MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Friday, August 31, 2012

Ratiba ya Ligi Kuu

 
 
 
 



LIGI KUU TANZANIA BARA 2012/2013
Michuano ya Ligi Kuu kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kwa msimu wa 2012/2013 itaanza Septemba 15 mwaka huu kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja tofauti.
 
Mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba vs African Lyon (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT vs Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto Africans vs Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).
 
Mzunguko wa kwanza (first round) utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye mzunguko huo mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa mechi kati ya Toto Africans vs Ruvu Shooting (Kirumba), Mgambo JKT vs African Lyon (Mkwakwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam Complex), Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Sokoine), Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh Amri Abeid Kaluta) na Polisi Morogoro vs Coastal Union (Jamhuri).
 
Endapo Simba na Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.
 
MECHI YA UFUNGUZI WA MSIMU WA LIGI 2012/2013
Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 kati ya bingwa mtetezi Simba na makamu bingwa Azam itachezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
SERENGETI BOYS KUJIPIMA KWA ASHANTI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyokuwa kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya itavunja rasmi kambi yake kesho (Jumamosi) kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ashanti United.
 
Mechi hiyo dhidi ya Ashanti United iliyoko daraja la kwanza itachezwa kuanzia saa 10 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh. 2,000.
 
Serengeti Boys ilikuwa Septemba 9 mwaka huu icheze na Kenya kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, lakini Kenya ikajitoa ambapo sasa itacheza na Misri katika raundi ya pili. Mechi ya kwanza itachezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 
Mwishoni mwa Septemba, Serengeti Boys itarejea tena kambini kujiandaa kuikabili Misri ambapo kabla inatarajia kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu itakayotangazwa baadaye.
 
MCHEZAJI WA MTIBWA SUGAR NAYE APATA ITC
Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) limetuma Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na Mtibwa Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.
 
ITC hiyo ilitumwa jana (Agosti 30 mwaka huu), hivyo kufanya wachezaji ambao ITC hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu. Dirisha la usajili wa wachezaji litafungwa rasmi Septemba 4 mwaka huu.
 
Wachezaji ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba. ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati wowote kwani tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeshaziomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa zikitakiwa kupatikana.

No comments:

Post a Comment