DRFA yazipongeza Red
Coast, Abajalo, Friends Rangers
CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA),
kimezipongeza timu zake tatu zilizofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa, baada ya
kumalizika kwa Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora Aprili 27 mwaka huu.
Timu hizo ni Red Coast, Abajalo na Friends Rangers,
zitakazoungana na timu za mikoa mingine kucheza Ligi ya Mabingwa itakayoanza
Mei 12 mwaka huu chini ya Usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, alisema
ligi hiyo ilikuwa na ushindani wa hali ya juu na kuzitaka timu zilizofuzu hatua
hiyo kujipanga vizuri ili kuuwakilisha vyema mkoa na hatimaye kucheza Ligi
Daraja la Kwanza.
“Kwa niaba ya DRFA napenda kuchukua nafasi hii kuzipongeza
timu hizo kwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuuwakilisha mkoa wa Dar es
Salaam katika kutafuta kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao wa 2013/2014.
“Tunaamini watajiandaa vyema na kutuwakilisha vizuri katika
ligi hiyo, kufanya kwao vizuri ndio itakuwa fahari yetu DRFA na wadau wa mpira
wa miguu mkoa wa Dar es Salaam, tunawatakia kila la kheri na tupo pamoja katika
kushirikiana nao.
Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora mkoa wa Dar es Salaam
ilianza Aprili 15 mwaka huu ambapo ameziomba timu za Sharif Stars, Day Break na
Boom FC zilizoshiriki ligi hiyo kujiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano
yajayo.
No comments:
Post a Comment