Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Jeshi la Polisi kuanzia sasa
halitahifadhi silaha za washabiki, na badala yake litawazuia kabisa
kuingia viwanjani wakati wa mechi.
Jeshi
la Polisi limekuwa likihifadhi silaha za washabiki wanaokwenda
viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya mechi kumalizika kwa vile
Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) zinakataza silaha viwanjani.
Wikiendi
iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi
lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa washabiki waliokwenda kushuhudia
mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile kati ya JKT Ruvu na Simba.
Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki.
Hivyo,
kwa washabiki wanaomiliki silaha hatawaruhusiwa kabisa kuingia
viwanjani, na badala yake tunawashauri kuzihifadhi huko wanakotoka kabla
ya kufika viwanjani.
Pia
tunatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona mwenzake akiwa na silaha
uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi la Polisi ili
aweze kuchukuliwa hatua.
SIMBA KUIVAA RUVU SHOOTING VPL
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka huu) kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio
katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed Theofil kutoka
Morogoro kuanzia saa 10 kamili jioni vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh.
15,000 na sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani kuanzia saa 4 asubuhi.
Mechi
nyingine za kesho ni JKT Ruvu itakayoumana na Kagera Sugar kwenye
Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Coastal Union ikiwa mwenyeji
wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ndiyo utakaotoa
fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya City kuoneshana ujuzi katika
kusaka pointi tatu.
Ligi
hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga
na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Mgambo
Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga.
FDL KUTIMUA VUMBI VIWANJA KUMI
Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) msimu ujao (2014/2015) inaendelea wikiendi hii (Jumamosi na
Jumapili) kwa kuzikutanisha timu 20 zitakazopambana katika viwanja kumi
tofauti.
Jumamosi
kutakuwa na mechi kati ya Green Warriors na Friends Rangers (Uwanja wa
Mabatini, Mlandizi), Kimondo na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Vwawa,
Mbozi), Mlale JKT na Mkamba Rangers (Uwanja wa Majimaji, Songea) na
Kurugenzi dhidi ya Polisi Morogoro (Uwanja wa Wambi, Mafinga).
Polisi
Dodoma na Stand United (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Toto Africans na
JKT Kanembwa (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mwadui na Polisi Mara
(Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Polisi Tabora na Pamba (Uwanja wa
Ali Hassan Mwinyi, Tabora).
Keshokutwa
(Jumapili) kutakuwa na mechi kati ya African Lyon na Transit Camp
(Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Villa Squad dhidi ya Polisi Dar es
Salaam (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam).
No comments:
Post a Comment