Serikali imeuagiza mfuko wa Bima ya Afya
kubadilisha mfumo wa vitambulisho vya Bima ya Afya ili kuongeza uthibiti wa
udanganyifu unaofanyika ndani ya
mfumo uliopo.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii Mhe. Dkt. Seif Seleman Rashidi alipokuwa akijibu swali
lililoulizwa na Mhe. Mariam Kisangi (CCM Viti Maalumu) na kuongeza kuwa Wizara
inafahamu udanganyifu unaofanyika hivyo inashirikiana na Mfuko wa
Bima ya Afya ili kuhakikisha udanganyifu huo una dhibitiwa.
Ubadilishaji wa mfumo huo pia umelenga katika
kubadilisha vitambulisho vya sasa ili kuwa na aina bora zaidi inayotumia
teknolojia mpya ya utambuzi na kuimarisha usimamizi wa huduma katika vituo
vilivyosajiliwa na Mfuko hasa vituo vikubwa vilivyopo Dar es Salaam.
Alisema baadhi ya wanachama wamekuwa sio
waaminifu kwa kuuza nafasi zao au kuingiza majirani badala ya kujaza wategemezi
wanaostahili kisheria .Aidha alisema wapo wanaoshirikiana na watoa huduma wasio
waaminifu na kuingiza watu wenye magonjwa sugu na yenye gharama kubwa na kutolea
mfano wa magonjwa ya saratani.
Naibu Waziri alisema kwa mfumo wa sasa eneo la
wategemezi linalenga wategemezi halisi wa wanachama kwa mujibu wa taratibu za
Utumishi wa Umma.
Hata hivyo alisema Mfuko huo uko makini katika
kuhakikisha unatoa huduma stahili kwa wateja wake na kwa wale walioandikishwa
kama wategemezi hadi pale utaratibu mpya utakapopitishwa rasmi .
Akieleza
manufaa ya mfuko huo alisema msingi mkubwa wa Bima ya Afya za Jamii ni kuwezesha
mwanachama kutibiwa kulingana na tatizo au ugonjwa unaomsumbua bila kujali
michango yake.
Alisema dhana ya bima ya afya imejengeka
katika misingi ya kuchangiana ,ambapo mwenye familia ndogo bila wategemezi
anawasaidia wenye familia kubwa . Mwenye mshahara mkubwa husaidia wenye
mishahara midogo na vijana wanawasaidia wazee.
Aidha Dkt.Seif alisema Wizara inasubiri
ushauri kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu suala hili na
inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa Bima ya Afya na utendaji
kazi wa vitambulisho hivyo.
No comments:
Post a Comment