Wananchi wa Kenya wakiwa kwenye foleni ya kupiga kura ya kuchagua Rais wa nchi hiyo
Wakenya wangali wanapiga kura licha ya muda wa mwisho
wa shughuli hiyo kutimia.Upigaji kura ulianza asubuhi na mapema baadhi
ya wagombea wakiwa katika vituo vya kupiga kura saa nane na saa tisa
usiku.
Mwandishi wa BBC Ann Mawathe anasema kuwa katika
kituo kimoja mjini Kisumu, bado mamia ya wapiga kura wamepiga foleni
wakisubiri kupiga kura.
Kulingana na tume ya uchaguzi mkuu,
kila mpiga kura ambaye angali kwenye foleni hata baaya ya muda
kukamilika, ataruhusiwa kupiga kura, lakini hakuna watu wataruhusiwa
kujiunga na foleni kupiga kura.
Baadhi ya vituo vya kupigia kura vimefunga rasmi shughuli ya kupiga kura baada ya muda wa mwisho wa shughuli hiyo kutimia.
Milolongo mirefu ilishuhudiwa katika sehemu
nyingi za nchi baadhi zikiwa hata karibu kilomita moja, ishara ya
walivyojitokeza wakenya kwa shughuli hiyo ambayo ni ya kihistoria.
Kuna hofu kuwa huenda shughuli hiyo ikaendelea hadi usiku kwani milolongo bado ni mirefu sana.
Kwa hili kuna taarifa kuwa baadhi ya wagombea wanapinga swala la kuendelea na shughuli ya kupiga kura kwa hofu ya wizi wa kura.
Usalama ulidhibitiwa kote nchini polisi
wakiwekwa katika sehemu mbali mbali, kuhakikisha wapiga kura wanaendelea
na shughuli katika mazingira salama.
Katika sehemu mbali mbali kulikuwa na visa vya
vurugu mfano mjini Mombasa ambako wanachama wa kundi la MRC
waliwashambulia polisi waliokuwa wanashika doria na kuwaua wanne.Pia
waliwaua raia kadhaa wasiokuwa na hatia.
Lengo la kundi hilo lilikuwa kuvuruga uchaguzi mjini Mombasa pwani ya Kenya.
Kundi hilo limekuwa likitaka uhuru wa jimbo hilo kwa madai kuwa wametengwa na serikali.
Magombea wa urais Raila Odinga aliwataka wananchi kustahimiliana pamoja na kuwapongeza kwa kupiga kura kwa utulivu.
Naye Uhuru Kenyatta alisikitika na matukio ya Mombasa na kuwambia wakenya kuwa watulivu pia.
Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza anasema kuwa
foleni mjini Nakuru zimeanza kupungua na huenda wapiga kura wakamaliza
shughuli hiyo itimiapo saa kumi na moja jioni muda wa mwisho wa kupiga
kura
Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa leo
usiku ingawa tume ya uchaguzi ina hadi siku saba kutoa matangazo ya
matokeo ya kura za urais.
No comments:
Post a Comment