MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Thursday, November 7, 2013

MVUNGI APELEKWA AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU ZAIDI



 Dkt. Mugisha Clement Mazoko wa Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) (kushoto), Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Assaa Rashid (mwenye tai) na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia (wa pili kulia) pamoja na ndugu na jamaa wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi wakiangalia wakati Mjumbe huyo akipandishwa ndani ya ndege kusafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Dkt. Mvungi alivamiwa na kujeruhiwa na watu nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jumapili, Novemba 3, 2013.





Mke wa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi (kulia), pamoja na marafiki wakimuombea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana kabla hajasafirishwa kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia


 Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dkt. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) amesafirishwa leo (Alhamisi, Novemba 7, 2013) saa 5:45 asubuhi kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi.


 Akiwa nchini Afrika Kusini, Dkt. Mvungi atapata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg.
Itakumbukwa kuwa Dkt. Mvungi alivamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013. Tukio hilo la uvamizi linaendelea kuchunguzwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.


Tangu siku alipojeruhiwa, Dkt. Mvungi alikuwa akipata matibabu katika Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI). Hata hivyo, Madaktari waliokuwa wakimtibu MOI, walishauri afanyiwe uchunguzi na matibabu zaidi. 

Dkt. Mvungi ameondoka na ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Flightlink na ameambatana na Dkt. Mugisha Clement Mazoko kutoka MOI; Muuguzi Bi. Juliana Moshi; na mtoto wa kaka yake Bw. Deogratias Mwarabu. Serikali inagharamia gharama zote za matibabu ya Dkt. Mvungi.

Tume inawaomba wananchi wote waendelee kumuombea kwa Mungu Dkt. Mvungi ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida na hatimaye kuendelea majukumu yake.

No comments:

Post a Comment