MDAU POPOTE ULIPO TUMA PICHA NA HABARI KWA E-mail:  antonysiame74@yahoo.com

Friday, May 17, 2013

JESHI LA POLISI LAKANUSHA KUMWACHIA MTUHUMIWA WA UJANGILI.



(Na. Veronica Kazimoto – MAELEZO)
Dar es Salaam
16/05/2013.


Jeshi la Polisi mkoani Arusha limekanusha taarifa ya kuachiwa huru kwa mtuhumiwa wa ujangili  Bw. Frank William Silangei maarufu kwa jina la “Ojung’s Mwarusha” mkazi wa Ngaramtoni Kibaoni iliyotolewa na gazeti moja la kila wiki. 


Akizungumza katika mahojiano kwa njia ya simu na Idara ya habari MAELEZO leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas amesema kuwa mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 32  hivi sasa yuko mahabusu na taratibu za kumfikisha  mahakamani zinaendelea kufanyika.

Kamanda Sabas ameeleza kuwa  mtuhumiwa  Silangei hajaachiwa huru kama ilivyoripotiwa na gazeti  hilo linalotoka kila Alhamis katika ukurasa wake wa kwanza na wa pili na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo liko makini katika kutekeleza majukumu yake.

“Si kweli hajaachiwa, natamani ungekuwa hapa Arusha nikakupeleka mahabusu ukamuona mtuhumiwa kwa macho yako”, amesema Kamanda Sabas.

Kamanda Liberatus Sabas amesema Serikali kupitia Jeshi la Polisi  itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya ujangili vinatokomezwa na yeyote atakayehusika na vitendo hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.




No comments:

Post a Comment