jukumu
la wazazi kuwakumbusha umuhimu wa kufanya kazi kwani ni aibu kijana kula
chakula bila ya kukitolea jasho huku mzazi akihangaika kufanya kazi.
“Vijana watambue kuwa fursa ya kupata ajira ipo
katika kero zinazowazunguka hivyo basi uongozi wa Serikali mkoani humu
uwahamasishe vijana ili waweze kujiajiri na kuajiri kwani maendeleo ya
Kagera yanawategemea wao hakuna mtu mwingine atakayeleta maendeleo yao”,
alisema Waziri Dk. Mukangara.
Alimalizia
kwa kuwataka viongoziwa Serikali kuwafuatilia vijana kwa ukaribu katika
Kata na kuweza kuwafundisha na kuwashirikisha katika
miradi ya maendeleo ili waweze kusaidiana na jamii inayowazunguka kwa
kushiriki ulinzi shirikishi, kupambana na tatizo la uhamiaji haramu na
kufahamu umuhimu wa utii wa sheria.
Mkoa
wa Kagera unakadiriwa kuwa na idadi ya watu 2,739,492 kati ya hao
wanawake 1,386,669 na wanaume 1,353,123 ambapo vijana ni 903,608 wenye
umri wa miaka 15 hadi 35 sawa na asilimia 33 ya wakazi wote ambapo kati ya hao wa kike ni 459,867 na wa kiume 443,741
No comments:
Post a Comment