MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Monday, May 20, 2013

WANASIASA WAASWA KUJIEPUSHA NA RUSHWA

Na Zawadi Msalla-MAELEZO DODOMA
Viongozi wa serikali na wanasiasa wametakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na mambo yanayoweza kuleta hisia za rushwa ili kuzuia mianya ya kutuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi,Ofis ya Rais (Utawala Bora) Mhe. Kept.George Mkuchika alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mh.David Silinde mbunge wa Mbozi Magharibi. Alisema zipo kesi nyingi zilizofunguliwa juu ya viongozi na wanasiasa ,tuhuma hizo huchunguzwa na vyombo husika na endapo tuhuma hizo huwa na ushahidi ndani yake wahusika hufikishwa mahakamani.
Waziri alisema hakuna takwimu zinazoonyesha kwa nambari idadi kamili ya watanzania wanaowatuhumu viongozi na wanasiasa wanaojihusisha na rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Alisisitiza kuwa tuhuma si kosa hivyo ni wajibu wa Serikali kufanyia kazi kwa umakini tuhuma zote zinazotolewa ili kuangalia ukweli wa tuhuma hizo.
“Tuhuma ni hisia ambazo lazima zithibitishwe vinginevyo si haki kutuhumu viongozi wa Serikali na wanasiasa bila kutoa ushahidi  wa kuthibitisha tuhuma hizo kwa kiwango kinachotakiwa na sheria za Nchi.Kiwango hicho ni kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka yoyote ya maana” Alisema Waziri.
Alitoa wito kwa viongozi wa Serikali kutumia rasilimali za Mamlaka kwa maslahi binafsi na kwamba wawe mfano bora wa uongozi. Aidha kwa yeyote anayetoa tuhuma awe na ushahidi wa kutosha na ushahidi huo utolewe katika vyombo vya upelelezi.

No comments:

Post a Comment