Na
Lydia Churi, MAELEZO-DODOMA
Serikali imewataka wachimbaji wote wa madini
nchini wanaovamia maeneo ya wawekezaji wengine kuacha kufanya vitendo hivyo na
badala yake waendeleze maeneo wanayomiliki kwa mujibu wa sheria.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini)
Steven Masele alisema tabia ya uvamizi wa leseni kubwa za utafiti unatishia
nchi yetu kukosa miradi mikubwa ya migodi mipya katika siku za usoni.
Akijibu swali la msingi lililoulizwa na
mbunge wa Kishapu, Mheshimiwa Suleiman Nchambi aliyetaka kujua mpango wa
serikali kuwasaidia mitaji na nyenzo za kufanyia kazi wachimbaji wadogo Mhe.
Masele alisema serikali inatambua na kuthamini mchango wa wachimbaji hao katika
kuinua uchumi na pato la taifa pamoja na kutoa ajira kwa watanzania wengi.
Alisema inakadiriwa kuwa watanzania milioni
moja wanajishughulisha na kazi ya uchimbaji wa madini nchini na kutokana na
hilo serikali kuanzia mwaka wa fedha wa 2009/2010 ilianzisha mpango wa kutenga
fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo ili waweze kununua vifaa
bora vya uchimbaji na uongezaji thamani madini.
Amewashauri wachimbaji wadogo nchini
kuungana ili iwe rahisi kukopesheka kupitia utaratibu ulioandaliwa na serikali.
Aidha amewashauri wachimbaji wadogo kuomba mikopo kupitia taasisi nyingine za
kifedha kama vile benki na kuhakikisha wanatimiza vigezo vinavyotakiwa na
taasisi husika.
Akizungumzia vurugu zilizotokea jana baina
ya wachimbaji wadogo na STAMICO huko Buhemba mkoani Mara, Mhe. Masele amewataka
wananchi wa eneo hilo kuwa wavumilivu wakati serikali ikiangalia namna ya
kutatua tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment