MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Thursday, March 22, 2012

Tido Mhando Mkurugenzi Mwananchi Communication

BODI ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imemteua Mwandishi wa Habari Mkongwe barani Afrika, Tido Mhando kuwa Mkurugenzi mpya wa kampuni hiyo kuanzia jana.
 
Tirdo anajiunga na kampuni ya Mwananchi akichukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo aliyeondoka nchini baada ya kumaliza muda wake, Sam Shollei.
 
Akizungumza jana ofisini kwake, Tido alisema," Ninafurahi kujiunga na kampuni ya Mwananchi na nitatumia uzoefu wangu kuiinua kampuni kwa kuongeza kiwango cha weledi."
 
Kuhusu historia yake, Tido alisema alianza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1969 katika Redio Tanzania akiwa mtangazaji wa muziki na baadaye michezo hasa mpira wa miguu.
 
"Niliwahi kutangaza mpira katika nchi nyingi ikiwamo Uganda katika kombe la Chalenji mwaka 1973, mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Madola mwaka 1974 na nilikuwa nasafiri na timu ya Taifa Stars katika nchi kadhaa Nijeria, Sudan, Kenya na Malawi," alisema Tido na kuongeza:
 
Aliendelea," Mwaka 1976 nilichaguliwa kwenda kutangaza mashindano ya Olympic nchini Canada na mwaka 1978 nilienda kutangaza mashindano ya mpira ya nchi za Jumuiya za Madola nchini Canada kabla sijaenda nchini Kenya mwaka 1979 kutangaza mchezo wa Kenya Chalenji na timu ya Taifa, Taifa Stars."
 
Tido alisema baada ya mashindano hayo, alichukuliwa na kampuni ya High Fidelity Production Ltd ya nchini Kenya akiwa mtengenezaji vipindi  na baadaye kuanza kufanya kazi ya uandishi wa habari kwa kujitegemea akiyawakilisha mashirika ya BBC, VOA na Sauti ya Ujerumani.
 
"Nilikaa Kenya kwa miaka kumi kuanzia 1980 hadi 1990. Wakati huo mimi ndiye nilikuwa mwakilishi wa mashirika hayo katika nchi zote za Afrika Mashiriki na Kati. Moja ya habari maarufu niliyowahi kuifanya nikiwa Kenya, ni taarifa za kifo cha kutatanisha cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Robert Ouko mwaka 1990," alisema.
 
Tido alisema mwaka 1990 hadi 2007, alijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Uingereza (BBC) ambako alikuwa Mwafrika wa kwanza kuiongoza idhaa hiyo na kufanikiwa kuongeza idadi ya wasikilizaji wake kutoka Milioni saba hadi milioni 21 kwa juma.
 
"Ilipofika mwaka 2007 Rais Jakaya Kikwete alinifuata London-Uingereza na akaniomba nirudi nchini kuliongoza Shirika la Habari la Taifa TBC,"
 
"Ninafurahi kuja Mwananchi, kampuni kubwa ya habari nchini na nitatumia uzoefu wangu kutoa mchango wangu katika ukuza demokrasia ya kweli nchini kwa faida ya watanzania na taifa kwa ujumla," alisema.
 

No comments:

Post a Comment