MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Monday, July 9, 2012

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI, MHESHIMIWA SYLVESTER MHOJA KASULUMBAYI (MB) WIZARA YA MAJI KUHUSU MAPITIO YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013



Waziri Kivuli wa Maji Sabrina Sungura
HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI, MHESHIMIWA SYLVESTER MHOJA KASULUMBAYI (MB) WIZARA YA MAJI KUHUSU MAPITIO YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
1.   UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, mwanzo kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuweza kusimama hapa mbele yenu hivi sasa na kutoa maoni ya kambi ya upinzani kuhusiana na bajeti ya wizara ya ya maji kwa mwaka wa fedha 2012/2013, kwa mujibu wa kanuni za Bunge kanuni ya 99(7) toleo la mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru viongozi wetu. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe kwa imani kubwa kwetu na  kututeua  kuwa wasemaji wa wizara hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu; aidha nimshukuru , Mh. Zitto Zuberi Kabwe (Mb), Naibu Kiongozi  wa Upinzani na Mheshimiwa Tundu Lissu (Mb), Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Tunawashukuru kwa kutuongoza vema kutimiza majukumu yetu kwa wananchi wetu wote. Pia nawashukuru wote waliotoa mchango wao katika kuandaa hotuba hii muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo niwashukuru wananchi wa mkoa wa kigoma kwa ujumla kwa ushirikiano wanaotupatia katika kutimiza majukumu yetu sisi wabunge tutokao mkoani humo. Nasema asanteni sana nanina waahidi kuendelea kuwasemea juu ya kero zenu kwa kipindi chote nitakachokuwa  bungeni. Pia naishukuru familia yangu kwa ushirikiano wote wanaonipa kwa kipindi chote cha majukumu yangu na kwa wakati huu ambapo nafanya shughuli za uwakilishi wa wananchi bungeni. Nawakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa, nakupongeza wewe binafsi kuweza kuongoza vyema Bunge hili la Kumi lenye changamoto nyingi.

2.0 MAPITIO YA BAJETI YA MAENDELEO KWA MWAKA 2011/2012 NA MAPENDEKEZO KWA MWAKA 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Maji ni kuwa wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama ni asilimia 86 katika miji mikuu ya mikoa na asilimia 57.8 vijijini. Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam upatikanaji wa maji safi ni asilimia 55 tu. Taarifa hizi zinatia wasiwasi kwani nchi yetu ina rasilimali za maji za kutosha ila tatizo ni vipaumbele vyetu katika kutumia rasilimali zilizopo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Dar es Salaam hali hii haikubaliki kwani vyanzo vya maji kwa ajili ya jiji la Dar es Salaam vimepatikana na maji mengi chini ya ardhi yamegunduliwa kwenye maeneo ya Kimbiji na Mpera. Ila mpaka leo hii vyanzo hivi havijatumika kikamilifu katika kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuweza kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, Bunge liliidhinisha fedha za ndani kwa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kiasi cha shilingi bilioni 41.6 fedha za ndani, na   fedha za nje shilingi bilioni 387.1.  Kwa hali hii, ni dhahiri kuwa serikali imeamua kuachia jukumu la kutoa huduma ya maji kwa wananchi wake kwa kutegemea fedha za wafadhili na wahisani wa nje badala ya kutenga fedha za ndani za kutosha ili kuweza kuokoa wananchi ambao wanaathirika kutokana na kukosa maji safi na salama kutokana na miradi hii ya wafadhili kutokutekelezwa kwa wakati na mfano ni mradi wa maji wa Benki ya Dunia kila wilaya.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kutoa huduma za kijamii duniani kote ni kazi ya Serikali inayokusanya kodi. Kitendo cha Serikali kutegemea mashirika ya nje kugharamia huduma za kijamii kama maji kwa wananchi wetu si sahihi kwa sababu ama mashirika hayo huchelewesha misaada hiyo au misaada haiji kabisa, kwa mwaka 2011/2012 fedha za nje zilikuwa shilingi bilioni 387.1 wakati za ndani zilikuwa shilingi bilioni 41.6, mwaka huu 2012/2013 fedha za nje ni shilingi bilioni 325.7 za ndani ni shilingi bilioni 140.

Kambi ya Upinzani,  inaitaka serikali iondokane na utaratibu huu wa kutegemea wafadhili kwenye huduma muhimu kama ya maji; badala yake zitengwe fedha za ndani za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wananchi wetu wanapata maji safi na salama, na hasa ikizingatiwa kuwa kwa mujibu wa tafiti mbalimbali maji ndio yameonekana kuwa kero kuu kwa wananchi wetu .

Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kuwa mradi wa programu ya maji vijijini kwa mwaka 2011/2012 ulitengewa  jumla ya shilingi bilioni 50.8 wakati program ya maji safi na maji taka mijini ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 313.55.  

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha, 2012/2013, programu ya maji vijijini imetengewa  fedha za ndani jumla ya shilingi bilioni 9.6 na fedha za nje shilingi bilioni 27.2 na program ya maji safi na maji taka ni shilingi bilioni 126.8 za ndani na shilingi bilioni 245.2 fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, upangaji mipango na ugawaji wa raslimali fedha usiozingatia uwiano wa hali halisi ya mahitaji ni kosa kubwa ambalo litaendelea kukandamiza jamii ziishizo vijijini. Takwimu zinatuonyesha kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini (31,809,808) na ndio wenye shida kubwa ya maji ikilinganishwa na wale waishio mijini. (Chanzo; Randama ya Wizara ya Maji, mpango wa bajeti ya kwa mwaka 2012/2013)

Mheshimiwa Spika, pamoja na tatizo kubwa la maji mijini lakini hali ni mbaya zaidi vijijini na hili linathibitishwa na kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Mbunge Juma Nkamia kuwa kwa sasa wananchi kwenye moja ya vijiji vilivyopo jimboni mwake wanabadilishana kati ya debe la mahindi na ndoo ya maji. Hali hii haikubaliki kwa taifa ambalo lina vyanzo vya kutosha vya maji kama vile mito, maziwa na chemichemi nyingi za asili na za kutosha.

Kwa sababu hiyo basi, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali  kuanzia bajeti hii kuanza kuangalia ugawaji wa fedha kwa uwiano kati ya programu ya maji vijijini na programu ya maji safi na maji taka mijini ili kuwawezesha wananchi wa vijijini kupata huduma ya maji, kwani kwa hali ilivyo ni kuwa uwiano wa mgawanyo wa fedha za miradi ya maendeleo baina ya mijini na vijijini ni 1:10 .


3.0 HALI YA SEKTA YA MAJI
3.1 Uhaba wa Wataalamu wa Maji.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu zilizopo ni kuwa wataalamu wa maji waliopo wengi ni wale ambao walisomeshwa wakati wa miaka ya 70 wakati wa kutekeleza mpango kabambe wa maji wa miaka 20 , kwani Julai 1974, Chuo cha Maji kilianzishwa rasmi kikiwa na wanafunzi 30 na wakafuatiwa na wanafunzi wengine 60 mwezi Machi 1975.

Mheshimiwa Spika, kozi za wanafunzi zilikuwa ni Hydrolojia, Hydrojiolojia na Ujenzi na zilikuwa ni za miaka mitatu kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne. Kila aliyemaliza alipata stashahada ya Water Resources Engineering kwa fani hizo. Ilitarajiwa kuwa Chuo kingedahili wanafunzi 250 kila mwaka, lakini kiwango cha juu kilicho fikiwa ni wanafunzi 128 tu waliodahiliwa mwaka 1983.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi 129 walipelekwa nchini India kwa mafunzo ya Shahada ya Uhandisi wa Maji katika Chuo Kikuu cha Roorkee, chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden ikishirikiana na Serikali za India na Tanzania.
Mheshimiwa Spika, sekta ya maji imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa wataalam wa kutosha katika fani mbalimbali za masuala ya maji. Kwa sasa kwa mujibu wa taarifa za wizara ni kuwa mahitaji ya watalaam hao ni: Sekretariati ya Mikoa zinahitaji wataalam 63, wanatakiwa wahandisi 560 na mafundi sanifu katika fani za maji zaidi ya 1,700 katika ngazi za Halmashauri ya Wilaya. Kwa upande wa usimamizi wa rasilimali za maji, changamoto kubwa iliyopo ni kukosa wataalamu wa ngazi ya juu kutokana na wengi wao kumaliza kipindi chao cha utumishi kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu ni kwanini serikali iliamua kuachana na utaratibu wa kusomesha vijana wetu kwa kuwapa ufadhili haswa kwenye sekta ya maji ili kuiweza kukabiliana na changamoto hii. Aidha, tunataka kujua mwaka huu wa fedha wizara inajiandaa kusomesha vijana wangapi ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wataalamu hawa? Kwani taarifa zilizopo ni kuwa wengi wamestaafu na hakuna waliokuwa wameandaliwa kuchukua nafasi.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vya kutosha vya maji kuweza kutosheleza mahitaji ya watanzania wote kwa kipindi chote cha mwaka, vyanzo hivyo ni maji yaliyo juu ya uso wa ardhi na yaliyochini ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya maji kwa nchi yetu kwa takwimu za mwaka 2002 yalikadiriwa kuwa ni mita za ujazo milioni 5,142. Kati ya hizo kilimo kilitumia mita za ujazo milioni 4,624  (karibu asilimia 90 ya maji yote) kati ya ujazo huo, mita za ujazo milioni 4,417 zilitumika kwa umwagiliaji  na mita za ujazo milioni  207 kwa ajili ya mifugo,  kiasi kilichobaki cha mita za ujazo milioni  493 ndicho kilitumika kwa matumizi ya viwandani na majumbani.

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa maji umefikia mita za ujazo 304,443 kwa siku kwa mwaka 2011 japokuwa mahitaji ya maji ni mita za ujazo 468,051 kwa siku hii maana yake ni kuwa kuna upungufu wa uzalishaji wa maji kulingana na mahitaji ya kiasi kinachohitajika kwa matumizi kwa siku.

Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta ya maji katika pato la taifa kwa mwaka 2011 ulipungua na kuwa asilimia 0.3 kwa kulinganisha na asilimia 0.4 kwa mwaka 2010. Hii maana yake ni kwamba shughuli nyingi za uzalishaji zinazotegemea maji ili kutoa tija, zilishindwa kuzalisha kwa kadri ya uwezo wake kutokana na sababu mbalimbali nyingine zikiwa ni ukosefu wa mipango na mikakati thabiti.

Mheshimiwa Spika, mchango wa fedha za ndani katika bajeti ya maendeleo kwenye sekta ya maji   kwa kipindi cha miaka minne (2007 hadi 2011), takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2005/2006 mchango wa fedha za ndani kwenye bajeti ya maendeleo ya sekta ya maji ilikuwa 57% na mwaka 2008/2009 ikawa 33% na kwa bajeti ya 2011/2012 ilikuwa ni 10%. (Chanzo: taarifa ya utafiti wa umasikini na maendeleo ya binadamu ya mwaka 2011 uk wa 99).

Mheshimiwa Spika, kushuka huku kwa mchango wa Serikali kwenye fedha za maendeleo ya miradi ya maji maana yake ni kuwa jukumu la msingi la Serikali kuwahudumia wananchi wake katika kupata huduma za msingi na haswa maji linaelekea kuishinda Seriakali kadiri siku zinavyozidi kwenda, jambo hili linapelekea Serikali kukosa uhalali wa kuendelea kuongoza nchi hii kama inashindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi kama huu ile hali wakijua kuwa maji ni uhai na kama hakuna maji hakuna maisha.


Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kutoa sababu za kina na za kimsingi ni kwanini haitilii maanani upatikanaji wa maji na haswa kwa kutenga fedha zetu za ndani za kutosha kwa ajili ya kuhudumia wananchi wetu na kuondoa tatizo la akinamama kuhangaika usiku na mchana kutafuta maji na kuacha kufanya shughuli nyingine za kuongeza uzalishaji.

Aidha tunaitaka serikali kuwasilisha mpango mahususi wa kutatua kero ya maji haswa vijijini ili tuweze kupunguza umaskini kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, takwimu zinaonyesha kuwa hata fedha zinazotolewa na wadau wa maendeleo toka nje katika kutekeleza program ya maendelelo ya sekta ya maji (WSDP) kwa mwaka 2011 hadi juni takribani asilimia 62 ya fedha zote walizoahidi zilikuwa zimetolewa kwa ajili ya kutoa usawia wa miradi ya maji nchini kote.

Mheshimiwa Spika, tafiti mbalimbali zinaonyesha kutokuwepo kwa usawa kwa Serikali katika ugawaji wa fedha hizo kwa miradi ya maji safi na salama kati ya maeneo ya mijini na vijijini. Na hii ni kutokana na ukweli kuwa Mgawo kwa maeneo ya vijijini ni asilimia 36 ya fedha zote na maeneo ya mijini ni asilimia 64 ya fedha zilizotolewa.

Mheshimiwa Spika, hii maana yake ni kuwa kila shilingi mia moja zilizotolewa na wafadhili kwa ajili ya miradi ya maji maeneo ya vijijini yalipata mgawo wa shilingi 36 ile hali maeneo ya mijini walipewa mgawo wa shilingi 64. Hii ni pamoja na ukweli kwamba katika nchi yetu watanzania waishio vijijini ni takribani asilimia 77.

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi kuhusiana na fedha zilizotengwa sio njema na haswa kutokana na ukweli kuwa Wananchi wengi waishio katika mikoa yenye ukame ni wafugaji na asilimia kubwa ya mifugo ipo vijijini. Mifugo hiyo inahitaji maji ya kunywa ya wastani wa lita 25 kwa ng’ombe wa kawaida kwa siku. Ili kuhakikisha kuwa mifugo inapata maji ipasavyo, Sera ya Maji inaelekeza kujenga mabwawa makubwa na madogo au kuchimba visima virefu na vifupi katika maeneo ya wafugaji na usanifu wa miradi yote ya maji vijijini uzingatie mahitaji ya mifugo.

Kambi ya Upinzani tunahoji kutokana na mgawo wa aina hii ni lini tatizo la maji vijijini litamalizika? Kuna mkakati gani wa kumaliza tatizo la maji vijijini?

3.2 Matumizi Bora ya Rasilimali za Maji.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria inayolinda raslimali za maji, inayohusu Usimamizi wa Rasilimali za Maji [The Water Resources Management Act] Na. 11 ya Mwaka 2009 inahusika na usimamizi wa rasilimali za maji - vyanzo vya maji juu na chini ya ardhi. Imetungwa na Bunge tar 28/4/2009, imesainiwa na Mhe. Rais tar 12/5/2009 na kuanza kutumika rasmi tar 1/8/2009 baada ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GN 235 LA 10/7/2009).3

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha sheria utunzaji wa Raslimali za maji, matumizi ya Maji Chini ya Ardhi kinasema kuwa Endapo katika ardhi anayoishi mtu kihalali yatapatikana Maji chini ya ardhi, ataruhusiwa kujenga kisima cha mkono kwa ajili ya kutumia Maji kwa matumizi ya nyumbani bila kuwa na kibali cha kutumia Maji kwa viwango vya uchimbaji vitakavyotangazwa katika kanuni zinazoidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya Maji”.

Mheshimiwa Spika, aidha, kifungu cha 54 (1) kinasema kuwa “Mtu yeyote anayetarajia kujenga, kuchimba, kuongeza ukubwa au kina cha kisima katika eneo lililotangazwa kuwa la hifadhi ya maji chini ya ardhi anapaswa aombe kibali cha maji chini ya ardhi .Maombi ya Kibali cha Maji ya Chini ya Ardhi yatachukuliwa kama ni maombi ya matumizi ya maji yatakayochukuliwa kutoka kwenye kisima husika na kwamba Bodi ya Maji ya Bonde ina mamlaka ya kufanya ukaguzi, kifungu. 54(2) na (3)]”.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa vipo viwanda na makampuni mbalimbali ambao wameamua kuchimba visima virefu na vifupi kwa ajili ya kupata maji kwa matumizi ya shughuli mbalimbali kwenye viwanda na Makampuni husika.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze watanzania ni kwa vipi inathibiti matumizi ya maji ya chini ya ardhi na kupata mapato stahiki kutoka kwenye  viwanda vikubwa kama vile kiwanda cha bia, kiwanda cha sigara, kiwanda cha kibuku, kiwanda cha cement, kiwanda cha mafuta ya kupikia, viwanda cha nguo, n.k

Mheshimiwa Spika, viwanda vyote tajwa hapo juu vimechimba visima vya maji kwa ajili ya matumizi ya viwanda vyao, na wachimbaji wa visima binafsi wanaongezeka kwa kadri mahitaji ya maji kwa matumizi ya majumbani na viwandani yanavyozidi kuwa shida, hasa maeneo ya mijini. (chanzo; Drilling and Dam Construction Agency, 2001).

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kufuatilia kwa makini uchimbaji huu wa visima na kuhakikisha kuwa fedha ambazo wamiliki binafsi wa visima wanatakiwa kulipa walipe na visima hivyo viwe chini ya uangalizi wa mamlaka husika kwa lengo la kuzia usababishwaji visima hivyo vya maji safi na salama kutokubadilika na kuwa na maji yasiyokuwa na ubora kwa mujibu wa sheria na viwango vya kimataifa.

3.3 Upatikanaji wa Maji na Matumizi yake.
Mheshimiwa Spika, maji yatokayo ardhini kwa matumizi ya nyumbani kwa maeneo yote ya mijini na vijijini  yanakadiriwa kuwa ni mita za ujazo 755,000 kwa siku(60% ya matumizi yote), wakati mahitaji ni ni mita za ujazo milioni 0.8 hadi 3.4 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, umwagiliaji kwenye mashamba ya miwa, maua, matunda, hutumia  mita za ujazo 130,000 kwa siku (10%), wakati matuzi ya viwandani na migodini hutumia takribani mita za ujazo 30,000 kwa siku(2%). Mifugo na matumizi mengine kama vile ufugaji wa samaki kwenye maeneo yasiyo na maji hutumia mita za ujazo 350,000 kwa siku (28%). Matumizi ya jumla kwa maji yatokayo ardhini  yanakadiriwa kuwa ni mita za ujazo milioni 1.265 kwa siku, ambayo ni sawa na asilimia 12 ya rasilimali yote ya maji ya ardhini ya mita za ujazo milion 11 kwa siku.

 Mheshimiwa Spika, matumizi ya maji ya ardhini kwa uzalishaji viwandani yamejikita zaidi kwa maeneo ya mijini, hasa Dar es Salaam, ambapo takribani 80% ya viwanda vyote nchini vipo.
Matumizi haya ya maji ya ardhini kwa viwanda yanatokana na kushindwa kwa mamlaka inayotoa huduma hiyo kwa mkoa wa Dar es Salaam kutoa maji ya kutosha kwa ajili ya viwanda.
 (chanzo, Taarifa ya  Utafiti  wa Dr. Josephat Kashaigili wa SUA  kwa INTERNATIONAL WATER MANAGEMENT INSTITUTE –IWMI Desemba 2010)

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kiasi gani cha fedha kinashindwa kukusanywa kutokana na viwanda kuchimba visima vyao binafsi na hivyo kuacha kutumia maji ya DAWASCO? Je, matumizi ya maji haya yanayofanywa na viwanda ni endelevu kwa sekta ya maji?
         
3.4 Huduma za Maji Mijini na Vijijini
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2011 sekta ya maji ilishuka kwa kiwango cha asilimia 4.0 ikilinganishwa na asilimia 6.3 mwaka 2010. Hata hivyo, mchango wa shughuli za usambazaji maji katika pato la taifa ulipungua kutoka asilimia 0.4 mwaka 2010 hadi asilimia 0.3 mwaka 2011.

Mheshimiwa Spika, taarifa ya hali ya uchumi  wa taifa kwa mwaka 2011 sura ya 18 uk. wa 245 inaonyesha kuwa uzalishaji wa maji mijini kwa mwaka 2011 ulipungua hadi kufikia mita za ujazo milioni 116.45 kutoka mita za ujazo milion 116.55 kwa mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kabisa kuwa upungufu huu unasababishwa na kuwepo kwa miundombinu chakavu kwa ajili ya usambazaji wa maji mijini na hasa kutokana na kukaa muda mrefu bila kufanyiwa matengenezo au ukarabati na hivyo kusababisha upotevu mwingi wa maji .

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa za serikali ni kuwa Mamlaka za Majisafi na Majitaka katika miji mikuu ya mikoa hutoa huduma ya maji bila gharama kwa kaya zisizokuwa na uwezo kwa kuzisaidia lita 160 kwa siku sawa na lita 5,000 kwa mwezi.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya maji kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru inaonyesha kuwa hadi sasa jumla ya kaya 1,466 zinapata huduma ya maji bure kutoka Mamlaka za maji katika miji mbalimbali hapa nchini.

Kambi ya Upinzani, inataka kupata majibu kuhusiana na masuala yafuatayo:
i.                    Je, ni katika miji gani huduma hii hutolewa na ni utaratibu gani unaotumika katika kuzitambua kaya hizo?
ii.                  Je, ni utaratibu gani unaopaswa kufuatwa na kaya husika ili wananchi waweze kufuatilia na kupata huduma hii?
iii.                Je. ni kwa nini kaya masikini za vijijini zinasahaulika kutokana na kukosekana kwa utaratibu kama huu na ikizingatiwa kuwa kiwango cha umaskini ni kikubwa zaidi vijijini kuliko mijini ?.

3.5 Mradi wa maji wa visima virefu Kimbiji na Mpera.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka uliopita Serikali ililieleza Bunge kuwa tayari  imekwishatoa fidia kwa wananchi kwa maeneo ya kuchimba visima virefu 20  vya uzalishaji wa maji  wa kutoa mita za ujazo  260,000 kwa siku, kwenye maeneo ya Kimbiji na Mpera kwa ajili ya kusambaza maji Jiji la Dar Es Salaam.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwa mwaka wa fedha uliopita 2011/2012 mpango huo ulitakiwa kutengewa kiasi cha shilingi. bilion 22.4, na mwaka huu wa fedha 2012/2013 mradi huo ulitakiwa kutengewa kiasi cha shilingi. bilioni 39.2.
Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo kwenye randama zinaonyesha kuwa bajeti iliyopangwa kwa mradi huo kwa mwaka huu wa fedha ni Tshs. Billioni 1 kama fedha za ndani na Tshs. Billioni 29.992 kama fedha za nje. Tofauti ya fedha zilizopangwa katika mpango wa miaka mitano kwa mradi huo na bajeti iliyotengwa ni Tshs.Billioni 9.208.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kuwa tofauti hiyo ni kubwa kiasi kwamba inaweza kukwamisha utekelezaji wa mradi huu na ni kinyume cha utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano na hivyo wananchi watachelewa kupata huduma ya maji safi katika Jiji la Dar es Salaam.
Aidha, fedha nyingi zilizotengwa ni fedha za nje na kwa uzoefu wetu katika miradi mbalimbali iliyokuwa inategemea fedha kutoka nje imekwama kukamilika kwa muda mrefu sana.

3.6 Mradi wa Maji Bwawa la Kidunda
Mheshimiwa Spika, Serikali haionyeshi kuwa ina nia ya dhati ya kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa na Bunge hili kwani Mpango wa maendeleo unaelekeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha zitengwe shilingi billioni 46 kwa ajili ya mradi huu lakini kwa mwaka huu wa fedha Serikali imetenga shilingi Bilioni 3.398 fedha za ndani na shilingi bilion 1.824 fedha za nje.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunataka maelezo ya kina kuhusiana na mradi huu na haswa ikizingatiwa kuwa fedha zinazopaswa kutengwa ni nyingi ila zilizotengwa ni kidogo sana , na ni dhahiri kuwa serikali haina nia ya dhati ya kuutekeleza mradi huu.
Na hii ni kutokana na ukweli kuwa jumla ya mabwawa 568 tu yalijengwa sehemu mbalimbali nchini tangu Uhuru mpaka mwaka 2011.

4.0 MAJI JIJI LA DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Dar es Salam unapata maji kutoka mito na visima kwa matumizi ya nyumbani, viwanda, bustani, mifugo, usafi na mazingira. Eneo kubwa linalopata maji linahudumiwa na Kampuni ya DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage Company). Maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, taasisi na watu binafsi.   
Mheshimiwa Spika, vyanzo vikuu vya maji ni mitambo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini, Mtoni na visima virefu 1,100 na vifupi 238 vilivyopo katika mkoa. Vyanzo vyote hivi huzalisha lita milioni 353 kwa siku wakati Jiji lina mahitaji ya lita milioni 469.3 kwa siku, ambapo ni sawa na upungufu wa lita milioni 116 kwa siku. Aidha kuna maji ambayo yanapotea wakati wa usambazaji yakiwa njiani kutokana na uchakavu wa mitambo na miundombinu.
Mheshimiwa Spika, changamoto zinazoathiri utoaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ni pamoja na uzalishaji mdogo wa maji ukilinganisha na mahitaji, uhaba wa vyanzo vya maji, ubadhirifu, uwezo mdogo wa watumia maji kulipia gharama, na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji maji ambayo husababisha upotevu mkubwa sana wa maji.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hizo jiji huwa na ukosefu mkubwa wa maji na kitaifa ni jiji la mwisho kwa upatikanaji wa maji hapa nchini kwani ni asilimia 55 tu ya wakazi wa Jiji ambao wanapata maji ikilinganishwa na Majiji na Miji mingine nchini ambayo wastani wake ni asilimia 75.
Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji.
Mheshimiwa Spika, majukumu ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam yanahusu pia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) ambayo ni mmiliki, mkodishaji na msimamizi wa utoaji wa huduma ya majisafi na maji taka katika jiji la Dar es salaam kwenye wajibu wa kupanga na kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuiendeleza na kugharamia matengenezo ya dharura na makubwa.
Kambi ya upinzani, tunaitaka serikali kutoa majibu kuhusiana na mambo yafuatayo:
i.                    Kuna mkakati gani wa kuhakikisha kuwa maji yanapatikana kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na hasa kwenye maeneo ya ujenzi wa makazi mapya kama vile Kimara, Changanyikeni, Msakuzi, Mbezi, Kigamboni, Kilungule, Tabata, Kinyerezi na kwingineko?
ii.                  Kuna mpango gani wa kuhakikisha kuwa maji yanayozalishwa hayapotei yakiwa njiani na hasa kutokana na uchakavu wa miundombinu ya maji?
iii.                Wizara itakamilisha lini miradi ya maji iliyopangwa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la upatikanaji wa maji Jijini?
iv.              Serikali iwasilishe bungeni Mpango Maalum wa kuboresha huduma za Majisafi na uondoaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 kwa ajili ya kuidhinishwa, kutengewa bajeti ya utekelezaji wa haraka katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kusimamiwa.
v.                Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulianza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 24 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kuwa Oktoba 2012 katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa.
vi.              Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.
vii.             EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali. Aidha, EWURA iharakishe kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.
viii.          Serikali ieleze imefikia hatua gani katika kutekeleza mapendekezo ya taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012.

Mheshimiwa Spika, katika Jiji la Dar es Salaam miaka ya hivi karibuni kumejitokeza na kushamiri tabia ya wananchi kuharibu na kuiba miundombinu ya miradi ya maji na kuiuza kama chuma chakavu. Vifaa vinavyoibwa sana ni mifuniko ya mashimo ya maji taka, mabomba ya maji, mita za maji na vifaa vinginevyo.
Kambi ya Upinzani, inaamini kuwa serikali inafahamu kunakouzwa vyuma hivi chakavu kwa kuwa ndio imetoa leseni kwa biashara hii. Tunaitaka kuwachukulia hatua wale wote ambao wanafanya biashara hii ya kuhujumu miundombinu yetu ya maji.

Mheshimiwa Spika, huduma ya uondoaji wa majitaka jijjini Dar es Salaam si ya kuridhisha kutokana na uwekezaji mdogo unaofanywa na Serikali katika eneo hili. Hadi sasa ni asilimia 18 tu ya wakazi mijini ndio wameunganishwa kwenye huduma hii. Jambo hili limewafanya wakazi wengi wa mijini kutumia vyoo vya mashimo, makaro (septic tanks) na vyoo vya shimo ambavyo huchangia uchafuzi wa maji yaliyoko chini ya ardhi.
Kambi ya Upinzani, tunaitaka serikali kuhakikisha kuwa inawekeza vya kutosha ili kuweza kukabiliana na hali hii na hasa ikizingatiwa kuwa kama hatua zitachelewa kuchukuliwa uchafuzi huu utaendelea kuathiri wananchi kiafya.



4.1. Mtandao wa Maji Safi na Maji Taka katika Jiji la Dar es salaam:
Mheshimiwa Spika, uchakavu wa miundombinu kutokana na mabomba kutokarabatiwa ipasavyo pamoja na uharibifu katika mitandao ya maji wa kujiunganishia kinyemela na kiholela umesababisha ongezeko kubwa la upotevu wa maji mpaka kufikia kati ya asilimia 40 hadi 45.

Mheshimiwa Spika, hali hii imesababisha ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo wanaonunua maji kwa madumu hununua bei ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata huduma ya maji ya bomba.

Mheshimiwa Spika, mtandao wa uondoaji wa maji taka ni chini ya asilimia 10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa licha ya ongezeko kubwa la watu. Kampuni ya Majisafi na Majitaka (DAWASCO) ambaye ni mwendeshaji mwenye wajibu wa kuendesha shughuli za kutoa huduma ya maji, kutoa ankara kwa wateja, kukusanya maduhuli, kutekeleza matengenezo makubwa yanayogharamiwa na DAWASA na kutekeleza uunganishaji wa maji kwa wateja wapya kwa kutumia mfuko wa maji. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali iongeze mtandao wa maji safi na maji taka hasa kwa maeneo mapya kama tulivyoyataja hapo juu.

5.0.  PROGRAMU YA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu miradi inayochangiwa na nchi wahisani iliyotolewa Juni 2011, sura ya 3 Uk. wa 13-15 inaonyesha fedha zilizotolewa na  Serikali  pamoja na  nchi washirika wa Maendeleo zilikuwa jumla ya shilingi 226,913,350,139 kwa ajili ya miradi ya maji. Aidha katika Programu hiyo ilikuwa na bakaa ya shilingi 68,332,741,760 na hivyo kufanya mwaka huo wa fedha kuwa na Jumla ya shilingi 295,246,091,899 na Hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha kulikuwa na fedha zisizotumika kiasi cha shilingi 72,582,156,680.

Mheshimiwa Spika,  hadi kufikia 30Juni, 2011 vitabu vya Halmashauri mbalimbali vilikuwa vinaonyesha kuwa kiasi cha shilingi 32,240,623,989.47 zilikuwa kama bakaa ambayo ilikuwa ni sawa na 58% ya fedha za miradi ya maji, Kwa maoni ya Mkaguzi kiasi hiki kikubwa ni kutokana na kushindwa kwa Halimashauri kutekeleza miradi ya maji kwa mujibu wa mipango.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze ni kwanini fedha hizi zinashindwa kutumika wakati tatizo la maji ni kubwa mno kwa wananchi. Mfano ni halimashauri ya Wilaya ya Mbozi ambayo miaka yote toka enzi za (Mhe Simpasa, Luka Siyame,na sasa Mhe.Godfrey Zambi na mhe.David Silinde) imekuwa na tatizo kubwa la maji, lakini takwimu zinaonyesha kuwa Halimashauri ilishindwa kutekeleza mpango wake wa miradi ya maji na mwisho wa mwaka wa fedha ilibakiza fedha za miradi ya maji kiasi cha shilingi milioni 865.7. Hizi ni fedha nyingi kwa wananchi ambao wanatatizo la maji.

Mheshimiwa Spika, Tatizo kama hili lilizikumba Halimashauri za Wilaya Karagwe, Kondoa, Musoma, Mbeya Vijijini, Ngorongoro, Iringa, Meatu, Temeke na Ilala ambazo ziliacha kiasi kikubwa sana cha fedha bila kutumika. Aidha Halimashauri ya Wilaya ya Iramba ilishindwa kutekeleza miradi ya maji kwa kipindi hicho na kubakiza fedha kiasi cha shilingi 894,376,237.15
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa hizi ni dhahiri kuwa miradi mingi ya Maji imekuwa ikishindwa kutekelezwa na fedha nyingi kubakia bila kutumika ile hali wananchi wetu wakiteseka kutafuta huduma za maji. (chanzo: taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, ukaguzi wa miradi inayochangiwa na wafadhili-(donor funded projects) ya 30 Juni, 2011)

Kambi ya upinzani, tunataka maelezo ya kina kuhusiana na fedha hizi kutokutumika ni sababu gani zilipelekea hali hiyo kujitokeza? Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa miradi hii inatekelezwa?

6.0 MIGOGORO YA MAJI
6.1  Mgogoro wa wananchi na Mamlaka za Maji Mbalizi.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na taarifa mbalimbali za migogoro baina ya wananchi na wakala mbalimbali wa usambazaji maji kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini , na hali hiyo imetokana na ama wananchi kutokuhusishwa kwenye kupanga bei mpya za maji au huduma kuwa chini ya kiwango ile hali wananchi wakiwa wanapaswa kulipia huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 29/10/2011, Wananchi wa Mbalizi walifunga Ofisi za Mamlaka ya Majisafi Mbalizi kutokana na   huduma wanayopata ni duni, vilevile mradi wa maji ni wao na hivyo walipaswa kuuendesha mradi wao  wenyewe, bei ya maji ya shilingi 10,000 kwa mwezi ni kubwa na walitaka ipungue hadi shilingi 7,000 kwa mwezi  na Meneja wa Mamlaka pamoja na Mafundi hawatakiwi kuonekana Ofisini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na madai ya wananchi hawa kuwa sahihi Mkuu wa Wilaya aliitisha mkutano wa hadhara mnamo tarehe 09.11.2011 na kuzungumza na wananchi hao lakini walimueleza wazi kuwa hawatakuwa tayari kufungua ofisi kama madai yao ya msingi hayatapata ufumbuzi, na hadi anaondoka kwenye mkutano huo walikuwa hawajakubaliana .

Mheshimiwa Spika, wananchi walikubali kufungua ofisi hizo mnamo tarehe 17.11.2011 na hii ni baada ya  madai yao kukubaliwa ikiwemo Meneja wa Mamlaka aliyekuwepo kuhamishiwa Kituo chake cha awali cha kazi Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na  baadhi ya mafundi waliokuwa wanalalamikiwa kusimamishwa kazi na bodi mpya ya mamlaka kuundwa ikiwa na wajumbe saba.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mtafaruku huu uliipelekea Mamlaka ya maji Mbeya kuzuia huduma ya maji kwa wananchi wa Mbalizi na hivyo kuwafanya wananchi kukosa huduma ya maji kwa muda mrefu tangu mwezi Oktoba 2011 hadi mwezi Juni mwaka huu ilikuwa haijarejeshwa.
Aidha tunataka kujua hatua zilizochukuliwa dhidi ya meneja na mafundi wote ambao walikuwa wanalalamikiwa na wananchi , na ni lini huduma hii ya maji itarejeshwa katika mji wa Mbalizi?

6.2.  Mgogoro baina ya wananchi na Mamlaka ya Maji Manispaa Kigoma.
Mheshimiwa Spika, mkoa wa Kigoma unatoa huduma ya maji kwa kutumia teknolojia mbalimbali, kwa mfano kusukuma maji kwa mashine, chemichemi, skimu za maji ya mtiririko, visima vifupi na virefu vyenye pampu za mkono, pamoja na uvunaji maji ya mvua.

Mheshimiwa Spika, ukosekanaji wa mita hususani kwa wakazi wa manispaa ya Kigoma ujiji, mamlaka ya maji mkoani  Kigoma imeshindwa kutekeleza kabisa maagizo ya ewura ya kutaka wananchi wapewe mita ili waweze kujua wanatumia maji kiasi gani na kulipa kulingana na kiasi cha maji wanayotumia.

Mheshimiwa Spika, Waziri ameshindwa kujibu barua aliyoandikiwa na manispaa  baada ya kumteua Diwani mmoja ili awe mjumbe Wa bodi ya maji na muwakilishi Wa wananchi katika bodi hiyo lakini Mpaka dakika hii waziri hajajibu kwahiyo idara ya maji inapanga itakavyo gharama za maji ilianza na shilingi 5,200 ikaenda shilingi 17,500 hadi shilingi 19,500 na sasa wanataka kupandisha Ankara hadi shilingi 23,000  kwa mwezi, huku ni kuwakomoa watu wa kigoma ,huu ni udhalilishaji  na dharau kwa wananchi na wakazi wa mkoa wa Kigoma, Mpaka sasa hatua zilizochukuliwa ni kwamba wenyeviti wa mitaa 68 wamechanga pesa kwa ajili ya kuishtaki body ya maji ya mkoa.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina juu ya utaratibu wa kupandisha bei za maji bila kuwashirikisha wadau ambao ni wananchi, kwani huku ni kwenda kinyume na sera ya maji.
6.3.  Mgogoro wa Maji-Goba
Mheshimiwa Spika, migogoro katika miradi ya maji ya wananchi haipo tu maeneo ya vijijini bali pia katika maeneo ya mijini ikiwemo katika Jiji la Dar es salaam. Mfano wa migogoro hiyo ni wa mradi wa wananchi wanaotumia maji katika kata ya Goba uliodumu kwa zaidi ya miaka mitano, na kusababisha wananchi kukosa huduma ya maji.
Vyanzo vya matatizo hayo ni pamoja na uendeshaji mbovu wa mradi wa maji chini ya kamati za maji unaosababisha kuibuka kwa tuhuma za mara kwa mara za ufisadi, malimbikizo ya madeni na kuharibika kwa miundombinu. Aidha, chanzo kingine kikubwa ni uwezo mdogo wa miradi hiyo ya maji ukilinganisha na ongezeko la idadi ya watu katika mitaa ya kata hiyo ambayo awali ilikuwa vijiji.

Mheshimiwa Spika, ili kushughulikia kasoro hizo tarehe 24 Oktoba 2011 Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni aliandikiwa barua ili  achukue hatua za dharura kutatua mgogoro huo na kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji; taarifa ya suala hilo ilifikishwa Wizara ya Maji, hata hivyo mgogoro huo umedumu mpaka hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani  inaitaka Wizara ya Maji kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni kuchukua hatua za haraka kufuatilia kwa dharura kuhakikisha maji yanarejeshwa Goba. Hatua hii iende sambamba na kupanua wigo wa maji Goba kwa kutekeleza kwa haraka upatikanaji wa maji kutoka pia mradi wa maji toka Madale Kisauke. Wizara ya Maji ishirikiane na Manispaa kuhakikisha matatizo yaliyopo yanatatuliwa kwenye miradi ya maji inayoendeshwa na manispaa pamoja na kamati za wananchi au vyama vya watumia maji katika maeneo mbalimbali.

7.0   UCHAFUZI WA VYANZO VYA MAJI
Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina vyanzo vikuu vya maji ambavyo ni mito mikubwa, maziwa, chemichemi na maji chini ya ardhi. Maji ya vyanzo hivyo ndiyo yatumikayo majumbani, viwandani, mashambani na kwa ajili ya mifugo. Maji yanayotumika toka ziwa Viktoria kwa kiasi kikubwa yanachafuka kutokana na viwanda kama vile vya kusindika kahawa, pamba, mafuta ya kula na viwanda vya sabuni na manukato bila kusahau viwanda vya samaki ambapo uchafu toka viwanda hivyo huelekezwa ziwani, au uchafu huelekezwa kwenye mito ambayo inaingiza maji yake ziwani. 
Mheshimiwa Spika, matumizi ya madawa ya kuchenjulia dhahabu yanayotumiwa na wachimbaji wadogo kwenye mito ambayo wakati wa masika maji hutiririka hadi ziwa Viktoria na mahali pengine kwenye mito mikubwa ambayo ni vyanzo vya maji ambayo maji yake yanatumika kwa matumizi ya majumbani.

Mheshimiwa Spika, kilimo cha matumizi ya mbolea na madawa ya viwandani kinachoendeshwa katika maeneo yaliyo karibu na vyanzo vikuu vya maji ni mojawapo ya vyanzo vya uchafuzi mkubwa wa vyanzo vyetu muhimu vya maji. 

Mheshimiwa Spika, kutokana na uvamizi wa vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira vipo vyanzo vya maji ambavyo vilikauka, kupungua maji na vingine kuchafuka na kutokufaa kama vile Ziwa Chala, Ziwa Jipe, mto Umba na ziwa Manyara.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali katika hili la matumizi ya mbolea za viwandani, katika uchafuzi wa vyanzo vya maji, suluhu ya hilo ni kuingia katika matumizi ya mbolea za asili kama vile mboji  au mbolea za na marejea  na mimie kama hiyo hasa kwa wakulima ambao wanafanya shughuli zao karibu na vyanzo vya maji.
Aidha, tunaitaka serikali kuweka mkakati mahususi wa kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinalindwa kikamilifu dhidi ya uchafuzi wowote na kama ikitokea viwanda vinahusika basi sheria ya mazingira itumike ili wahusika wawajibishwe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa  maoni hayo kwa niaba Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

……………………………………………
Sabreena Hamza Sungura (Mb)
k.n.y Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani-Wizara ya Maji.
09.07.2012

No comments:

Post a Comment