Na Lydia Churi, MAELEZO-DODOMA
Watu milioni
mbili hufariki kila mwaka na asilimia nne ya matatizo ya kiafya duniani
hutokana na matumizi ya pombe.
Akijibu swali
bungeni mjini Dodoma Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Seleman
Rashidi alisema Serikali inawataka watanzania kutokutumia pombe kupita kiasi kwa
kuwa ina madhara kwa afya zao, familia na taifa kwa ujumla.
Alisema utafiti
unaonyesha kuwa tatizo hili ni baya zaidi katika nchi zinazoendelea kutokana na
hali mbaya ya uchumi na ustawi wa jamii inayochangiwa na magonjwa ya Malaria,
Kifua Kikuu na Ukimwi.
Alisema
utafiti uliofanyika nchini kati ya Februari na Oktoba 2012 kuhusu viashiri vya
magonjwa yasiyo ya kuambukiza umebaini kuwa asilimia 26.8 hadi 31.9 ya wananchi
wanatumia pombe na kati ya hao asilimia 27.4 ya wanaume ni walevi wa kupindukia
na wanawake ni asilimia 13.4.
Dkt. Rashidi alisema kutokana na kuongezeka
kwa athari zinazotokana na matumizi ya pombe hasa kwa magonjwa yasiyo ya
kuambukiza, Serikali inatekeleza mkakati wa kukabiliana na magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ambao unaelekeza kuhusu kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia
mbalimbali.
Alisema
Serikali imeanzisha utaratibu wa kuziwezesha hospitali za rufaa za mikoa kuanza
kutoa huduma kwa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya na pombe. Aliongeza
kuwa hivi sasa hospitali za kanda pia zimejiimarisha katika kutibu magonjwa
yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na waathirika wa magonjwa wa matumizi ya
pombe.
No comments:
Post a Comment