Na Lydia Churi, MAELEZO
Serikali
imetoa wito kwa watanzania kuhakikisha wanachangia ipasavyo katika
kutoa maoni juu ya rasimu ya katiba iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba nchini ili Tanzania ipate katiba itakayokidhi
matakwa ya wananchi.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ameyasema hayo leo jijini Dar es
salaam wakati akizindua Kitabu kiitwacho Mabadiliko ya Katiba na Hatima
ya Tanzania kilichoandikwa na Naibu Kamishna Jenerali wa Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji Tanzania Luteni Kanali Lidwino Mgumba.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo, Waziri Chikawe ameitaka Tume ya Mabadiliko ya
Katiba nchini kuhakikisha inawafikia wananchi wengi na kusikiliza maoni
yao juu ya rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume hiyo hivi karibuni.
Amesema
jukumu la Tume hiyo si kutetea rasimu yao ya Katiba bali ni kusikiliza
wananchi wana maoni gani juu ya rasimu hiyo. Aidha, Waziri huyo
aliwataka wajumbe wa mabaraza ya katiba kutumia nafasi waliyonayo ili
ipatikane katiba itakayowajali watanzania wote.
Waziri
Chikawe alimpongeza mtunzi wa kitabu hicho kwa kutumia Katiba kuandika
kitabu kwa kuwa ni suala nyeti. Aliongeza kuwa wananchi hawana budi
kuandika vitabu mbalimbali vinavyohusu mila na tamaduni za kitanzania
ili kuzihifadhi kwa kuwa zinatoweka.
Naye
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi alimpongeza
Mtunzi wa Kitabu hicho kwani amekiandika wakati muafaka huku akiwataka
watumishi wa Umma kutumia ujuzi walionao kuandika vitabu mbalimbali
vitakavyoelimisha Umma wa watanzania.
Awali
akizungumza kwenye uzinduzi huo, Luteni kanali Mgumba aliwasisitiza
watanzania kusoma kitabu chake ili wapate ufahamu wa masuala ya Katiba
na hatimaye washiriki vizuri katika mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Aidha
katika kuhakikisha wanafunzi wa shule za sekondari wanapata uelewa wa
masuala ya Katiba amegawa vitabu hivyo kwa wanafunzi waliopo kwenye
Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Nachingwea.
No comments:
Post a Comment