MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Sunday, October 9, 2011

matembezi ya hisani ya Asasi ya Saratani ya Matiti

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Matiti ya Tanzania breast Cancer, Angela kuzilwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu matembezi ya hisani ya kuelimisha jamii kuhusu Saratani ya Matiti. Kulia ni Kisura wa mwaka 2010, Lethina Christopher

Meneja Mipango wa Taasisi ya Kansa ya Tanzania bleast Kisa Mwakatobe akifafanua jambo wakati wa Mkutano huo Dar es Salaam



TANZANIA BREAST CANCER FOUNDATION

PRESS RELEASE

OCTOBER MWEZI WA UFAHAMU WA SARATANI YA MATITI
9 OKTOBA 2011 – SOUTHERN SUN HOTEL


Mimi naitwa Angela Kuzilwa, nimegundulika nina saratani ya matiti mwaka 2004.  Saratani ya aina yoyote inahusishwa na kifo kwani hata mimi nilipoambiwa nilijua siku za maisha yangu ni fupi.  Nimepata upasuaji wa kuondolewa titi na kufanyiwa matibabu na leo nina ishi kwa matumaini nikifahamu kuwa kila mtu ana siku yake ya kufa.  Mimi ni mwanzilishi wa Asasi ya saratani ya matiti Tanzania.  Tulipoanza tulikuwa wanawake kumi lakini kwa bahati mbaya wenzetu nane wamekwisha tangulia mbele za Muumba.  Tumejifunza kutouliza kwa nini Mungu sisi ndio tumepata ugonjwa huu ila tumetambua kutumia ugonjwa huu kuifunza jamii ili waweze kuelewa na kuufahamu vizuri ili pindi watakapogundulika waweze kwenda hospitali mapema na kuwahi kupata matibabu.  Kwani saratani ya matiti ikigundulika mapema hutibika.

Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania (Tanzania Breast Cancer Foundation – TBCF) ni Chama cha hiari kisicho cha kiserikali na cha kujitegemea kilichoanzishwa na wanawake jasiri ambao wamegundulika na ugonjwa wa saratani ya matiti pamoja na wanawake wachache wa kujitolea.

Mwezi wa Oktoba huwa unajulikana kama MWEZI WA UFAHAMU WA SARATANI YA MATITI duniani kote.  Ugonjwa wa saratani ya matiti ni mojawapo ya magonjwa hatari yanayowapata wanawake wengi Tanzania ingawa inasemekana saratani ya kwanza ni ya shingo ya kizazi.

Wanawake wengi waliogundulika na saratani ya matiti wanakumbana na matatizo mengi sana; wengi wanagundulika wamechelewa; matibabu ni ghali sana na zaidi uelewa wa ugonjwa wa saratani ni mdogo sana Tanzania.
Tumegundua mpaka sasa msaada tunaotoa katika Asasi yetu ni mkubwa sana

Asasi yetu ya Saratani ya Matiti  inahamasisha wanawake wote vijana kwa wazee wazungumzie kuhusu ugonjwa huu kwa uwazi na pia wachukue jukumu la kulinda afya zao kwa kujifahamu na pale wanapoona tofauti yoyote katika matiti waende haraka hospitali kwa uchunguzi.

Asasi yetu imeandaa matembezi ya HISANI kwa ajili ya kuelimisha jamii ya Kitanzania kuhusiana na ugonjwa huu, na jinsi unavyoua kina mama na kina dada zetu kwa wingi kutokana na ufahamu na uelewa mdogo waliokuwa nao.

Vituo vya kujiandikisha ni Mlimani City, Milleum Towers, Shoppers Plaza na Woolworth ya mjini.  Siku ya matembezi watu wanatakiwa kuanza kujiandikisha kuanzia saa 12 mpaka saa moja asubuhi na  matembezi yataanzia rasimi kuanzia saa moja na nusu asubuhi na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja.  Tshirt zitatolewa siku ya matembezi.

Ugonjwa wa saratani ya matiti sio ugonjwa unaoleta madhara kwa wanawake tu,  bali watoto na familia wanapata kipigo kutokana na kumpoteza mama au dada.  Matembezi haya yataongeza ufahamu wa kutambua umuhimu wakufahamu dalili za ugonjwa huu na umuhimu wa kuwahi kwenda hospitali.  Imegundulika kuwa mwanamke akiwahi kugundulika mapema  na kupata matibabu sahihi ana nafasi ya kupona.

Asasi yetu inatoa msaada kwa wanawake waliogundulika na saratani ya matiti kwa:

·        kutoa matiti bandia na sidiria maalum
·        kuwatembelea wagonjwa hospitali na majumbani na kutoa msaada wa fedha na chakula.
·        kuitisha vikao vya wanawake waliogundulika na saratani ili kubadilishana mawazo na kisikia changamoto wanazokumbana nazo
·        kutoa ushauri nasaha kutokana na matibabu na matatizo yake

Asasi yetu hufanya kampeni za uelimishaji kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa wa saratani ya matiti kwa njia mbalimbali kama mikutano ya hadhara, warsha na semina.  Asasi inagawa vipeperushi vyenye ujumbe mbalimbali kuhusu saratani ya matiti.

Asasi ya saratani ya matiti ilifanya matembezi ya hisani mwaka jana tarehe 26 April 2010 na kufanikiwa kupata fedha taslimu Shs. 34,447,000.  Fedha zilitumika kwa kutoa huduma mbali mbali kwa wagonjwa wa saratani ya matiti.

Asasi yetu inazidi kupigana na ugonjwa huu kwa kuzidi kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya campaign ya ufahamu na uelewa wa ugonjwa wa saratani ya matiti katika shule za secondari.  Asasi inaamini kuwa kama wanafunzi wapata elimu ya kutosha itakuwa nirahisi kwa jamii kuelimika pia kwani wanafunzi ni waelewa kwa urahisi na kwa kuzingatia kuwa vijana ndiyo Taifa letu la kesho.

Asasi yetu kwa mwezi huu pia imeandaa Chakula cha Usiku tarehe 28 Oktoba 2011 kuchangia mfuko wa Asasi hii ili kuweza kufikisha malengo yake ya kuweza kueneza ufahamu na elimu ya saratani ya matiti kwa jamii ya Kitanzania.

Mwisho napenda kutoa shukurani zetu kwa mashirika na Asasi mbali mbali ambazo zimejitolea kutusaidia katika kufanikisha matembezi ya tarehe 23 Oktoba:

Kwanza kabisa ni Shirika la Susan G. Komen for the Cure kutoka United States of America. Katika matembezi wamesaidia kutoa sare ya siku ya matembezi. Pia walifadhili zoezi la kutoa elimu ya saratani ya matiti  shule za Secondary.  Mwaka huu tunategemea ujumbe mzito wa  watu wawili kutoka Susan G. Komen na mwingine kutoka George W. Bush Institute kujumuika nasi siku ya matembezi na pia kuwa na mazungumzo ya pamoja.

Foundation for Civil Society ambao tunaweza kusema ndio mhimili wetu mkubwa katika shughuli zote tunazofanya katika Asasi hii kwa kipindi cha miaka mitatu sasa.

Napenda kuwashukuru pia wafuatao:Twiga Cement kila mwaka wanaendelea kufadhili matembezi haya, Shear Illusions, PPF na Southern Sun.

Mwisho kwa kipekee ningependa kuwashukuru Beautiful Tanzanie Agency wa kiongozwa na Mkurugenzi wao Juliana Urio  kwa kutoa msaada mkubwa wa wafanyakazi wake kujumuika nasi katika matayarisho ya matembezi haya kwa mafanikio makubwa.

Nawashukuru sana waandishi wa habari  kwa  kufika kwenu leo na nimategemeo yetu mtakuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kuhusu saratani ya matiti kwa kutumia kalamu zenu na katika magazeti.

Ili uweze kujua yote yanayofanywa na Asasi yetu tafadhali wasiliana nasi kwa namba zifuatazo 0715-943484/0715-174586 na 0784-443484



No comments:

Post a Comment