Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dkt. Fenella Mukangara (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi
Msaidizi Mkaazi wa Shirika la Kazi Duniani, Bibi Hopran Fololo wakati
akimwelezea kuhusu utekelezaji wa mpango wa Ujasiriamali kwa Vijana
unaoendeshwa na Shirika hilo hivi karibuni Jijini Dar es Salaam. Wa kwanza
kushoto ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Dkt. Elisante Ole Gabrieln na
wengine ni wajumbe kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO). Picha na Concilia Niyibitanga, WHVUM
Na
Concilia Niyibitanga
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imelitaka Shirika la Kazi Duniani (ILO) kutunisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili vijana wengi waweze kukopa na kuanzisha miradi ya ujasiriamali.
Hayo yamesemwa hivi
karibuni na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella
Mukangara wakati akiongea na ujumbe kutoka Shirika hilo uliokuja ofisini kwake
kwa ajili ya kuzungumzia Mradi wa Ujasiriamali kwa vijana unaoendeshwa na
Shirika hilo.
Dkt. Mukangara pia
amelitaka ILO kupitia mradi huo kutoa mafunzo husika katika vituo vya Vijana
vya Sasanda, Marangu na Ilonga kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa vituo
hivyo.
Akielezea mpango huo,
Mkurugenzi Msaidizi Mkaazi wa Sh
irika hilo, Bibi Hopran Fololo amesema kuwa
wataanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana 225 waliomaliza Vyuo Vikuu
katika fani mbalimbali na baadae vijana hao watatakiwa kwenda vijijini
kuhamasisha vijana wenzao kuhusu elimu ya ujasiriamali na umuhimu wake.
Bibi Fololo amesema
kuwa Shirika kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
wanatarajia kuingiza elimu ya Ujasiriamali katika mitaala ya elimu ya Sekondari
na Vyuo vya Ualimu kwa lengo la kuwawezesha vijana kuhitimu wakiwa na elimu
hiyo jambo amabalo litawasaidia kujiajiri wenyewe.
Katika mradi huo wenye
lengo la kuibua fursa za ajira kwa vijana kupitia ujasiriamali shirika litatoa
mafunzo kwa Maafisa Vijana wa Wilaya nchi nzima ili waweze kuwaongoza vijana
ipasavyo katika sekta ya ujasiriamali. Ameongeza Bibi Fololo.
Aidha, Fololo amesema
kuwa Shirika litatoa ruzuku kwa baadhi ya miradi itakayobuniwa na vikundi vya
vijana ambapo vikundi vitashindanishwa na washindi kupatiwa ruzuku ya kuanzia
Dola 15,000 hadi Dola 20,000 kwa ajili ya kuendesha miradi yao.
Ameendelea kueleza kuwa
pamoja na kutoa ruzuku kwa vikundi vya vijana, watazisaidia pia taasisi za
fedha zinazokopesha vijana kwa kuzitunishia mifuko ili ziwe na uwezo wa
kukopesha vijana wengi zaidi.
Mradi huu unalenga
kuhamasisha vijana wapatao milioni moja na nusu katika maswala ya ujasiriamali
ili waweze kujiajiri wenyewe.
No comments:
Post a Comment