Jeshi nchini Nigeria limesema
watu hamsini na watano wameuawa huko kaskazini mashariki mwa Nigeria
katika mashambulio yaliyofanywa na wanamgambo wa kundi la Boko Haram.
Taarifa zinasema, wafungwa 105 walitoroshwa katika shambulio hilo mapema alfajiri lililotokea katika jimbo la Bama, Borno.
Aidha, mashahidi na jeshi linasema kituo cha polisi cha Bama, majengo ya serikali na kambi za kijeshi ziliteketezwa kwa moto.
Habari zinasema, mashambulio ya makundi yenye
msimamo mkali ni ya kawaida katika jimbo hilo lakini kiwango cha
umwagaji damu kilichotokea katika shambulio la sasa ni cha kutisha.
Mwandishi wa BBC jijini Lagos, Will Ross,
anasema shambulio hilo linafuatia mashambulio mengine mabaya siku za
nyuma linakinzana na taarifa kwamba, operesheni za kijeshi dhidi ya
wanamgambo hao zimepunguza tishio la Boko Haram.
Rais Goodluck Jonathan ameunda kamati
itakayopitia masharti ya msamaha kwa waasi hao lakini kiongozi wa Boko
Haram, Abubakar Shekau, mpaka sasa amekataa wazo hilo.
Msemaji wa jeshi, Musa Sagir, aliyeko mji wa
Maiduguri takriban kilomita 70 kutoka Bama, amedai kuwa, shambulio hilo
siku ya Jumanne katika mji huo mdogo lilianza baada ya watu 200
wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Boko Haram wakiwa na silaha nzito kuwasili
katika mabasi na magari madogo saa 11 alfajiri.
Msemaji huyo ameliambia shirika la habari la AFP
kwamba, baadhi ya watu hao wenye silaha walishambulia kambi za jeshi
lakini walirudishwa ambapo kumi kati yao waliuawa na wawili kukamatwa.
Polisi pia wauwa
“Lakini watu hao walivamia gereza , na
kuwaachilia wafungwa 105, na kuwauwa walinzi wote wa gereza waliokuwa
nje isipokuwa wale waliojificha ndani ya stoo ya ya kuhifadhia vyombo
vya kupikia,” ameongeza.
Baadhi ya washambuliaji hao walivalia sare maalum za kijeshi na walishambulia kwa takriban saa tano.
Maafisa wa polisi 22, walinzi 14 wa gereza,
wanajeshi wawili na raia wane inasemekana wameuawa katika shambulio hilo
pamoja na wafuasi 13 wa Boko Haram.
Kamanda wa polisi wa Bama, Abubakar Sagir
amekaririwa akisema kuwa, miongoni mwa raia hao walikuwemo watoto watatu
na mwanamke mmoja.
Kama linavyofahamika, kundi la Boko Haram, lina
mizizi yake katika mkoa huo wa Nigeria. Linapigana kuipindua serikali
ili kuunda taida la Kiislamu.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, jeshi la Nigeria
lilianzisha mashambulizi ya kuwasaka wanamgambo hao katika majimbo ya
Baga na Borno, baada ya wapiganaji wa Boko Haram kushambulia msafara wa
kijeshi.
Watu wapatao 200 waliuawa katika msako huo na
maelfu ya majengo kuharibiwan hali iliyosababisha makundi ya kutetea
haki za binadamu kudai kuwa, jeshi lilitumia nguvu kupita kiasi. Jeshi
lilitangaza kuwa watu waliokufa walikuwa 37.
No comments:
Post a Comment