Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2013/2014 itakayochezwa kwa mkondo mmoja inaanza kutimua vumbi Mei 10 mwaka huu katika vituo vitatu vya timu tisa kila kimoja.
Timu itakayoongoza katika kila kituo cha ligi hiyo itakayomalizika Juni 2 mwaka huu ndiyo itakayopata tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa msimu ujao wa 2014/2015. Vituo hivyo ni Mbeya, Morogoro na Shinyanga.
Kituo cha Morogoro ambapo mechi zitachezwa Uwanja wa Jamhuri kitakuwa na timu za Abajalo FC ya Dar es Salaam, African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Mji Mkuu FC (Dodoma) Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na Pachoto FC (Mtwara).
Uwanja wa Sokoine ndiyo utakaotumika katika kituo cha Mbeya chenye timu za AFC ya Arusha, Magereza FC (Iringa), Mpanda United SC (Katavi), Njombe Mji FC (Njombe), Panone FC (Kilimanjaro), Tanzanite SC (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi (Rukwa) na Volcano FC (Morogoro).
Timu za Eleven Stars ya Kagera, Geita Veterans (Geita), JKT Rwamkoma FC (Mara), Mbao FC (Mwanza), Milambo SC (Tabora), Mvuvumwa FC (Kigoma), Simiyu United (Simiyu), Singida United (Singida) na Wenda FC (Mbeya) zitacheza katika kituo cha Shinyanga kwenye Uwanja wa Kambarage.
Orodha ya usajili wa wachezaji wa timu zote kwa ajili ya RCL imetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa na klabu zote za RCL, FDL na Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa ajili ya kipindi cha pingamizi ambacho kinamalizika Mei 4 mwaka huu.
Hata hivyo, katika usajili uliowasilishwa na baadhi ya klabu imebainika kuwa kuna wachezaji walioshiriki VPL, FDL na wale U20 za VPL waliocheza ligi msimu wa 2013/2014.
Kiongozi yeyote atakayebainika katika udanganyifu kwenye usajili huo, awe wa klabu au chama cha mpira wa miguu cha mkoa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni ikiwemo kufikishwa katika vyombo vya kimaadili vya TFF kwa hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment