Kocha
wa Taifa Stars, Kim Poulsen aksisitiza jambo wakati wa mkutano na
waandishi wa habari wa Tanzania, mjini Kampala jana kuhusu mechi ya leo
ya kufuzu kucheza michuano ya CHAN dhidi ya Uganda Cranes inayotarajiwa
kuchezwa kwenye Uwanja wa Namboole mjini humo. Wengine ni Kocha
Msaidizi, Sylvester Marsh (kulia) na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Boniface Wambura.
Wakati Taifa Stars inashuka dimbani kesho, Jumamosi dhidi ya
Uganda Cranes kutafuta tiketi ya kucheza fainali za CHAN mwakani, kocha wa
Stars, Kim Poulsen amesema kazi kubwa kesho ni kutangulia kufunga.
Taifa Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanajro Premium
Lager inaingia dimbani ikiwa nyuma kwa bao moja baada ya kufungwa na Cranes 1-0
wiki mbili zilizopita Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Kampala jana,
Poulsen alisema wachezaji wote wamejiandaa vizuri na licha ya kuwa ni mwezi
mgumu katika mpira kwani baadhi ya wachezaji wamefunga, wachezaji wamepania
kupata matokeo mazuri.
“Tunajua watanzania wengi walikataa tama au kupoteza
matumanini baada ya sisi kufungwa 1-0 lakini katika mpira haya yanaweza
kubadilika…tukifunga bao kesho litabadilisha kila kitu,” alisema Poulsen.
Alikiri kuwa mechi hii ya marudiano ni ngumu kwani Stars
itakuwa inacheza na timu bora Afrika Mashariki lakini lolote linaweza kutokea
ndani ya dakika 90 au zaidi za mchezo.
Alisema licha ya kuwakosa wachezaji Shomari Kapombe na
Mwinyi Kazimoto, maandalizi ni mazuri na hasa walipokuwa kambini Mwanza
wachezaji walionesha bidii sana katika mazoezi.
Alisema katika mechi ya kesho watajitahidi kutengeneza
nafasi nyingi na kufunga magoli. “Katika mazoezi yetu tumefanya mazoezi sana
katika ushambuliaji, kutengeneza nafasi na kufunga magoli,”alisema huku
akiongeza kuwa mabeki watahakikisha washambuliaji wa The Cranes hawapiti
kabisa.
Aliwataka watanzania wawe na imani na timu ya Taifa kwa
matokeo yoyote yatakayopatikana kesho kwani mpira ni safari na kukubali matokeo
ni sehemu ya mchezo.
“Wachezaji wana ari ya kupata ushindi ili waende CHAN
mwakani kwani hii itawapa nafasi nzuri ya kuonekana na vilabu kubwa duniani na
tayari tumeona jinsi watu wengi wametambua kuwa kuna wachezaji wazuri Tanzania….Kapombe
ameenda kwenye majaribio Uholanzi, Kyemba naye yuko njiani na nasikia Kazimoto
yuko Qatar..nawatakia kila la heri.” Alisema.
Poulsen alisema Jumatatu atazungumza na waandishi wa habari
kuhusu mipango ya muda mrefu ya Taifa Stars.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya
Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, ambaye Bia yake inadhamini Taifa
Stars alisema wao kama wadhamini wanawaomba watanzania wawe na imani na stars
na waiombee ifuzu mashindano ya CHAN.
“Sisi kama wadhamini tuna imani na timu yetu na tuna imani
watafanya maajabu katika mechi ya kesho ili wawape raha watanzania,” alisema
Kavishe.
Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya shilingi
bilioni 2 kwa mwaka kuidhamini timu ya Taifa kwa mkataba wa miaka mitano.
No comments:
Post a Comment