Na Lydia Churi, MAELEZO-DODOMA
Serikali imeridhia kutungwa kwa sheria ya
Kusimamia vyombo vya Habari ambapo muswada wa kutunga sheria hiyo utawasilishwa
bungeni hivi karibuni.
Akisoma hotuba ya bajeti ya Wizara yake
bungeni mjini Dodoma leo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt.
Fenella Mukangara alisema baada ya sheria hiyo kupitishwa na bunge, Wizara
itaanza kuandaa waraka wa mapendekezo ya kutunga sheria ya Haki ya kupata
Habari wakati serikali ikiendelea na utafiti ili kupata uzoefu kutoka nchi
mbalimbali zenye sheria hii.
Kwa mujibu wa Dkt. Mukangara kutungwa kwa
sheria ya kusimamima vyombo vya habari kutasaidia katika kuimarisha tasnia ya
habari nchini na kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zinazoikabili wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo likiwemo suala la mafunzo kwa waandishi wa
habari pamoja na mazingira duni ya kazi.
Katika hotuba yake Dkt. Mukangara alisema pia
Wizara yake imeazimia kutekeleza suala la uanzishwaji wa benki ya Vijana ya
Taifa katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Aliongeza kuwa Wizara pia itaboresha huduma ya
Mfuko wa Maendeleo ya mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana pamoja na
kuendelea kuzijengea uwezo SACCOS zinazotoa huduma kwa vijana.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
inaomba kuidhinishiwa bajeti ya jumla ya shilingi 21,328,045,000 ambapo kati ya fedha hizo, fedha za matumizi ya
kawaida ni 20,728,045,000 na fedha za miradi ya maendeleo ni shilingi
600,000,000.
No comments:
Post a Comment