SERIKALI mkoani Kilimanjaro, imesema itaendelea kuunga mkono
mbio ndefu za Kilimanjaro Marathon, zitakazofanyika mkoani humo mwezi Machi
mwakani kutokana na umuhimu wake katika kuutangaza mlima Kilimanjaro, Mkoa wa
Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla.
Ahadi hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa huo
Leonidas Gama, wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo kwa mwaka 2013,
uliofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wanamichezo na wakazi
mbali mbali wa mji huo na Mikoa ya jirani.
“Mashindano ya kimataifa ya Kilimanjaro Marathon ni moja
wapo ya matukio muhimu katika kalenda ya michezo hapa nchini na ambayo imekuwa
ikiwavutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi hivyo hatuna budi sisi
kama serikali kuungana na wadau wengine katika kuhakikisha yanaendela kuwepo”,
alisema.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya
Moshi, Ibrahim Msengi, Gama alitoa changamoto kwa wanariadha na viongozi wa riadha hapa nchini kuhakikisha
wanatayarisha timu ambayo itawezesha watanzania kushinda mbio hizo
mwakani.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alitoa pongezi zake kwa wadhamini wakuu
wa mbio hizo Kilimanjaro Premium Lager
pamoja na wadhamini wengine kwa kuendelea kuunnga mkono uwepo wa mashindano
hayo kupitia udhamini mbalimbali.
Kwa upande wake meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambao ndiyo
wadhamini wakuu wa mashindano hayo George Kavishe, alisema watatoa motisha ya
zawadi ya shilingi milioni 3 ya ziada kwa wanariadha wa kitanzania
watakaoshinda mbio za 42 km Kilimanjaro Premium Lager Marathon. Hii ni kuwapa
moyo Watanzania waweze kufanya vizuri katika mbio hii ambayo inafanyika hapa
kwenye ardhi yao.
“Iwapo mwanariadha wa Tanzania awe wa kike au wa kiume
atashinda mbio hizo Machi, mwakani, mbali na zawadi ya kwanza ya shilingi mioni
tatu, ataongezewa milioni nyingine tatu”, alisema.
Alisema matokeo ya mbio zilizopita jana yaliibua changamoto
kubwa kwa wanariadha wa Tanzania, viongozi wa riadha na wadhamini wenyewe na
kwamba mwaka huu wadau mbalimbali wamejipanga kuhakikisha watanzania wanashika
nafasi ya kwanza mwakani.
Kawishe aliendelea kusema kuwa Kilimanjaro premium lager
itaendelea kudhamini mashindano hayo
muhimu ya kimataifa na ambayo alisema ymeiletea Tanzania heshima kubwa. Pia
aliwashukuru wadhamini shirikishi Vodacom, GAPCO, Tanga Cement, CFAO Motors, KK
Security, Keys Hotel, TPC Sugar, Shoprite, New Arusha Hotel na Kilimanjaro
Water kwa kuendelea kuziunga mkono mbio hizo.
No comments:
Post a Comment