Tuesday, June 21, 2011
Aliyewashambulia waandishi wa habari afungwa jela mwaka mmoja na kulipa faini ya 200, 000
Mkazi wa Kijiji cha Lupembe wilayani Njombe, akifungukiwa mlango wa Mahabusu na askari baada ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na faini ya Sh 200,000 kwa kosa la kuwashambulia waandishi wa habari mwaka 2009 wakiwa
Na Mwandishi Wetu,Njombe
Mkazi wa kijiji Igombora katika tarafa ya Lupembe wilayani Njombe Bw.Shoto
Shaban amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na kutakiwa kulipa faini ya
shilingi 200,000 baada ya kupatikana na hatia ya kushambulia waandishi wa habari,
julai 15 mwaka juzi.
Akisoma hukumu iliyochukua nusu saa hakimu Mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya
Njombe Bw.Obeididom Chanjarika alisema kulingana na ushahidi uliotolewa
mahakamani hapo pamoja na maelezo ya mshitakiwa mwenyewe mahakama imeona
mtuhumiwa alihusika moja kwa moja kutenda kosa hilo.
“Hakuna ubishi kuwa mashahidi (waandishi) walikuwepo katika eneo hilo siku ya
tukio, hakuna ubishi kuwa mashahidi walishambuliwa pia hakuna ubishi kuwa
mtuhumiwa siku hiyo alifika eneo la tukio hivyo mahakama inamtia hatiani
mshitakiwa kulingana na ushahidi uliotolewa” alisema hakimu Chanjarika.
Hakimu Chanjarika alisema mshitakiwa anatiwa hatiani kwa makosa mawili moja la
kumjeruhi shahidi namba 1 Bw.Peter Mtitu aliyemjeruhi kwa panga kosa
linaloangukia kifungu cha sheria na.225 na la pili ni la kushambulia mwili wa
Mwandishi Mussa Mkama linaloangukia kifungu na.228 cha sheria ya makosa ya
jinai.
Kabla ya kutoa adhabu hakimu alimtaka mshitakiwa kuomba huruma ya mahakama ili
asipewe adhabu kali,ambapo alisema yeye ni mjasiriamali ambaye anategemewa na
familia ya watu 25,pia afya yake si nzuri kutokana na kuugua vidonda vya tumbo
kwa muda mrefu.
Hata hivyo hakimu alimtaka mwendesha mashtaka ASP Andrew Mchome aelezee tabia ya
mshitakiwa iwapo ana historia ya makosa ya jinai na atoe ushauri wake ni adhabu
ya namna gani anastahili mshitakiwa huyo.
Akieleza mahakama PP Mchome alisema hilo ni kosa la kwanza kwa mshitakiwa lakini
akaiomba mahakama kumpa adhabu kali kwani watu aliowashambulia ni wanahabari
ambao wanamajukumu makuwa kitaifa hasa katika kuelimisha jamii kuhusu masuala
mabalimbali.
“Mheshimiwa hakimu kitendo alichofanya mshitakiwa kimekuwa kikikemewa hata na
viongozi wa kitaifa kuhusu watu kujichukulia sheria mkononi, pia alilenga
kuwazuia wanahabari kutekeleza kazi zao za kila siku hivyo naiomba mahakama impe
adhabu kali” alisisitiza Bw.Mchome.
Hukumu hiyo ilisikilizwa na wanahabari 4 walioshambuliwa siku hiyo ambao ni
Mussa Mkama,Carlos Mtoya,Dotto Mwaibale wote wakazi wa Dar es Salaam na Peter
Mtitu ambaye ni mkazi wa Njombe, ambao pia walitoa ushahidi wao mahakamani.
Wanahabari hao walikwenda katika kijiji hicho Julai 15,2009 kusikiliza kero ya
wakulima wanaolalamikia serikali kufunga kiwanda cha chai cha Lupembe kwa miaka
3 na wao kukosa sehemu ya kuuza chai yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment