JAMII YATAKIWA KUJIHADHARI NA MATAPELI WANAOPITA MAOFISINI
KUWAHADAA VIONGOZI .
Serikali inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa
hivi karibuni kumezuka kundi la Watu wadanganyifu ambao wamekuwa wakitumia
majina ya viongozi waandamizi wa serikali na Taasisi nyeti ikiwemo Usalama wa
Taifa kujipatia fedha kwa madai ya
kutumwa na viongozi hao.
Watu hao wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa simu (SMS)
kwa maofisa mbalimbali wa wizara, mashirika ya umma na Idara za Serikali
zinazojitegemea kuomba pesa ili wawafanye mipango ya kupandishwa vyeo.
Utapeli huo umekuwepo nchini kwa kipindi kirefu
sasa , ambapo watu huwapigia simu viongozi wa Taasisi za fedha , Mifuko ya
Taasisi za Jamii na watu binafisi wakiomba fedha kwa madai ya kutumwa na
viongozi waandamizi Serikalini wakati si kweli.
Watu hao wamekuwa wakiwatapeli maofisa
mbalimbali kuwa wanaweza kuwafanyia mipango ya kupandishwa vyeo endapo watawapatia
kiasi cha fedha jambo ambalo halipo katika taratibu za utumishi wa umma.
Utumishi wa umma unazo taratibu zake za
kuwapandisha vyeo watumishi wake kulingana na sifa za kada zao na wala
haiwezekani kwa viongozi waandamizi kuwachangisha fedha kwa ajili ya
kuwapandisha vyeo.
Serikali inawataka wananchi kuwapuuza matapeli
hao na watoe taarifa katika vyombo vya dola na usalama mara wapatapo ujumbe wa
aina hiyo ili hatua zichukuliwe dhidi
yao.
IMETOLEWA
NA:
IDARA
YA HABARI (MAELEZO) DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment