Ofisi yaTaifa ya
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali imeingia katika mfumo mpya wa mawasiliano
wa matumizi ya barua pepe na intraneti utakaoiwezesha ofisi hiyo kutuma
na kupokea taarifa za utendaji kwa haraka kufuatia kukamilika kwa mradi
wa kuunganishwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam wakati wa makabidhiano ya
mradi huo uliofanywa na kampuni ya Simu Tanzania, Mdhibiti na Mkaguzi
mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utouh amesema kuwa mradi huo
utaiwezesha ofisi yake kuimarisha mawasiliano ya ndani na nje ya ofisi
kupitia mfumo wa intaneti.
Amesema mradi
huo ambao kwa sasa umeanza kwa kuziunganisha ofisi 12 za mikoa
mbalimbali utaleta mabadiliko makubwa katika nyanja nzima ya upashanaji
habari na utawawezesha watumishi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu
za serikali kupata mawasiliano kwa kwa haraka na usalama zaidi kupitia
makao makuu ya ofisi hiyo.
Amesema mkongo
wa taifa utaiwezesha ofisi hiyo kumiliki na kudhibiti taarifa mbalimbali
zinazotumwa kwa kuwatumia wataalam wa Tehama wa ndani huku akibainisha
kuwa mfumo huo mpya utawazuia watumishi wa ofisi hiyo kutumia mifumo ya
kawaida ya barua pepe na mitandao hatarishi inayoweza kuleta madhara
kwenye taarifa muhimu za serkali.
" Mradi huu
umekamilika wakati muafaka kwa sababu utatuwezesha kupunguza gharama,
kumiliki na kudhibiti sisi wenyewe taarifa zetu za kiutendaji za kila
siku kupitia wataalam wa Tehama tulionao katika ofisi zetu na kuondoa
kabisa mfumo uliokuwepo wa kubeba taarifa mikononi kutoka eneo moja hadi
jingine" amesema Utouh.
Amefafanua kuwa kukamilika
kwa mradi huo kutaiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za
Serikali nchini kujenga uwezo wa uimarishaji wa miundombinu za shughuli
za Ukaguzi na utendaji na kurahisisha mawasiliano kwa kutumia mfumo wa
kompyuta huku akifafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za
Serikali Tanzania kwa kipindi cha miaka 6 ni wakaguzi wa Umoja wa
mataifa ukaguzi unaofanywa katika miji mbalimbali duniani.
Utouh
amebainisha kuwa ofisi yake sasa itaweza kufanya mikutano ya kiutawala
moja kwa moja na ofisi za mikoani kupitia mfumo mpya wa mawasiliano wa
mtandao (video conference) na kuwataka watumishi wa ofisi hiyo kuutumia
ipasavyo mfumo huo kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake
Meneja wa njia za mawasiliano ya nje wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL)
Bw. Kisamba Tambwe akikabidhi mradi huo amesema kuwa kampuni hiyo
imetekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa ili uweze kukidhi malengo
yaliyokusudiwa.
Amesema TTCL
itaendelea kuhakikisha kuwa ofisi 12 za mikoa iliyouganishwa kwenye
Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa zinakuwa na usambazaji salama wa taarifa
kutoka eneo moja hadi jingine.
No comments:
Post a Comment