MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Thursday, February 6, 2014

WABUNGE WA BUNGE LA KATIBA WAATAHADHARISHWA

NA SHARIFA MARIRA, Dar

WABUNGE watakaoteuliwa kuingia kwenye bunge maalum la katiba, wametakiwa kuhakikisha wanajadili kwa makini mustakabali wa nchi na  vizazi vijavyo kwa kuzingatia masuala yanayoathiri vijana na jamii kama elimu, afya, ajira, uongozi na ushiriki wa vijana katika vyombo vya maamuzi.

Wito huo umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Muwezeshaji wa Mradi wa Kijana Wajibika unaoendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la Restless Development, Radhione Juma, wakati akizungumzia masuala ya katiba na namna vijana ambavyo wameshiriki katika mchakato wa rasimu ya pili ya katiba.

Alisema ni vyema Rais Jakaya Kikwete, akazingatia pia kuteua wawakilishi wa vijana katika  uteuzi wa wajumbe wa bunge maalumu la katiba ili kuwakilisha nguvu kazi ya taifa vijana ambao ni sehemu kubwa ya idadi ya Watanzania.

“Mradi wa ‘Kijana wajibika’ ni mradi ambao utatekelezwa chini ya shirika la Restless Development, kwa kutoa elimu ya kujitambua kwa vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa Katiba mpaka kukamilika kwake wakiwa na taarifa sahihi,” alisema Juma.

Alifafanua kuwa, Kuelekea bunge maalum la katiba Shirika hilo linaendelea kutoa elimu kwa vijana ili wawe na taarifa sahihi juu ya kile kinachoendelea kwenye mchakato wa katiba  mpya.

“Ni ukweli usiopingika kuwa mchakato wa Katiba Mpya  ni fursa pekee kwa  vijana  kushirikishwa katika utungaji wa Sera na kuchambua masuala ambayo ni muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu na jamii kwa ujumla,” alisema Juma.

Shirika hilo pia linawasaidia vijana kujihusisha na masuala ya Afya ya uzazi na haki, elimu ya uraia na ujasiriamali.


No comments:

Post a Comment